Israel-Gaza:Mashambulizi ya angani yatekelezwa na Israel huko Gaza

Iliyochapishwa

Israel imesema kuwa imeanzisha mashambulizi ya anga dhidi ya maeneo lengwa ya Hamas katika ukanda wa Gaza, kama njia moja ya kujibu kurushwa kwa maputo ya moto kuelekea upande wake .

Milipuko ilisikika katika mji wa Gaza alfajiri ya jumatano .

Maputo kadhaa ya moto yalirushwa kutoka upande wa Gaza kuelekea Israeli mapema Jumanne na kusababisha milipuko kadhaa kulingana na huduma ya zimamoto ya Israeli.

Hii ikiwa ni milipuko ya kwanza tangu kusitishwa kwa vita vilivyoendelea kwa siku 11 kati ya pande hizo mbili Mei 21.

Hilo limefuatia maandamanao yaliyofanywa na raia wa Kiyahudi katika eneo lililokaliwa la Jerusalem Mashariki Jumanne, ambayo yalikuwa yametishia upande wa Hamas, kundi la wanamgambo linaloendesha ukanda wa Gaza.

Tunajua nini kuhusu mashambulizi hayo?

Katika taarifa, wanajeshi wa ulinzi wa Israeli (IDF) walisema kuwa ndege za kivita zilivamia maeneo ya kijeshi yanayoendeshwa na Hamas katika miji ya Khan Yunis na Gaza

Pia taarifa hiyo imeongeza kuwa "shughuli za kigaidi" zilifanyika eneo hilo na kwamba wanajeshi wa Israeli walikuwa wamejitayarisha kwa "matukio yoyote yale, ikiwemo kuanza tena kwa mapigano kati yao ikiwa vitendo vya kigaidi kutoka upande wa Gaza vitaendelezwa".

Haikujulikana mara moja kama mashambulizi hayo ya anga yalisababisha majeruhi wowote.

Msemaji wa kundi la Hamas amesema katika taarifa yake kupitia mtandao wa Twitter kwamba raia wa Palestina wataendeleza "upinzani kwa dhati yote na kutetea haki zao na maeneo matakatifu" huko Jerusalem.

Huduma ya zimamoto ya Israeli ilisema maputo yanayolipuka yaliyorushwa mapema kutoka upande wa Gaza yalikuwa yamesababisha moto kwa maeneo yasiyopungua 20 katika maeneo ya jamii za kusini mwa Israeli.

Huu ndio ukabilianaji wa kwanza kivita tangu muungano mpya wa serikali ya Israeli kuingia madarakani wikendi iliyopita inayoongozwa na Naftali Bennett na kutamatisha utawala wa Benjamin Netanyahu aliyehudumu kama waziri mkuu wa nchi hiyo kwa miaka 12.

Makubaliano ya kusitisha mapigano ni tete

Mashabulizi ya anga ya hivi karibuni yalidumu kwa dakika 10 lakini kulikuwa na mengi ya kuamsha kumbukumbu za wenyeji wa mji huo ambao wanajitahidi kukabiliana na matokeo ya mapigano ya hivi karibuni kwamba makubaliano ya kusitisha mapigano ni tete.

Sio tu sauti za milipuko zinazokumbusha watu kwamba vita bado vipo bali unachohitajika kufanya ni kuendesha gari lako au kutembea katika mitaa ya mji huo kushuhudia uharibifu uliofanyika kwenye mji huo. Tani za vifusi bado zimeziba barabara kuu kitovu cha eneo la Gaza.

Mfanyabiashara katika eneo hilo, Abu Muhammad, anayeuza njugu katika eneo jirani la Rimal, ambalo lilikuwa lengwa kwenye mashumbulizi makubwa yaliyofanyika katika vita vilivyotangulia. Alisema: "Hatuwezi kuvumilia tena vita zaidi, janga la corona lilisitisha kazi zetu kwa miezi mingi tu, na vita vya hivi karibuni vimesababisha maafa makubwa kiasi kwamba sikuweza tena kulisha familia yangu ya watoto sita."

Jirani anayeishi karibu na eneo la jeshi la Hamas ambalo lililipuliwa katika mashambulizi ya hivi karibuni, alisema kwa njia ya simu ilikuwa inagopesha kutazama tena moto ukifuka juu kwenye anga.

Ni kipi kilichofanyika katika maandamano ya mwezi machi Jerusalem?

Zaidi ya waandamanaji 30 wa Kipalestina walijeruhiwa na watu 17 walikamatwa Jumanne wakati polisi wa Israeli walipotayarisha njia katika maeneo ya Mashariki mwa Jerusalem kwa maandamano hayo, wakirusha mabomu ya kuwatawanya watu na risasi za mpira.

Video kwenye mitandao ya kijamii inaonyesha baadhi ya waandamanaji wa Israeli wakiimba "kifo kwa Waarabu" kwa Wapalestina wa eneo hilo.

Maandamano ya bendera ya Siku ya Yerusalemu ni hafla ya kila mwaka inayoashiria kutekwa kwa Israeli kwa Yerusalemu Mashariki - makao ya Jiji la Kale na maeneo yake matakatifu - katika Vita vya Mashariki ya Kati vya 1967.

Hafla ya mwaka huu ilitarajiwa kufanyika Alhamisi iliyopita, lakini waandaaji waliifuta baada ya polisi wa Israeli kukataa njia iliyopendekezwa, wakitoa wasi wasi kuhusu usalama.

Baadaye ilikubaliwa na serikali ya mseto ya Israeli, lakini Waziri wa Mambo ya nje Yair Lapid alikosoa washiriki wa Israeli ambao waliimba nyimbo za kibaguzi na vurugu.

"Ukweli kwamba kuna watu wenye msimamo mkali ambao bendera ya Israeli inawakilisha chuki na ubaguzi wa rangi ni chukizo na haivumiliki," akasema Bw Lapid. "Haieleweki jinsi mtu anaweza kushika bendera ya Israeli mkononi mwake na kupiga kelele" kifo kwa Waarabu "wakati huo huo."

Ni kipi kimesababisha machafuko ya hivi punde?

Mapigano kati ya Israel na wanamgambo wa Kipalestina huko Gaza yalianza tarehe 10 Mei baada ya wiki kadhaa za mvutano uliotokea Mashariki mwa Jerusalem, ambao ulimalizika kwa mapigano huko al-Aqsa, eneo takatifu linaloheshimiwa na Waislamu na Wayahudi. Hamas ilidai Israeli iwaondoe polisi kutoka huko na wilaya iliyo karibu zaidi ya Kiarabu ya Sheikh Jarrah, ambapo familia za Wapalestina zinakabiliwa na tishio la kufukuzwa na walowezi wa Kiyahudi.

Hamas ilianza kufyatua roketi baada ya kuionya Israeli ijiondoe kwenye sehemu hiyo , na kusababisha mashambulizi ya kulipiza kisasi.

Jeshi la Israeli linasema zaidi ya roketi 4,300 zilirushwa kuelekea eneo lake na wanamgambo na kwamba ilishambulia zaidi ya sehemu 1,000 za wanamgambo huko Gaza.

Sitisho la mapigano baadaye liliafikiwa baada ya Misri na nchi zingine kuingilia kati , na kuanza kutumika mnamo 21 Mei.

Takriban watu 243, wakiwemo zaidi ya wanawake na watoto 100, waliuawa huko Gaza wakati wa vita, kulingana na wizara ya afya ya Gaza. Israeli imesema iliwauwa wapiganaji wasiopungua 225 wa Kipalestina.

Nchini Israeli, watu 12, pamoja na watoto wawili, waliuawa, huduma yake ya matibabu inasema.