TB Joshua: Jinsi Watanzania watakavyomkumbuka muhubiri wa Nigeria Temitope Balogon Joshua

TB Joshua

Chanzo cha picha, TB Joshua/Facebook

Iliyochapishwa

Kifo cha muhubiri maarufu wa Nigeria Temitope Balogon Joshua maarufu TB Joshua kiliwashangaza wengi duniani na kuwagusa Watanzani.

Kwa mujibu wa gazeti la The Citizen nchini Tanzania, taarifa ya kifo chake iliotolewa na kanisa lake la SCOAN ilisema kwamba TB Joshua alifariki siku ya Jumamosi usiku muda mfupi baada ya kukamilisha ibada ya kanisa .

Taarifa ya kanisa hilo ilisema: Mungu amemchukua muhudumu wake mtume TB Joshua nyumbani kama alivyopanga yeye mwenyewe. Hiki ndicho alichozaliwa kufanya , kuishi na kufa nacho.

Hatahivyo , taarifa hiyo haijaelezea sababu ya kifo chake huku ikiwaomba waumini wake kumuombea muhubiri huyo na kuipatia familia yake nafasi ya kuomboleza kifo cha mpendwa wao.

Juhudu za gazeti la The Citizen kuwasiliana na wawakilishi wa kanisa hilo hazikufua dau.

Gazeti hilo pia lilidai kufanya juhudi za kuwasiliana na waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa lakini simu yake haikujibiwa.

Hatahivyo , wakati msemaji wake Aboubacar Liongo alipoulizwa na gazeti hilo alisema kwamba Lowassa alikuwa anaomboleza kifo cha TB Joshua na angetoa taarifa kwa vyombo vya habari baadaye.

Ziara yake Tanzania

Muhubiri alikwenda Tanzania mara moja baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na kukutana na Hayati John Maguful na pia akakutana na viongozi wa upinzani.

Magufuli ni mmoja ya viongozi aliyetembelea kanisa lake nchini Nigeria
Maelezo ya picha, Magufuli ni mmoja ya viongozi aliyetembelea kanisa lake nchini Nigeria

Kulingana na the Citizen, alipowasili Novemba 4, 2015, alipokelewa na Hayati Magufuli, ambaye alikuwa rafiki yake na baadaye akakutana na rais wa zamani, Jakaya Kikwete kabla ya kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu Edward Lowassa, ambaye alikuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya Chadema.

Wakati wa mkutano wake na Lowassa, kulikuwa pia na baadhi ya viongozi wa upinzani akiwemo Mwenyekiti , Freeman Mbowe na wa NCCR Mageuzi, James Mbatia na Kada maarufu wa CCM , Kingunge Ngombare Mwiru.

Inasemekana TB Joshua alimtia moyo Lowassa , na kumtaka ashirikiane na wenzake katika upinzani ili aweze kushinda uchaguzi wa mwaka 2020.

Hatahivyo, Lowassa alirejea CCM mwaka 2019.

Edward Lowassa

Kabla hata TB Joshua kuwasili nchini humo, baadhi ya viongozi wa Tanzania walikuwa wametembelea kanisa lake nchini Nigeria.

Aliyetambuliwa kufanya hivyo zaidi ni Rais Magufuli ambaye alishiriki ibada katika kanisa lake mwaka 2011, akisema alishawishiwa na mchungaji huyo kugombea urais.

Lowassa kwa upande wake alitembelea kanisa la TB Joshua mwaka 2012, pamoja na Waziri wa fedha, Dkt Mwigulu Nchemba, ambaye alitembelea kanisa hilo mwezi Disemba, 2014, akiwa Naibu Waziri wa fedha.

Harusi ya binti yake

Tanzania itamkumbuka zaidi TB Joshua kwasababu binti yake Serah Joshua ameolewa na Mtanzania, Brian Moshi mjini Arusha.

Ndoa ya aina yake ilifungwa Tarehe 8 Mei, 2021 katika Kanisa Katoliki lililopo katika Unga Ltd na kufuatiwa na sherehe kubwa iliyofanyika katika katika ukumbi wa Arusha International Conference Center (AICC).

Wawili hao walifunga ndoa mara mbili katika kanisa la Kipentekoste la Nigeria na baadaye mjini Dubai katika milki za Kiarabu (UAE).

Je TB Joshua ni nani?

TB Joshua

Chanzo cha picha, TB Joshua /facebook

Muhubiri TB Joshua ni raia wa Nigeria kiongozi na mwanzilishi wa kanisa la SCOAN ambalo limekuwa likirusha matangazo yake mubashara katika runinga ya Emmanuel TV mjini Lagos kusini mwa Nigeria.

Alizaliwa kama Temitope Balogun Joshua mnamo tarehe 12 mwezi Juni katika jimbo la Ondo nchini Nigeria.

Kulingana na Mtandao wa kanisa lake la SCOAN , Joshua alikuwa ndani ya tumbo la mamake kwa miezi 15 kabla ya kuzaliwa kwake.

Joshua alisomea katika shule ya msingi ya St. Stephen Anglican {Ikare-Akoko, Nigeria 1971-1977} lakini aliwacha shule alipojiunga na shule ya upili baada ya mwaka mmoja na kufanya kazi katika shamba moja la kuku.

Akiwa shuleni alijulikana kama muhubiri mdogo kutokana na alivyokuwa akiipenda Biblia na uwezo wa kutabiri matukio yaliofanyika katika jamii yake , kulingana na mtandao wa SCOAN.

Alianzisha kanisa la SCOAN mwaka 1987 akiwa na waumini wachache kabla ya kanisa hilo kupanuka hadi kimataifa.

Mwaka 2009 TB Joshua alianzisha klabu ya kandanda kwa jina My people FC katika juhudi za kuwasaidia vijana.

Magufuli na muhubiri TB Joshua

Chanzo cha picha, Nation Media Group

Wanachama wawili wa timu hiyo Sani Emmanuel na Ogenyi Onazi walichezea Nigeria Golden mwaka 2009, katika kombe la dunia la wachezaji wasiozidi umri wa miaka 17.

Tayari wachezaji watatu wamepata ufadhili Ulaya kuwa wachezaji wa kulipwa nchini Sweden.

Kulingana na jarida la Forbes 2011 , Temitope Joshua ni muhubiri wa tatu tajiri nchini Nigeria akiwa na thamani ya $15m.