Wakazi wakimbia mji wa Lebanon huku Israeli ikionya kufanya mashambulizi
Jeshi la Israel latoa agizo la kuhamishwa kwa mji wa kusini wa Tiro - ikiwa ni pamoja na sehemu ya Wakristo - likisema litachukua hatua "kwa nguvu".
Muhtasari
- Katibu Mkuu wa Elimu Kenya abadilishwa
- Mtu mmoja uawa Kenya katika maandamana ya kupinga kituo cha Ebola cha Marekani
- Mwendesha mashtaka wa ICC asimamishwa kazi kwa tuhuma za unyanyasaji
- Vikosi vya Taliban vyashambulia waandamanaji wanaopinga sheria ya mavazi
- Gachagua kupinga uamuzi wa Mahakama katika Mahakama ya Rufaa
- Somalia yajibu baada ya refa wake wa FIFA kuzuiwa kuingia Marekani
- Wakazi wakimbia mji wa Lebanon baada ya onyo la Israeli
- Bunge la Seneti Kenya laamriwa kumlipa Gachagua milioni 50
- Tetesi za soka Jumanne: Tottenham wanaendelea na mazungumzo ili kumnasa Savinho
- Wahamiaji 300 waliokuwa wakielekea Uingereza watekwa nyara na kutishiwa kuondolewa figo zao
- Mwamuzi wa Fifa wa Somalia azuiwa kuingia Marekani
- Trump azomewa alipohudhuria mchezo wa mpira wa kikapu, NBA
- Vyombo vya habari vya Israel vyamkosoa Trump kwa kumtaka kujizuia kufanya mashambulizi
- Trump: Nilimwambia Netanyahu kwamba unaweza kuachwa peke yako kukabiliana na Iran
Moja kwa moja
Na Lizzy Masinga & Asha Juma
Habari za hivi punde, Katibu Mkuu wa Elimu Kenya abadilishwa
Rais William Ruto amemteua Katibu wa Elimu Profesa Julius Bitok kuwa Katibu Mkuu wa Utalii, huku Katibu Mkuu wa Utalii John Lekakeny Ololtuaa akichukua nafasi ya Wizara ya elimu.
Mabadiliko hayo yametangazwa katika taarifa ya rais iliyotolewa na Mkuu wa Wafanyakazi na Utumishi wa Umma Felix K. Koskei.
Kulingana na notisi hiyo, Bitok na Ololtuaa wamebadilishana wadhifa, Bitok akihamia kwenye Wizara ya Utalii na Ololtuaa akichukua jukumu la Elimu.
Ofisi ya Utendaji ya Rais ilisema mabadiliko hayo yaliidhinishwa na Rais Ruto na yataanza kutekelezwa mara moja.
Mabadiliko hayo yanajiri wakati sekta ya elimu ikikabiliwa na msururu wa matukio ya moto katika shule kadhaa nchini Kenya na zingine zikifungwa.
Mtu mmoja uawa Kenya katika maandamana ya kupinga kituo cha Ebola cha Marekani

Chanzo cha picha, Reuters
Mtu mmoja ameripotiwa kuuawa na wengine kadhaa kukamatwa wakati wa maandamano ya kupinga mipango ya kuanzisha kituo cha karantini cha Marekani kwa walioambukizwa virusi vya Ebola.
Wakaazi wa mji wa Nanyuki katika Kaunti ya Laikipia wamekuwa wakiandamana kupinga mradi huo, wakisema hawakushauriwa vya kutosha na kutaka kituo hicho kihamishwe.
Polisi walikabiliana na waandamanaji huko Nanyuki walioandamana kwa mara ya pili kupinga mipango ya kuanzisha kituo cha karantini ya Ebola cha Marekani karibu na Kambi ya Anga ya Laikipia.
Waandamanaji walikuwa wamepanga maandamano ya amani kuwasilisha ombi la kutaka kituo hicho kihamishwe, lakini hali ya wasiwasi iliongezeka baada ya polisi kuwazuia kufika eneo hilo.
Maafisa walifyatua gesi ya kutoa machozi na maji ya kuwasha ili kutawanya umati wa watu, huku waandamanaji wakiwasha moto na kuziba barabara.
Walioshuhudia wanasema mtu mmoja alipigwa risasi wakati wa machafuko hayo, ingawa polisi hawajathibitisha kisa hicho.
Ujenzi wa kituo hicho umesitishwa na Mahakama Kuu ukisubiri kusikilizwa kwa pingamizi la kisheria lililowasilishwa na makundi ya kutetea haki za binadamu.
Ghasia hizi zimetokea wiki moja tu baada ya watu wawili kuuawa kutokana na maandamano sawia na hayo katika eneo hilo.
Soma zaidi:
Mtu mmoja uawa Kenya katika maandamana ya kupinga kituo cha Ebola cha Marekani
Mtu mmoja ameripotiwa kuuawa na wengine kadhaa kukamatwa wakati wa maandamano ya kupinga mipango ya kuanzisha kituo cha karantini cha Marekani kwa walioambukizwa virusi vya Ebola.
Wakaazi wa mji wa Nanyuki katika Kaunti ya Laikipia wamekuwa wakiandamana kupinga mradi huo, wakisema hawakushauriwa vya kutosha na kutaka kituo hicho kihamishwe.
Polisi walikabiliana na waandamanaji huko Nanyuki walioandamana kwa mara ya pili kupinga mipango ya kuanzisha kituo cha karantini ya Ebola cha Marekani karibu na Kambi ya Anga ya Laikipia.
Waandamanaji walikuwa wamepanga maandamano ya amani kuwasilisha ombi la kutaka kituo hicho kihamishwe, lakini hali ya wasiwasi iliongezeka baada ya polisi kuwazuia kufika eneo hilo.
Maafisa walifyatua gesi ya kutoa machozi na maji ya kuwasha ili kutawanya umati wa watu, huku waandamanaji wakiwasha moto na kuziba barabara.
Walioshuhudia wanasema mtu mmoja alipigwa risasi wakati wa machafuko hayo, ingawa polisi hawajathibitisha kisa hicho.
Ujenzi wa kituo hicho umesitishwa na Mahakama Kuu ukisubiri kusikilizwa kwa pingamizi la kisheria lililowasilishwa na makundi ya kutetea haki za binadamu.
Ghasia hizi zimetokea wiki moja tu baada ya watu wawili kuuawa kutokana na maandamano sawia na hayo katika eneo hilo.
Mwendesha mashtaka wa ICC asimamishwa kazi kwa tuhuma za unyanyasaji

Chanzo cha picha, Reuters
Karim Khan, mwendesha mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, amesimamishwa kazi huku akisubiri kukamilika kwa uchunguzi kuhusu kesi inayomtuhumu kwa utovu wa nidhamu.
Uamuzi huo ulifanywa na kundi la ndani la usimamizi wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, na suala hilo pia limepelekwa kwa nchi 125 wanachama wa mahakama hiyo.
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ina makao yake makuu The Hague, Uholanzi.
Nchi wanachama wa mahakama hiyo zitapiga kura kuhusu mustakabali wa Bw. Khan katika kikao maalum kitakachofanyika "haraka iwezekanavyo." Ofisi ya Bodi ya Usimamizi ilisisitiza kwamba kusimamishwa kwake kazi sio maamuzi ya mapema ya matokeo ya mwisho ya kesi hiyo.
Karim Khan amekataa mara kwa mara madai yote ya utovu wa nidhamu wa kijinsia, na mawakili wake wameelezea uamuzi huo kama "usio halali, kinyume na kanuni za kesi inayoendeshwa kwa haki na uliokosa ushahidi."
Vikosi vya Taliban vyashambulia waandamanaji wanaopinga sheria ya mavazi

Chanzo cha picha, UGC
Vikosi vya serikali ya Taliban vimewatawanya waandamanaji wanawake katika mji wa Jibraeel magharibi mwa mkoa wa Herat ambako walifyatua risasi na vurugu zilizotokea zikasababisha vifo vya takriban watu wawili huku wengine sita wakijeruhiwa.
Katika video na picha za maandamano hayo baadhi ya waandamanaji wa kiume, waliojiunga na waandamanaji wa kike, wanaonekana wakijibu vurugu za vikosi vya Taliban kwa kurusha mawe.
Maandamano hayo yalifanyika asubuhi ya leo kwa wito wa wanawake kadhaa kupinga kile walichokiita "dhuluma," na wanaume kadhaa pia walijiunga nao.
Waandamanaji waliimba "Elimu, Kazi, Uhuru.
Maafisa wa serikali ya Taliban huko Herat walithibitisha kwa BBC kwamba takriban "watu watatu" walipelekwa hospitalini, lakini hawakusema chochote kuhusu waliokamatwa.
Hata hivyo, idadi kamili ya majeruhi bado haijulikani, na baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti idadi kubwa ya waliojeruhiwa.
Kwa mujibu wa mashuhuda waliozungumza na BBC, baadhi ya vikosi vya Taliban pia walikuwa wakiwafyatulia risasi "waandamanaji wa kike miguuni."
Msemaji wa kamandi ya usalama ya serikali ya Taliban mjini Herat aliiambia BBC:
"Vikosi vya usalama vimechukua hatua kwa mujibu wa wajibu wao wa kutoa usalama na kudumisha utulivu wa umma, na yeyote aliyevuruga usalama wa umma atachukuliwa hatua kulingana na sheria."
Soma zaidi:
Habari za hivi punde, Gachagua kupinga uamuzi wa Mahakama katika Mahakama ya Rufaa

Chanzo cha picha, EPA
Aliyekuwa Naibu Rais nchini Kenya Rigathi Gachagua, amesema kuwa atapinga uamuzi wa mahakama uliosema kuwa aliondolewa madarakani kwa njia ya halali na kusisitiza kuwa walitafsiri vibaya sheria na kulipa kishogo suala zima la haki.
Akisisitiza kuwa haki yake ya kusikilizwa ilikiukwa wakati wa mchakato huo, Gachagua ameahidi kuwasilisha pingamizi lake katika Mahakama ya Rufaa na vile vile, kutumia fursa zingine zote zilizopo ikiwa ni pamoja na Mahakama ya Juu Zaidi.
Gachagua alisema anaheshimu Idara ya Mahakama lakini hakubaliani na tafsiri ya mahakama kuhusu sheria katika kesi hiyo.
Alitangaza kuwa ataelekea katika Mahakama ya Rufaa.
"Tutakata Rufaa katika Mahakama ya Rufaa juu ya uamuzi huo na tunatumai haki itapatikana," alisema.
Gachagua alisema haki haikuzingatiwa wakati wa mchakato wa kuondolewa madarakani.
"Kanuni ya muda mrefu ya kisheria ya utaratibu wa haki na haki ya kusikilizwa bila upendeleo imetupiliwa mbali na kupuuzwa mchana kweupe. Ni siku ya huzuni iliyoje kwa wale ambao wamepitia haya siku za nyuma na wale ambao wanakabiliwa na hali kama hiyo siku zijazo," alisema.
Haya yanajiri baada ya majaji watatu wa Mahakama Kuu kutoa uamuzi jana Jumatatu kwamba mchakato wa kumuondoa madarakani kwenye Bunge na Seneti ulikuwa halali na kwamba uamuzi huo unasalia kuwa halali kwa mujibu wa Katiba.
Gachagua alisema kuwa timu yake ya wanasheria imepitia uamuzi wa Mahakama Kuu kwa kina na kubaini kile wanachoamini kuwa ni makosa ya kisheria na ukiukwaji ambazo ni sababu tosha za kuwasilisha kesi yake katika kukata rufaa.
Gachagua alikosoa vikali mahakama kwa kuunga mkono kuondolewa kwake licha ya kubaini kuwa mchakato wa Bunge la Seneti ulikuwa na dosari.
Alisisitiza kuwa mara baada ya mahakama kupata haki zake chini ya Ibara za 25, 47 na 50 za Katiba zimekiukwa, mchakato mzima wa kumuondoa madarakani ungetangazwa kuwa umebatilishwa.
Soma zaidi:
Somalia yajibu baada ya refa wake wa FIFA kuzuiwa kuingia Marekani

Chanzo cha picha, Getty Images
Serikali ya Somalia imesema "imehuzunishwa sana" na mazingira ambayo yamesababisha mwamuzi wa kimataifa wa Somalia, Omar Artan, kujiondoa kwenye mashindano ya Kombe la Dunia yanayotarajiwa kufanyika Marekani, Canada na Mexico.
Artan alikuwa amepangwa kuwa mwamuzi wa kwanza wa Somalia kuchezesha mchuano huo wa kandanda mkubwa zaidi duniani.
Katika taarifa iliyotolewa Jumanne, Wizara ya Vijana na Michezo ya Somalia ilisema juhudi za serikali, ikiwa ni pamoja na mazungumzo ya kidiplomasia zimeshindwa kumhakikishia Artan ushiriki katika mashindano hayo.
"Kwa uratibu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Shirikisho la Somalia, Wizara imefanya mazungumzo ya kidiplomasia na kuweka juhudi kubwa kuwezesha ushiriki wake katika mashindano ya FIFA na michezo mingine iliyopangwa kufanyika nchini Marekani.
Kwa bahati mbaya, pamoja na jitihada hizo, suala hilo bado halijapata ufumbuzi, na mwamuzi bado hawezi kusafiri," ilisoma taarifa hiyo.
Ikimuelezea Artan kama chanzo cha fahari ya taifa, serikali ilisema ushiriki wake kwenye jukwaa la kimataifa ungetoa fursa ya kuonyesha vipaji vya Somalia huku ikiimarisha sifa ya nchi katika michezo ya kimataifa.
"Kushiriki kwake katika jukwaa la kimataifa ni heshima na fursa kwa watu wa Somalia, na kunachangia katika kuimarisha sifa ya nchi na kuendeleza maendeleo ya michezo ya Somalia hadi viwango vya juu vya kimataifa," iliongeza taarifa hiyo.
Serikali ilithibitisha tena kumuunga mkono Artan na kusema itaendeleza maendeleo yake ya kitaaluma na ushiriki katika fursa za kimataifa za siku zijazo.
Soma zaidi:
Wakazi wakimbia mji wa Lebanon baada ya onyo la Israeli

Chanzo cha picha, Getty Images
Timu za ulinzi wa raia zinasaidia juhudi za uokoaji katika mji wa Tyre kusini mwa Lebanon baada ya Jeshi la Ulinzi la Israeli kutoa tahadhari kwa watu kuondoka, Shirika la Habari la Kitaifa linaloendeshwa na serikali linaripoti.
Kituo hicho kinaripoti kwamba makazi kwa ajili ya waliokimbia makwao yamejaa pomoni.
Jeshi la Israeli hapo awali liliwaonya watu kuhama na kuhamia kaskazini mwa mto Zahrani.
Watatu wauawa katika mashambulizi ya Israel kusini mwa Lebanon - ripoti
Vyombo vya habari vya Lebanon vinaripoti kwamba watu wasiopungua watatu wameuawa katika mashambulizi ya Israel kusini mwa Lebanon asubuhi ya leo.
Shirika la Habari la Kitaifa (NNA) linaloendeshwa na serikali lilisema waokoaji wa kwanza walipata mwili wa mtu mmoja baada ya majengo kadhaa kushambuliwa na mashambulizi ya anga ya Israeli katika eneo la mashariki mwa al-Massaken al-Shaabiya huko Tyre.
Tovuti ya L'Orient Today iliripoti kwamba watu wengine wawili hawakupatikana.
NNA ilisema watu wengine wawili waliuawa katika shambulio la ndege zisizo na rubani za Israeli kabla ya alfajiri katika mji wa Kfar Roumanne, ulioko milimani kaskazini-mashariki mwa Tyre.
Pia kumekuwa na mashambulizi ya anga asubuhi ya leo katika miji ya karibu ya Nabatieh na Kfar Sir, huku Jibchit ukishambuliwa na makombora ya mizinga, kulingana na NNA.
Siku ya Jumatatu, wizara ya afya ya Lebanon ilisema mashambulizi ya Israel kusini mwa Lebanon yaliwaua watu wasiopungua 14, wakiwemo saba katika wilaya ya Nabatieh na watano huko Tyre.
Soma zaidi:
Bunge la Seneti Kenya laamriwa kumlipa Gachagua milioni 50

Chanzo cha picha, Getty Images
Mahakama Kuu imeamuru Bunge la Seneti Kenya kumlipa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua KSh milioni 50 kama fidia ya kikatiba, ikibaini kwamba haki yake ya kusikilizwa kwa kesi ilikiukwa wakati wa kesi ya kumuondoa madarakani mnamo mwezi Oktoba 2024.
Jopo la majaji watatu linalojumuisha Jaji Eric Ogola, Jaji Anthony Mrima na Jaji Dkt. Freda Mugambi lilitoa amri hiyo kama sehemu ya uamuzi wa kihistoria hapo jana Jumatatu.
Mahakama ilitoa amri ya kwamba haki za Gachagua za kusikilizwa kwa kesi kwa njia ya haki zilikiukwa wakati Seneti ilipokataa kutoa idhini ya kuahirishwa kwa kesi hiyo licha ya kutokuwepo kwake Bungeni.
Mahakama ilisema kiwango hicho ni muhimu kama fidia na kama suluhisho la kikatiba.
"Mahakama inampa Mheshimiwa Gachagua fidia ya kikatiba ya shilingi milioni 50 za Kenya itakayolipwa na Seneti ili kudumisha utendaji unaozingatia Katiba, kurejesha heshima ya mhusika aliyeathiriwa, na kuzuia ukiukwaji wa siku zijazo," mahakama ilisema katika uamuzi wake.
Majaji walibainisha kuwa fidia hiyo ililenga kurejesha heshima ya Rigathi Gachagua na kutuma ishara wazi kwa vyombo vya serikali dhidi ya ukiukwaji wa haki wa siku zijazo.
Soma zaidi:
Tetesi za soka Jumanne: Tottenham wanaendelea na mazungumzo ili kumnasa Savinho

Chanzo cha picha, Getty Images
Tottenham wanaendelea na mazungumzo kuhusu dili la takribani £60m kwa ajili ya winga wa Manchester City, Mbrazili Savinho, mwenye umri wa miaka 22. (Mail)
Manchester United bado wana nia ya kumsajili Elliot Anderson, huku viongozi wa klabu wakiwa na matumaini ya kuipiku Manchester City katika mbio za kumnasa kiungo huyo Muingereza mwenye umri wa miaka 23, anayekadiriwa kuwa na thamani ya takribani £100m na Nottingham Forest. (Guardian)
Inasemekana Anderson ameonesha nia ya kujiunga na Manchester City badala ya Manchester United. (Talksport)
Atletico Madrid na FC Barcelona zipo katika nafasi nzuri ya kumsajili beki wa Chelsea Marc Cucurella, 26, ambaye anataka mabadiliko baada ya miaka minne Stamford Bridge. (Marca)
Newcastle United itamfuatilia kiungo wa Monaco, Lamine Camara, 22, endapo Sandro Tonali au Joe Willock wataondoka St James’ Park msimu huu wa joto. (Telegraph)
Macho ya skauti wa Manchester United yalimfuatilia mshambuliaji chipukizi wa Inter Milan, Pio Esposito, 20, alipokuwa akiichezea Italia dhidi ya Ugiriki katika mechi ya kirafiki. (Teamtalk)
Mshambuliaji wa Ufaransa wa Paris Saint-Germain, Randal Kolo Muani, 27, ambaye alicheza kwa mkopo Tottenham msimu uliopita, anataka kujiunga na Juventus. (Tuttosport)
Manchester City wanafikiria kumsajili winga wa Real Madrid Rodrygo, 25, na Iliman Ndiaye wa Everton na Senegal, 26. (Mail)
Beki wa kati Mreno Gonçalo Inácio wa Sporting yuko kwenye orodha ya Liverpool FC kama mbadala wa Ibrahima Konaté anayeondoka. (CaughtOffside)
Atalanta BC wanafanya mazungumzo na Nottingham Forest kumrudisha beki Nicolò Savona, 23, Serie A. (Goal)
AC Milan wanatarajiwa kufanya duru ya pili ya mazungumzo na kocha wa zamani wa Crystal Palace Oliver Glasner kuwa meneja mpya. (Calciomercato)
Wahamiaji 300 waliokuwa wakielekea Uingereza watekwa nyara na kutishiwa kuondolewa figo zao

Chanzo cha picha, Kurdish Regional Government
Zaidi ya wahamiaji 300 waliokuwa wakielekea Uingereza msimu uliopita wa kiangazi walitekwa nyara, kuteswa na kutishiwa kuondolewa viungo vyao kwa nguvu, BBC imebaini.
Wanaume hao vijana, wote kutoka Kurdistan ya Iraq, walikamatwa nchini Libya na kundi la wanamgambo ambao walidai fidia ya dola 5,000 kutoka kwa kila familia ya watu hao, na wakatishia kuwatoa figo ikiwa malipo hayatafanyika haraka.
Tumezungumza na baadhi ya mateka ambao waliachiliwa baadaye, na pia kuona ushahidi wa picha unaoonesha kuwa upasuaji wa kulazimishwa huenda ulifanyika.
Waliokuwa mateka walionesha ushahidi wa mateso, na walisema walikuwa wakishikiliwa katika mazingira duni sana, huku karibu watu 180 wakiwa kwenye seli moja.
Mateka mmoja ameripotiwa kufariki, na bado haijulikani ni wangapi wanaoendelea kushikiliwa.
Wanamgambo hao walipaswa kuwa wanawaongoza wahamiaji kupitia Libya hadi pwani ya Bahari ya Mediterania. Hata hivyo, mgogoro wa malipo ulizuka kati yao na msafirishaji haramu wa watu wa Kurd wa Iraq, Noah Aaron, ambaye alipanga safari hiyo ya wahamiaji.
Aaron kwa sasa anatumikia kifungo cha miaka 10 jela nchini Ufaransa kwa makosa tofauti ya utakatishaji fedha na usafirishaji haramu wa watu.
Maelezo kuhusu utekaji nyara huo yaliibuka wakati wa uchunguzi wa hivi karibuni wa BBC kuhusu msafirishaji mwingine wa watu, Kardo Jaf, ambao ulisababisha kukamatwa kwake mwezi uliopita.
Inaaminika kuwa wasafirishaji hao wawili walikuwa wakifanya kazi pamoja hapo awali. Wote wawili wanatoka katika mji wa Ranya huko Kurdistan ya Iraq, eneo ambalo limeelezwa kuwa “limejaa mitandao hai ya usafirishaji haramu,” kulingana na ripoti ya taasisi ya utafiti ya Uingereza, Chatham House.
Mwezi Februari, timu ya uchunguzi ya BBC ilikuwa ikifanya utafiti kuhusu Jaf mjini Ranya, wakati ilipofikiwa na mwanaume mmoja wa eneo hilo aliyesema kuwa mtoto wake alikuwa miongoni mwa vijana waliowekwa mateka.
Unaweza kusoma;
Trump azomewa alipohudhuria mchezo wa mpira wa kikapu, NBA

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Donald Trump amezomewa wakati wa mechi ya mpira wa kikapu mjini New York, akiwa Rais wa Marekani aliyeko madarakani wa kwanza kuhudhuria Fainali za NBA.
Vishindo vya kuzomewa vilisikika baada ya mashabiki waliokuwa na tiketi kulazimika kusubiri kwa saa kadhaa kwenye mistari mirefu zaidi nje ya Madison Square Garden kutokana na hatua kali za kiusalama zilizoambatana na uwepo wa rais.
Trump alihudhuria mechi kati ya New York Knicks na San Antonio Spurs katika mchezo wa tatu wa mfululizo wa fainali za NBA za michezo saba. Knicks walikuwa wameshinda michezo miwili ya kwanza.
Meya wa New York Zohran Mamdani na kundi la watu maarufu pia walihudhuria mchezo huo.
Tukio la kuzomea lilizuka Jumatatu jioni wakati kamera ilipomuonesha Trump kwenye skrini kubwa ndani ya uwanja, akiwa anatoa saluti wakati mwimbaji akiimba wimbo wa taifa.
Rais huyo alihudhuria mchezo huo akiwa na mjukuu wake Kai Trump na mmiliki wa New York Knicks, James Dolan, pamoja na baadhi ya maafisa wa utawala wake wakiwemo Waziri wa Uchukuzi Sean Duffy, Waziri wa Mambo ya Ndani Doug Burgum, mkuu wa EPA Lee Zeldin, na mjumbe maalum Steve Witkoff.
Rais huyo wa chama cha Republican, ambaye alizaliwa katika eneo la Queens mjini New York City, amekuwa na uhusiano mgumu na mji wake wa asili ambao kwa kiasi kikubwa unaunga mkono chama cha Democratic.
Mwamuzi wa Fifa wa Somalia azuiwa kuingia Marekani

Chanzo cha picha, Getty Images
Omar Artan, ambaye alikuwa anatarajiwa kuwa Msomali wa kwanza kuchezesha mechi katika fainali za Kombe la Dunia, ameondolewa kwenye orodha ya waamuzi baada ya kunyimwa kuingia nchini Marekani.
Artan, aliyekuwa Mwamuzi Bora wa Wanaume wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kwa mwaka 2025, alizuiwa kuingia nchini Marekani akiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Miami na kwa sasa yuko nchini Uturuki.
Hakuna sababu rasmi iliyotolewa na mamlaka za uhamiaji za Marekani kuhusu kurudishwa kwake, lakini Somalia ni miongoni mwa nchi kadhaa zilizowekwa kwenye orodha ya marufuku ya safari iliyowekwa na utawala wa Rais Donald Trump.
Baada ya kufanya mazungumzo na mamlaka za Marekani, shirikisho la soka duniani FIFA lilisema Artan hatashiriki kwenye michuano hiyo.
FIFA ilisema: “Tunaweza kuthibitisha kwamba mwamuzi Omar Abdulkadir Artan hataweza kuhudhuria mafunzo na kuchezesha Kombe la Dunia 2026 baada ya kunyimwa kuingia Marekani.”
FIFA iliongeza kuwa haijihusishi na taratibu za uhamiaji za nchi mwenyeji, ikiwa ni pamoja na utoaji wa visa, na imearifiwa na mamlaka kwamba hadhi ya Artan haitabadilishwa kwa sasa.
Kwa mujibu wa utaratibu wa awali wa mashindano ya FIFA, serikali ya nchi mwenyeji ndiyo hatimaye huamua nani anapata visa na nani anaruhusiwa kuingia nchini.
Mshauri mkuu wa Wizara ya Vijana na Michezo ya Somalia alithibitishia BBC kwamba Artan alinyimwa kuingia licha ya kuwa na nyaraka halali.
Afisa wa ubalozi wa Somalia mjini Nairobi aliiambia BBC kwamba pasipoti ya kidiplomasia ya Artan ilitolewa mahsusi kurahisisha safari yake baada ya changamoto za awali za visa.
Shirikisho la Soka la Somalia (SFF) limewasiliana na FIFA likitaka ufafanuzi wa haraka.
Akizungumza na BBC World Service, Andrew Giuliani, anayesimamia Kikosi Kazi cha Ikulu ya Marekani kuhusu Kombe la Dunia, alisema: “Ingawa siwezi kuingia kwa undani kuhusu taarifa hizo, naweza kukuambia kwamba ilikuwa uamuzi sahihi wa mamlaka za forodha na ulinzi wa mipaka na naunga mkono uamuzi huo.”
Artan alikuwa miongoni mwa waamuzi 52 waliotangazwa na FIFA kuchezesha fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Canada, Mexico na Marekani kuanzia Juni 11 hadi Julai 19.
Akiwa mmoja wa waamuzi wa ligi ya taifa ya Somalia, Artan alikua mwamuzi wa FIFA mwaka 2018 na pia amewahi kuchezesha michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Unaweza kusoma;
Vyombo vya habari vya Israel vyamkosoa Trump kwa kumtaka kujizuia kufanya mashambulizi

Chanzo cha picha, Jim WATSON / AFP via Getty Images
Vyombo vya habari vya Israel vimemkosoa Rais wa Marekani Donald Trump kwa kuitaka Israel kutofanya mashambulizi dhidi ya Iran, huku Israel ikiendelea kushambulia Iran licha ya wito huo.
Baadhi ya wachambuzi wanaona tofauti hizi za hadharani kuwa sehemu ya mkakati mgumu wa kusimamia mvutano huo.
Tarehe 7 Juni, Israel ililenga makao makuu ya Hezbollah katika kitongoji cha Beirut, hatua iliyosababisha Iran kurusha makombora dhidi ya Israel na kisha Israel kujibu mashambulizi hayo.
Gazeti la kiliberali la Haaretz liliripoti kwamba Israel ilishambulia Iran “licha ya ombi la Trump kwa Netanyahu.”
Ingawa Israel na Iran wameepuka mashambulizi ya moja kwa moja dhidi ya kila mmoja tangu mwanzoni mwa Aprili, Benjamin Netanyahu amekuwa akisisitiza mara kwa mara haja ya kurejea kwenye mzozo, jambo linaloibua swali iwapo makubaliano kati ya Marekani na Iran yanaweza kuzuia kikamilifu mpango wa nyuklia wa Iran na pia kutimiza matarajio ya Israel.
Barak Ravid, mwandishi wa masuala ya kidiplomasia wa Channel 12, alimnukuu afisa mwandamizi wa Marekani na chanzo cha Israel wakisema kwamba Trump alimwambia Netanyahu katika simu: “Usijibu mashambulizi ya makombora ya Iran na ipe diplomasia siku kadhaa zaidi.”
Gazeti la Haaretz liliandika kwamba: “Asubuhi ya leo ilibainika wazi kuwa juhudi hizo zimeshindwa na kwamba Israel imeishambulia Iran,” likiongeza kwamba pia kombora la balistiki lilirushwa kutoka Yemen.
Gazeti la Ma’ariv lilitangaza kwamba Israel ina haki ya kujilinda “kwa nguvu, kwa uthabiti na bila kusita” dhidi ya mashambulizi ya makombora ya Iran, huku likikosoa taarifa kwamba Donald Trump alijaribu kuizuia Israel kujibu mashambulizi hayo. Gazeti hilo liliongeza kuwa Marekani inapaswa kuunga mkono hatua za Israel katika mzozo wa pamoja, badala ya kuzuia hatua hizo.
Unaweza kusoma;
Trump: Nilimwambia Netanyahu kwamba unaweza kuachwa peke yako kukabiliana na Iran

Siku moja baada ya Iran na Israel kufanya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya kila mmoja, Donald Trump alizungumza na vyombo vya habari kwa kina kuhusu juhudi zake za kujaribu kusitisha mzozo huo.
Trump alisema kwamba alimuonya Waziri Mkuu wa Israel katika simu siku ya Jumapili kwamba “huenda hivi karibuni akabaki peke yake dhidi ya Iran.”
Marekani pia ilitangaza jana kwamba “haikuhusika” katika mashambulizi ya Israel ya anga na makombora dhidi ya Iran.
Baada ya wasiwasi kuongezeka kuhusu uwezekano wa vita vikubwa zaidi vya moja kwa moja katika Mashariki ya Kati, Iran na Israel zilitangaza Jumatatu kwamba zitasitisha operesheni za kijeshi dhidi ya kila mmoja.
Unaweza kusoma;
Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu za leo











