Mzozo wa Israel na Wapalestina : Netanyahu asema wanamgambo 'wamerejeshwa nyuma kwa miaka mingi'

There were protests, some of them violent, across the West Bank

Chanzo cha picha, Reuters

Iliyochapishwa

Mashambulizi ya siku kumi ya Israeli huko Gaza "yamerudisha nyuma Hamas kwa miaka mingi", Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu amesema.

Wafanyikazi wawili wa kigeni wa shamabani waliuawa na roketi zilizorushwa na wanamgambo wa Palestina kusini mwa Israeli Jumanne.

Israeli iliendeleza mashambulio yake ya anga huko Gaza. Katika Ukingo wa Magharibi, angalau Wapalestina watatu waliuawa na polisi wa Israeli wakati wa maandamano karibu na Ramallah.

Jitihada za kidiplomasia kumaliza vurugu hazikufanikiwa sana.

Ufaransa imewasilisha azimio kwa Baraza la Usalama la UN, kwa kushirikiana na Misri na Jordan, ikitaka kusitishwa kwa mapigano.

Mapema Jumanne, Israeli ilifungua kwa muda mfupi mpaka unaovuka kwenda Gaza ili kuruhusu msafara wa misaada kuingia. Walakini, mpaka huo ulifungwa tena baada ya kushambuliwa na roketi zinarushwa kutoka Palestina .

Netanyahu amesema nini?

Bwana Netanyahu alisema Hamas, kundi la wanamgambo wa Kipalestina linalosimamia Gaza, lilikuwa limeshughulikiwa "mapigo yasiyotarajiwa" na kwamba operesheni "zitaendelea kwa muda mrefu ili kurejesha utulivu" kwa raia wote wa Israeli.

Takriban watu 215, wakiwemo karibu wanawake 100 na watoto, wameuawa huko Gaza hadi sasa, kulingana na wizara yake ya afya.

Nchini Israeli watu 12, pamoja na watoto wawili, wameuawa, huduma yake ya matibabu inasema.

Siku ya Jumanne Israeli ilisema angalau wanamgambo 150 walikuwa miongoni mwa waliouawa huko Gaza. Hamas haijatoa takwimu za majeruhi kwa wapiganaji.

Netanyahu

Chanzo cha picha, EPA

Israeli ilikadiria kuwa mwanzoni mwa mzozo, vikundi viwili vya wanamgambo wa Palestina vilikuwa na silaha ya roketi karibu 12,000 huko Gaza.

Kuanzia saa 15:00 GMT siku ya Jumanne, wanamgambo walikuwa wamerusha maroketi takriban 3,300 nchini Israeli, ambayo 450 hadi 500 hayakufika malengo yake , na kusababisha majeruhi huko Gaza, msemaji wa jeshi la Israeli alisema.

Nini kilifanyika West Bank?

Wapalestina wengi katika Ukingo wa Magharibi na Jerusalem ya Mashariki walishiriki katika maandamano ya kupinga mabomu ya Israeli dhidi ya Gaza. Maeneo ndani ya Israeli yenye idadi kubwa ya Waarabu wa Israeli, kama Haifa, pia yalijiunga na maandamano hayo

Huduma za umma, shule na biashara nyingi zilifungwa.

Kulikuwa na mapigano katika maeneo kadhaa. Katika mji wa Ramallah Ukingo wa Magharibi, polisi wa Israeli walisema walifyatuliwa risasi wakati wa "ghasia kali" na wakajibu kwa kufyatua risasi .

mashambulizi

Chanzo cha picha, Reuters

Wapalestina watatu katika eneo hilo waliuawa, wizara ya afya ilisema. Mpalestina mwingine aliuawa baada ya kujaribu kushambulia wanajeshi huko Hebron, jeshi la Israeli limesema.

Kulikuwa pia na machafuko katika Lango la Damascus huko Yerusalemu, ambapo wanajeshi wa Israeli waliwakamata watu kadhaa

Ni kipi kilichofanyika katika kivuko cha mpakani?

Mapema Jumanne, Israeli ilifungua kivuko cha Kerem Shalom ili kuruhusu misaada kuingia Gaza. Umoja wa Mataifa ulikaribisha uamuzi huo, lakini pia ulihimiza Israeli kufungua njia kuu ya Erez, ili wafanyikazi wa kibinadamu, pamoja na vifaa, waweze kuingia.

Walakini, wakati msafara wa malori ya msaada ulipoingia Gaza, wapiganaji wa Palestina walirusha roketi katika eneo hilo. Raia wawili wa Thailand wanaofanya kazi kwenye shamba umbali wa kilomita 14 (maili tisa) kutoka mpakani waliuawa.

Ili kujibu hilo , Israeli ilifunga tena njia hiyo. Askari wa Israeli karibu na Erez alijeruhiwa kidogo, jeshi lilisema.

Wakati huo huo katika kivuko cha Rafah na Misri, sehemu pekee ya kuingia Gaza isiyodhibitiwa na Israeli, msafara tofauti wa malori 15 zilizobeba mafuta na 18 zilizobeba chakula na dawa ziliingia katika eneo hilo.

Diplomasia haijapiga hatua

Katika taarifa, Ufaransa ilisema azimio lake la Baraza la Usalama lilitungwa wakati wa mkutano wa video na kiongozi wa Misri Abdel Fattah al-Sisi na Mfalme Abdullah wa II wa Jordan.

Marekani imezuia majaribio ya hapo awali ya kutoa taarifa ya pamoja ya Baraza la Usalama inayotaka kusitishwa kwa vita mara moja.

Marekani , EU na mamlaka zingine zimetaka kumaliza mzozo. Misri imekuwa ikitafuta kupatanisha kati ya Israeli na Hamas.

Walakini, Israeli imesema itaendelea na mashambulizi kwa sasa, katika juhudi za kuharibu uwezo wa Hamas na Islamic Jihad.

Wakati huo huo, Marekani imemtumu Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kwa kutoa matamshi ya uchochezi juu ya Israeli.

Alishutumu Israeli kwa "ugaidi" dhidi ya Wapalestina na hivi karibuni alisema: "Ni katika asili yao". Halafu aliita Israeli "wauaji".

Nini kilisababisha mapigano?

Mapigano kati ya Israeli na Hamas yalisababishwa na siku kadhaa za kuongezeka kwa mapigano kati ya Wapalestina na polisi wa Israeli kwenye uwanja mtakatifu wa kilima huko Mashariki mwa Yerusalemu.

Eneo hilo linaheshimiwa na Waislam wote, ambao huiita Haram al-Sharif (Patakatifu Pema), na Wayahudi, ambao kwao linajulikana kama Mlima wa Hekalu. Hamas ilidai Israeli iwaondoe polisi kutoka huko na wilaya iliyo karibu zaidi ya Kiarabu ya Sheikh Jarrah, ambapo familia za Wapalestina zinakabiliwa na hatari kufukuzwa na walowezi wa Kiyahudi. Hamas ilizindua makombora wakati makataa yake hayakutiliwa maanani.

ramani

Hasira ya Wapalestina tayari ilikuwa imepanda baada ya wiki kadhaa za mvutano ulioongezeka huko Mashariki mwa Jerusalem, uliowashwa na mfululizo wa makabiliano na polisi tangu katikati ya Aprili.

Ilichochewa zaidi na sherehe ya kila mwaka ya Israeli ya kuadhimisha kudhibiti Yerusalemu ya Mashariki katika vita vya Mashariki ya Kati vya 1967, inayojulikana kama Siku ya Yerusalemu.