Siku ya akina mama Duniani: Changamoto za kuwa mama aliyehudumia kifungo jela

Chanzo cha picha, Cyprine
- Author, Anne Ngugi
- Nafasi, BBC Swahili
- Iliyochapishwa
Kuna msemo unaosema kwamba matatizo yanapoanza kutiririka katika maisha ya mtu , huingia kwa kishindo.
Msemo huu umedhihirika katika maisha ya Bi. Cyprine Omollo mama mwenye umri wa miaka 44 mwaka huu .
Mwanamke huyo anasimulia kwamba alipitia mateso na dhiki baada ya kufungwa gerezani.
Anaelezea kwamba mvua ya mateso pamoja na dhiki ilianza kumpiga alipowekwa katika rumande ya gereza kuu la wanawake jijini nairobi baada ya kushindwa kulipa deni.
Hatahivyo anasema kwamba kilichomgusa kabisa ni ni kulazimishwa kumuacha mtoto wake wa miaka minne huku mume wake akifariki akije gerezani.
" Tukio la pili nililazimika kumuacha mtoto wangu wa kike wakati huo akiwa na miaka 4 ili kukaa rumande , huku la nne mume wangu akifariki wakati nilipokuwa jela."anakumbuka Cyprine .

Chanzo cha picha, Cyprine Omollo
Na huku dunia inapoadhimisha siku ya akina mama duniani , kwake mama Cyprine ni wakati wa kutathmini na kurejesha mawazo yake nyuma katika matukio hayo ambayo nusura ya mpe ugonjwa wa kiakili.
Mwanamke huyu amekiri kupata sonona akiwa gerezani hasa kwa kumfikiria binti yake aliyekuwa mikononi mwa watu wa jamii yake .
Siku ya kimataifa ya akina mama hulenga kushabikia akina mama kwa juhudi zao za kutunza na kulea jamii bora .
Lakini kwake Cyprine anakabiliwa na changamoto ya kuishabikia siku hii muhimu kwa wanawake kutokana na yale aliopitia.
Changamoto ya pili inakuja baada ya kuachiliwa gerezani - na jinsi watoto watakavyokupokea nyumbani mbali na kwamba je ndoa zao zitasimama kama walivyoziwacha?
Safari ya kwenda gerezani ilianzia wapi?
Mwaka wa 2013 , Cyprine alikuwa anadaiwa na watu wake wa karibu, deni ambalo alilazimika kulilipa kwa kutoa jasho jingi na machozi .
Wakati huo mume wake waliokuwa wameishi naye kwenye ndoa kwa miaka miwili alianza kuugua ugonjwa wa moyo .
Ilimlazimu mama huyo kuchukua majukumu yote kuhakikisha kuwa jamii yake inaisha vyema.
Lakini kwasababu alikuwa na matatizo ambayo yalikuwa yakimzonga kila pembe alishindwa kulilipa deni lile , hivyo basi sheria ikachukua mkondo .
Alikamatwa na kuwekwa rumande ghafla hadi pale ambapo angeweza kulipa deni lake .

Chanzo cha picha, cyprian Omollo
Nyumbani alimuacha binti yake wa miezi minne na mume wake akiwa anapambana na maradhi sugu ya moyo .
Kama mama alishindwa la kufanya kwani uhuru wa kuamua au kufanya chochote ulikuwa haupo .
Akiwa gerezani alianza maisha ya kuwa mfungwa , huku bintiye akiwekwa mikononi mwa malezi ya dada yake Cyprine.
Hatahivyo hali ya maisha aliokuwa akipitia gerezani ilikuwa ni msimu wa kiza kikuu .
Miezi minne baada ya kuwekwa rumande mume wake aliaga dunia huku Cypriane akikosa kupata fursa ya kumzika mume wake .
Kulingana na mwanamke huyo ulikuwa wakati mgumu kuwahi kutokea katika maisha yake.
Anasema kwamba akiwa gerezani alipoteza ajira yake baada ya muajiri wake kugundua kwamba alikuwa akikabiliwa na kesi iliomuweka rumande.
"Hakuna siku katika maisha yangu niliwahi fikiria kuwa ningefika chini kiasi nilipokuwa ,nakumbuka siku yangu ya kwanza gerezani , niliamrishwa kuzivua nguo zangu zote , nikiwa nasubiri kupewa sare ya kuwa mfungwa huku vurugu ikiibuka katika jela ambapo wanawake wafungwa walikuwa wanapigana.'', alkisema

Chanzo cha picha, Cyprian Omollo
Aliongezea kwamba : Kelele na nduru zilitanda kote , kabla ya walinzi kupiga risasi hewani . hatua ilionyamazisha ghasia zile.
Anasema kwamba ni wakati huo alipojiuliza moyoni iwapo hayo ndio yaliokuwa maisha yake mapya gerezani.
Kulingana na bi Cyprine wakati mwingi alikuwa anawaza sana kuhusu binti wake .
Anasema kwamba alijiuliza maswali kama ; "Je mtoto wangu ananikumbuka? Je mimi ni mama wa aina gani kuwa gerezani huku mtoto wangu akiwa mikononi mwa watu wengine? "
Ama kwa kweli ni maswali ambayo alikosa majibu yake .
Cyprine anasema kuwa alijifunza maisha ya gerezani kwa haraka mno.
Anasema kitu kimoja muhimu alichojifunza ni kwamba mfungwa akiwa rumande huishi na wasiwasi wa ni lini kesi yake itasikilizwa na kukamilika.
Wakati mwingi Cyprine anasema kuwa ilibidi apumbaze muda wake mwingi kwa kusoma vitabu kwenye maktaba ya wafungwa mara kwa mara huku pia akiimba nyimbo za maombi.
Baada ya miezi 6 akihudumia kifungo gerezani , mara akaangukiwa na bahati, mlalamishi wa kesi yake hakurudi tena mahakamani hivyobasi akaachiliwa baada ya kesi kutupiliwa mbali.
"Bila shaka nilibubujikwa na furaha kwa kuwa nilitamani nimuome binti yangu , ila nilifahamu kuwa maisha hayangekuwa kama yalivyokuwa tena baada ya kifo cha mume wangu " anasema Cyprine
Cha kwanza alichokifanya alipotoka gerezani ni kukutanishwa na binti wake .
Cyprine anasema kuwa mojawapo ya wakati uliokuwa mgumu ni kukutana na bintiye baada ya kutoka gerezani .
Lakini cha kuvunja moyo kabisa ni kwamba uamuzi wa uchungu wa yeye na bintiye kutoishi pamoja ulifanywa.
Mwanawe tayari alikuwa akiishi na binamu yake ,lakini miaka sitaa baadaye uhusiano wake na mwanawe uliimarika na kurudi kama ulivyokuwa, lakini bado hangeweza kuishi naye kwa kuwa kwani bado alikuwa akiishi kwa dadake.

Chanzo cha picha, cyprine Omollo
Wakati dunia inawapa hongera kina mama kwa kuwa kiunganishi thabiti cha ustadi wa jamii , Cyprine anawakilisha kina mama wengi duniani ambao aidha wako gerezani wakati huu , au ambao wametumikia vifungo na sasa wamerudi kutangamana katika jamii .
Mama huyu anakiri sio rahisi kutangamana katika jamii kama mama anayetoka gerezani .
Mradi wa kufanyakazi na akina mama wafungwa
Kutokana na mapenzi yake ya kuwasaidia wanawake wanaotoka jela kurejea katika maisha yao ya kawaida , alijiunga na shirika moja kwa jina Clean Start Kenya , Shirika ambalo limesaidia makumi ya wanawake na wasichana wanaofungwa, kujiamini na kuendeleza maisha yao baada ya kutumikia vifungo vyao. Cyprine hivi sasa ni Meneja msimamizi na amewasaidia wanawake wengi ambao waliwaacha watoto wao , walipofungwa , kuanzisha maisha yao upya .
.












