Virusi vya Corona: Kwanini baadhi ya nchi za Afrika hazijatumia chanjo zote walizopokea?

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Peter Mwai
- Nafasi, BBC Reality Check
- Iliyochapishwa
Licha ya kwamba mataifa mengi ya Afrika yanapata wakati mgumu kupata chanjo za kutosha za Covid-19, baadhi ya mataifa yana maelfu ya dozi zilizoisha muda wake na hazikuweza kutumika.
Mataifa gani yana chanjo ambazo hazitumiki?
Malawi imebaki na chanjo 16,400 za dozi ya Oxford-AstraZeneca, huku Sudan Kusini ikiwa ina dozi 59,000 -ambazo zote muda wake wa matumizi uliisha Aprili 13.
Mataifa yote mawili yameamua kuteketeza mzigo huo wa chanjo ambao ulitolewa msaada na Umoja wa Afrika, ingawa Shirika la Afya Duniani (WHO) iliwataka wazihifadhi wakati wakichunguza kama muda wa matumizi unaweza kuwa salama kuongezwa.

Chanzo cha picha, Reuters
Kwa upande wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, imesema haiwezi kutumia dozi zote milioni 1.7 za Oxford-AstraZeneca ambazo walipokea chini ya mpango wa dunia wa Covax, kwa mataifa maskini.
Ni dozi zipatazo 1,000 tu ndio zimetumika mpaka kufikia mwisho wa mwezi wa Aprili.
Na nyingi zikiwa zinatarajiwa kuisha muda wake ifikapo Juni 24 - na sasa zinapelekwa Togo na Ghana, miongoni mwa mataifa ambayo tayari wametumia chanjo za awali.
Kwanini chanjo hizo hazijatumika?
Chanjo ya Oxford-AstraZeneca inaweza kuhifadhiwa salama kwenye jokofu kwa muda wa miezi sita baada ya kutengenezwa.
Na Umoja wa Afrika inasambaza chanjo ambayo ilipelekwa Afrika Kusini mwezi Februari ikiwa inatakiwa kumaliza muda wake Aprili 13.
Serikali ya Afrika Kusini iliamua kutotumia chanjo hiyo ikiwa na wasiwasi juu ya kuwa na kinga ya kutosha ya virusi vilivyotokea nchini humo.
Mwishoni mwa mwezi Machi, dozi milioni moja za chanjo ziliuzwa kwa Umoja wa Afrika ili kuwapa mataifa mengine ya Afrika.
Lakini baadhi ya mataifa hayo kama Sudan Kusini, imesema ilikuwa haifahamu kuhusu dawa hiyo kuisha muda wake.
Nigeria,imesema haitaweza kutumia dozi zote kwa wakati.
Hivyo nyingine zimepelekwa Togo na Ghana.
Na nyingine zilipelekwa Jamaica.
WHO imesema kuwa ni Togo na Gambia peke yake ndio zimethibitisha kutumia dozi zote walizopokea kabla ya tarehe ya mwisho ya matumizi ya dawa hizo.
Na taarifa kuhusu nini kilitokea kawa nyingine bado hazijatolewa.
Nini kimesababisha ucheleweshwaji wa matumizi ya chanjo?
Mataifa mengi walishindwa kujiandaa vizuri kabla ya kupokea chanjo hizo, Phionah Atuhebwe, kutoka WHO barani Afrika anasema.
"Hiyo ni sababu moja inayosababisha usambazaji wa chanjo kuchelewa," amesema.
Na baadhi ya mataifa yanakabiliana na changamoto za kifedha.
Mkuu wa kituo cha kudhibiti magonjwa barani Afrika John Nkengasong amesema mataifa yanahitaji kuungwa mkono kwa kuongeza idadi ya wafanyakazi wa afya na kupata vifaa kinga vya afya.
Na wale ambao chanjo zao zinazokaribia kumalizika muda wake wa matumizi au zimepita muda inabidi kuwasiliana na Shirika la Afya Duniani WHO au kituo cha kudhibiti magonjwa Afrika CDC.
"Bara hili kwa ujumla linafahamu jinsi ya kutoa chanjo na limekuwa likitoa chanjo kwa magonjwa mengine," amesema.
"Lakini la muhimu hapa ni jinsi ya kujipanga na kutoa kwa uharaka-?"

Chanzo cha picha, Reuters
Kwa DRC,ambayo ilikuwa inafahamika kama Zaire, tatizo halipo kwenye upungufu huduma za afya pekee bali pia mtando mbovu wa usafirishaji hivyo inawawia vigumu kusafirisha chanjo katika maeneo ya pembezoni yaani vijijini.
Na hali ikawa mbaya pale taifa hilo lilipositisha kutoa ya chanjo ya Oxford-AstraZeneca katikati ya mwezi -Machi, ikiwa na hofu ya usalama wa chanjo hiyo na kurudi kuendelea kuitoa Aprili 19, zaidi ya mwezi mmoja baadae.
Vipi kuhusu ubora wa chanjo?
Baadhi ya wataalamu na wanasiasa wamelalamikia kuhusu wasiwasi wa usalama na ubora wa chanjo kwa ujumla katika mataifa mengi ya Afrika lakini ni ngumu kuainisha athari zilizojitokeza.
"Ilichukua muda kuwashawishi watu, "Waziri wa afya wa Sierra Leone Austin Demby ameiambia BBC News
"Hivyo si suala la ubora wa chanjo tu."

Chanzo cha picha, Reuters
Mtaalamu wa afya wa Malawi Gama Bandawe amesema watu kutoamini ubora wa chanjo imechangia sehemu kubwa katika taifa hilo kushindwa kutumia chanjo zote ambazo walizipokea.
Na maamuzi ya Afrika Kusini ya kusitisha chanjo ya Oxford-AstraZeneca, kwa wasiwasi wa watu kuganda damu, iliongeza hofu .
Utafiti wa chanjo ya Covid -19 uliofanywa na tume ya kituo cha kudhibiti magonjwa Afrika (CDC)u meangazia mataifa 15 ambayo yalikuwa na wasiwasi wa usalama wa chanjo.
Kwa wastani , asilimia zipatazo 20% zilijibu kuwa hazikuweza kuwa na chanjo -lakini uwiano ulioko chini ya 10% nchini Ethiopia, Niger na Tunisia mpaka 41% nchini DR Congo.















