Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mzozo wa DRC: Rais Felix Tshisekedi awateua wanajeshi kuwa magavana wa Ituri na Kivu Kaskazini
Rais wa DRC Felix Tshisekedi amefanya uteuzi wa maafisa wa kijeshi kuchukua usimamizi wa mikoa miwili mashariki mwa nchi hiyo ili kushughulikia tatizo la ukosefu wa usalama katika sehemu hizo .
Luteni jenerali Luboya Nkashama Johnny ndiye gavana mpya wa mkoa wa Kivu kaskazini katika jamhuri ya kidemokrasia ya Congo .Naibu wake atakuwa Alonga Boni Benjamin. Mwanajeshi mwingine Luteni Jenerali Constant Ndima Kongba atachukua usimamizi wa mkoa wa Ituri .Msaidizi wake atakuwa Ekuka Lipopo.
Mwishoni mwa wiki rais huyo altangaza mikoa hiyo kuwa katika hali ya 'tahadhari' na 'iliyozingirwa' baada ya msururu wa mauaji yanayotekelezwa na makundi ya wapiganaji wenye silaha .
Tangazo la kuletwa jeshi
Rais Tshisekedi mapema wiki hii aliwataka raia wa nchi hiyo kutoa ushirikiano kwa jeshi na serikali ili kumaliza tatizo la usalama Mashariki mwa nchi hiyo.
Akizungumza katika hotuba kwa njia ya televisheni, Rais Tshisekedi alisema hatua ya baadhi ya maeneo ya Mashariki mwa nchi hiyo kuwa chini ya jeshi ni muhimu ili kuleta hali ya amani.
Tangu kuingia kwake madarakani mnamo mwaka 2019, Rais huyo amekua akisisitiza kuwa moja ya azma yake kuu ni kuleta utulivu katika maeneo hayo.
Jimbo la Ituri limekuwa na vita vya kikabila na jimbo la Kivu Kaskazini ambapo wapiganaji wa kundi la ADF wamekuwa wanawashambulia raia.
Hatua hii ikiwa ina maanisha kuwa wanasiasa inabidi wasijihusishe na wanajeshi maana wanajeshi walikuwa wanalalamika kuwa hawana vifaa tofauti na vile ambavyo wanavipata Umoja wa mataifa na kwa upande wa raia wanapaswa kutoa ushirikiano kuonesha maadui.
Aidha mashirika ya kiraia yamekuwa yakilalamika kuhusu uhusiano wa wanajeshi wa ngazi za juu kutojali uimarishwaji wa usalama kwa raia na kuwa ni hatua ni nzuri ila ni vyema wabadilishe viongozi wa juu wa maeneo hayo.
Jumatatu, iliripotiwa kuwa wapiginaji wenye silaha wamewaua takriban watu 19 wakiwemo wanajeshi kumi baada ya kushambulia vijiji viwili mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo siku ya Jumamosi muda muda mfupi baada ya Rais Felix Tshisekedi kutangaza kwamba mikoa miwili mashariki mwa nchi hiyo Ituri na Kivu Kaskazini ,imezingirwa .
Ongezeko la mashambulizi ya makundi yaliyojihami na machafuko ya kikabila yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 300 tangu mwanzoni mwa mwaka huu huku wanajeshi wa serikali na walinda amani wa umoja wa mataifa wakijaribu kuleta utulivu mashariki mwa nchi hiyo .
Shambulio la hivi punde limefanyika siku ya Jumamosi wakati wapiganaji wenye silaha waliposhambulia vijiji viwili katika mji wa Kivu kaskazini wa Beni, mamlaka za jimbo hilo zimesema.
Baadaye siku hiyo imam mwenye ushawishi mkubwa aliuawa kwa kupigwa risasi msikitini mjini Beni alipokuwa akiwaswalisha watu wakati wa jioni . Alitambulika kwa kupinga itikadi kali za kidini kupitia kituo kimoja cha redio katika jimbo hilo.
Siku ya Ijumaa Polisi katika mji wa Beni waliwatawanya wanafunzi waliokuwa wakifanya maandamano ya kuketi katika ukumbi mmoja wa mji huo kulalamikia ongezeko la hali ya ukosefu wa usalama.
Watu kadhaa walijeruhiwa na wengine kukamatwa kulingana na shahidi mmoja aliyezungumza na shirika la habari la Reuters.
Wanasiasa waliokuwa ofisini sasa watafanya nini?
Hatua ya kuingizwa kwa jeshi katika uongozi wa mikoa hiyo itawaacha nje wanasiasa waliokuwa afisini .
Mkuu wa Wilaya ya Beni Donna Kasereka Kibwana akizungumza na BBC alisema anaikaribisha hatua ya serikali kulileta jeshi na atasalia nje ya ofisi yake kwa muda wote ambao jeshi litakuwa likiongozwa mikoa hiyo .
Kibwana anaunga mkono juhudi zinazochukuliwa na serikali ili kuleta amani mashariki mwa nchi hiyo . Mkuu huyo wa wilaya alisema wanasiasa wanafaa kuwaunga mkono wanajeshi kuleta utulivu kwani wanajeshi hawatakuwa katika uongozi wa majimbo hayo milele .
Ameelezea matumaini kwamba viongozi wote waliokuwa afisini watarejea katika nafasi zao pindi jeshi litakaporejesha hali ya amani . Kibwana anasema kwa muda ambao jeshi litakuwa ofisini atakuwa nyumbani na ataweza kulipa ushauri patakapohitajika .
Kundi la ADF
Kundi moja la waasi kutoka Uganda kwa jina Allied Democratic Forces (ADF) limekuwa mashariki mwa DRC tangu miaka ya 1990 na linaaminika kuhusika na visa vingi vya mashambulizi katika eneo hilo .
Kundi hilo limefanya msururu wa mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya raia tangu jeshi lilipoanza oparesheni ya kuliangamiza mwaka wa 2019 na liliwaua watu 850 mwaka jana kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa .
Ghasia hizo zimesababisha mgogoro wa kibinadamu mashariki mwa DRC ambapo Zaidi ya watu milioni 1.6 wameachwa bila makazi huko Ituri ,mkoa wenye jumla ya watu milioni 5.7 shirika la UNICEF lilisema mwezi Aprili . Watu wengine miloni 2.8 wanahitaji usaidizi wa dharura ,shirika hilo lilisema .