Je wanawake kukatazwa kusali msikitini ni ubaguzi wa kijinsia?

Iliyochapishwa

Mamilioni ya Waislamu kote duniani wakati huu wanafunga mwezi mtukufu wa Ramadhan. Lakini baadhi ya misikiti nchini Uingereza inazuilia wanawake kusali huku mingine ikisema wakati wa mabadiliko umewadia.

Almas huwa ni nadra sana kuwa na muda wa kusali msikitini. Yeye ni mjane wa watoto watatu na anasoma chuo kikuu. Na hiyo ndio sababu anaichukulia Ramadhan kama fursa ya kipekee ya kuabudu.

"Huwa nataka sana kuswali swala ya Taraweeh hasa wikendi wakati tuna muda wa kutosha," alisema. "Lakini sikuwahi kujua hadi nilipowasiliana na msikiti mmoja wa eneo wakaniambia kwamba wazee, watoto na wanawake hawaruhusiwi kusali msikitini'."

Na sio tu kwa Almas, kuna misikiti mingi kote nchini Uingereza ambayo imeamua kupiga marufuku wanawake kwenda misikitini mwezi huu wa Ramadhan. Mara nyingi huwa wanasema ni kwasababu ya janga la virusi vya corona.

Wanawake kama Almas sio tu kwamba wanashindwa kuswali sala ya Taraweeh ambayo huwa inaswaliwa mwezi wa Ramadhan lakini pia kuna misikiti inakataza wanawake kusali sala ya Ijumaa.

'Makataa ya wanawake kutosali msikitini ni ubaguzi wa kijinsia?'

Wakati familia nyingi zinaswali nyumbani, kusali misikiti kunaonekana kukumbwa na ubaguzi wa kijinsia huku wengi wakiamini kwamba kunawafanya wengi wao walegeze kamba kidogo katika kuabudu.

Wakati mwingine wanawake huswali nyuma ya wanaume eneo moja. Hata hivyo, mara nyingi kuwa kuna sehemu mbili kwa wanawake na wanaume, wanaume wakiswali eneo kuu na wanawake wakiswali eneo la kibinafsi au eneo dogo.

Lakini sio misikiti yote inayotenga wanawake. Zaidi ya msikiti mmoja kati ya minne nchini Uingereza, haina sehemu ya wanawake kusali. Katika maeneo ambayo hakuna sehemu ya wanawake kusali, ukubwa wa eneo la kusali hutofautiana.

Anita Nayyar, ambaye anaendesha kampeni ya 'Fungua Msikiti Wangu kwa Wanawake kuwa Huru Kusali' amesema mara nyingi wanawake "huwa wako nyuma". Amesema nafasi yao huwa ni ndogo.

Janga la corona nalo limefanya hali kuwa mbaya zaidi.

"Wakati wa janga la corona, tulipokea taarifa kuwa sehemu za misikitini ambako wanawake wanasali, zitafungwa kama njia moja ya kukabiliana na sheria hizo kwasababu kama vile, hawakuweza kuhakikisha sheria zinafuatwa upande wa wanawake," amesema.

BBC imewasiliana na misikiti 29 mikubwa Uingereza kusikiliza mipango yao wakati huu wa Ramadhan.

Miongoni mwa misikiti ambayo ilikuwa ni Greenwich Islamic Center na Baitul Futuh ya London na msikiti wa Jamia Al-Akbaria uliopo Luton na msikiti wa Lanarkshire uliopo Scotland.

Msikiti anaosali Almas wa Milton Keynes Islamic Center, awali, haukujibu ombi la kuwasiliana na BBC juu ya suala hilo lakini baadaye ukakubali kuwa umepiga marufuku wanawake, watoto na wazee kusali msikitini.

"Kinaya ni kwamba kuna sehemu ya wanawake kusali na vyumba vitatu vikubwa ghorofa ya chini," Almas alielezea. "Kuna wanawake ninaowajua msikitini ambao ni wajane na hawana watoto na pia wana matatizo ya akili.

"Ikiwa mimi nimekasirika, ninachojiuliza, wanawake wengine wamekasirika kiasi gani na hatua hii."

"Je hali hii inaweza kubadilishwa"

Julie Siddiqi, mwanaharakati wanamke wa Uingereza, aliweka video kwenye mtandao wake wa Instagram akilalamikia hatua ya wanawake kukatazwa kwenda msikiti wakati wa Ramadhan.

Mamia ya wanawake Uingereza walimtumia ujumbe wakimuarifu kwamba pia nao wanakabiliwa na hali kama hiyo.

"Najua kwamba kuna suala la umuhimu wa kulinda afya zetu," amesema. "Lakini misikiti yetu ni mikubwa. Inawezekana kabisa wanawake kusali msikitini. Yaani, hakika hii ni zaidi ya corona. Hili limekusudiwa, dhana ya kwamba wanaume wataamua ama ikiwa wanawake watasali misikitini au la."

Hata hivyo msikiti wake uliiarifu BBC kuwa wamechukua hatua hiyo baada ya kushauriana na baadhi ya wanawake waliokuwa wamejitoleaa, "wenye shauku ya maendeleo ya wanawake". Alisema hatukutaka kukaweka wanawake hatarini.

Aidha msikiti wa Baitul Futuh uliopo London ulisema kuwa "katika Uislamu, sio lazima kwa wanawake kusali msikitini, bali ni sharti lsilo na mjadala kwa wanaume".

Dini ya Kiislamu inaweka wazi kuwa sala ya pamoja ni lazima kwa wanaume lakini sio lazima kwa wanawake ambao wameruhusiwa kusali nyumbani.

"Masharti ya kukabiliana na corona yakiondolewa, wanawake wataendelea kusali msikitini kama kawaida," msikiti huo umesema katika taarifa yake.

Unaweza pia kusoma:

Zara Mohammed, Rais wa chama cha Muslim Brotherhood huko Uingereza, amesema kuwa wito wao ni kwa wanaume na wanawake kuruhusiwa kutumia misikiti "wakati wa Ramadhan au wakati mwingine wowote ule".

"Wanawake wajumuishwe katika mipango ya usimamizi na tunahamisha majadiliano endelevu kutoa fursa zaidi kwa wanawake."