Picha ya mtandaoni 'iliyokejeli' hali ya janga la corona India yaibua hisia kali China

Chanzo cha picha, Sina Weibo
Picha iliyochapishwa mtandaoni kwenye akaunti inayohusishwa na Chama cha Kikomunisti cha China imeibua hisia kali baada ya picha hiyo kuonesha ikikejeli hali ya janga la virusi vya corona nchini India.
Kwenye mtandao wa Weibo nchini China kuliwekwa picha inayoonesha roketi ya China ikipaa huku pembeni yake ikionesha miili ya watu waliopoteza maisha kutokana na Covid-19 ikichomwa moto nchini India.
Picha hiyo ilisomeka: ''Kuwasha moto China VS kuwasha moto India.''
Picha hiyo ilioonekana siku ya Jumamosi jioni, ilifutwa kwenye mtandao huo baadaye.
Inaripotiwa kuchapishwa na akaunti inayomilikiwa shirika la usimamizi wa sheria-ya Tume ya siasa na sheria ya chama cha kikomunisti kilicho na mamilioni ya wafuasi kwenye mtandao wa Weibo, mtandao maarufu nchini humo.
Wafuasi walijibu chapisho hilo, ambalo baadaye lilisambazwa mitandaoni waliandika kuwa ''haikuwa jambo zuri'' na kuwa China ''inapaswa kuihurumia India''.
Chapisho la picha hiyo liliwekwa siku moja baada ya Rais wa China Xi Jinping kutuma salamu za rambirambi kwa Waziri Mkuu wa India Narendra Modi kutokana na athari kubwa zilizojitokeza kutokana na janga la corona.
Bw. Xi alisema China iko tayari kushirikiana na India kwa msaada wowote wa ziada utakaohitajika.
India iko kwenye jitihada ya kudhibiti wimbi la pili la virusi vya corona, huku hospitali zikifanya jitihada za kutibu wagonjwa wakati huu wakikabiliwa na changamoto ya upungufu wa vitanda na oksijeni.
Hii leo Jumapili, India imerekodi vifo vya watu 3,689. Idadi kubwa kuwahi kutokea nchini humo.












