Siku ya wafanyakazi: Fahamu matarajio ya Wafanyakazi wa Tanzania

Rais Samia Suluhu
    • Author, Walter Nguma
    • Nafasi, Mchambuzi
  • Iliyochapishwa

Wafanyakazi wengi Tanzania inapofika siku ya Mei Mosi huwa wanaitizima serikali kwa jicho la namna ya tofauti.

Siku hii imekuwa ni siku muhimu sana kwao kwani ndio siku wanapata wasaha wa kuweza kuelezea kero zao kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kupewa majibu.

Mei mosi ilikuwa imezoeleka kama siku ambayo wafanyakazi walikuwa wakiongezewa mishahara lakini hali hiyo imebadilika kwani kwa zaidi ya miaka mitano (5) hivi sasa tokea Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aondoke madarakani 2015 wafanyakazi wa Tanzania hawajapata kupandishiwa mishahara .

Athari za kutoongezwa kwa mishahara

Kutoongezwa kwa mishahara ya wafanyakazi kumesababisha athari mbalimbali katika sekta tofuti nchini .

  • Mfano imepelekea kushuka kwa morali ya wafanyakazi kufanya kazi kwa bidii.
  • Imewafanya baadhi ya watendaji wa serikali kuacha kazi kutokana na ujira hafifu.
  • Imesababisha kiwango cha ubunifu katika utendaji wa shughuli za kiserikali kushuka kwa kasi kubwa.
  • Imeshusha ufanisi wa utendaji wa wafanyakazi ndani ya Serikali kuwa ni wa kusuasua sana kiasi kwamba matokeo ya utendaji wao ndani ya Serikali kuonekana siyo wa kuridhisha kabisa.

Katika kuboresha utendaji wa Serikali ni muhimu maslahi ya watendaji wa Serikali yaani mishahara kuboreshwa kama maadai yao yanavyoainisha na vyama vyao vya wafanyakazi kama vile; TUCTA, RAAWU, CWT, CHODAWU, TUICO, JT, TAMICO, TALGWU na TUGHE, kwani kwa kutokufanya hivyo kunapelekea baadhi ya mambo ya kiserikali kufanyika katika viwango hafifu na visivyo vya kuridhisha hata kidogo.

Mei Mosi nchini Kenya

mei

Mwaka 2017, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alitangaza nyongeza ya mshahara wa chini zaidi ambapo alisema mfanyakazi anastahili kulipwa kwa asilimia 18(18%) na hayo aliyatangaza kwenye siku ya wafanyakazi duniani 1 Mei, 2017.

Hakuishia hapo tu bali alisema mshahara ulio chini ya shilingi 13,475 hautotozwa kodi.

Hata hivyo bado wafanyakazi wa Kenya wanahitaji kuongozewa mishahara kwani hali ya kiuchumi imebadilika na hivyo wanahitaji maboresho pia katika mishahara yao.

Donge nono la wanasiasa

Wanasiasa wameonekana kuwa na misharahara mikubwa kwa nchi za Afrika hasa Afrika ya Mashariki lakini watendaji wengi wa serikalini kama vile walimu, wauguzi, madaktari na wengine wakiwa na mishahara ya tia maji tia maji huku watu kama wabunge na mawaziri wakiwa na mishahara mikubwa, posho kubwa na viinua mgongo vikubwa jambo ambalo limetengeneza tabaka na wivu mkubwa sana katika viwango vya mishahara huku watu wengi wakitamani kuingia kwenye siasa kuliko kuwa mfanyakazi katika ofisi za umma.

Kumekuwa na tatizo la mishahara duni katika nchi za Afrika kiasi kwamba watu wanakimbia kufanya kazi kutoka serikalini na kwenda sekta binafsi na hata kuingia kwenye siasa.

Uganda

Mwaka 2017 nchini Uganda madaktari wa hospitali za umma nchini waligoma kupinga mishahara duni na uhaba wa vitendea kazi, hali iliyopelekea baadhi ya wagonjwa kufariki, hali iliyopelekea hasira nyingi za wananchi dhidi ya Serikali.

Jambo hili lilidhihirika pia Tanzania siku za karibuni pale madaktari na wauguzi walipochaguliwa na Serikali kwenda kufanya kazi katika hospitali za umma kuziacha kazi hizo na kwenda hospitali binafsi ambapo Raisi wa wakati ule Dkt. John Magufuli alitishia kuwafutia leseni zao za udaktari.

Virusi vya Corona

Hivi sasa dunia inapita kwenye wimbi zito la ugonjwa wa Corona (COVID-19) jambo ambalo limesababisha mataifa mengi duniani kuyumba kiuchumi.

Hali za wafanyakazi kwa ujumla siyo njema hata kidogo kwani gharama za maisha zimeongezeka huku mishahara yao ikibaki kuwa ile ile jambo linalowapelekea kushindwa kumudu gharama za maisha na kufanya maisha yao kuwa magumu.

Wafanyakazi wengi leo Mei 1, 2021 wanajiuliza maswali lukuki juu ya uongozi mpya wa Rais Samia Suluhu Hassan juu ya hatma ya wafanyakazi watanzania. Wanajiuliza maswali magumu;-

•Je, ataboresha maslahi (mishahara) yetu au atashikilia mpini wa Raisi aliyepita?

•Je,suala la kupandishwa madaraja kwa watumishi wa umma atalisemea vipi au mtaji wa maskini utasalia kuwa nguvu zake mwenyewe?

•Je, Mazingira ya ufanyajikazi wa watumishi wa Serikali atayatizama upya hususani vitisho vinavyotolewa na viongozi wa kiserikali dhidi ya watendaji wa serikali na ofisi nyingine za umma?

Haya ni baadhi ya machache wafanyakzi wanajiuliza juu ya siku ya wafanyakazi duniani 1 Mei, 2021 chini ya uongozi mpya wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Wafanyakazi wa Afrika mashariki

Wafanyakazi wa kiwanda cha korosha Mtwara

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wafanyakazi wa kiwanda cha korosha Mtwara

Mataifa mengi hivi sasa duniani kama vile Marekani, Uingereza, Rwanda, Ujerumani, Ufaransa na nyingineza yameweza kuandaa mikakati ya kuweza kuwasaidia wafanyakzi wao.

Lakini unaweza kuona kwa nchi kama Tanzania, Kenya , Uganda na nchi nyingine za kiafrika hazijaweka bayana namna zililivyojipanga kuboresha maslahi ya wafanyakazi.

Ni vyema kufanya hivyo hivi sasa kwani gharama za maisha zimeongezeka na hivyo kupelekea hali ngumu ya kimaisha kwa watumishi wengi wa umma.

Wafanyakazi ni nyenzo muhimu sana katika taifa lolote lile kuweza kupiga hatua za kimaendeleo, kwa namna hiyo ni vyema mataifa yote kama vile Tanzania, Kenya, Uganda na nchi nyingine kuona namna ya kuboresha maslahi au mishahara ya wafanyakazi wao serikalini kwani kutasidia kuongeza ufanisi katika maeneo yao ya kazi.

Kama maslahi ya wanasiasa yalivyoboreshwa ni vyema na maslahi ya wafanyakazi wa umma nayo yakaboreshwa ili kuwewza kuendana na hali za kiuchumi zilizopo hivi sasa.