Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya corona: Kwanini uhusiano wa mapenzi unaendelea kudorora?
Janga la virusi vya corona limebadilisha maisha ya ngono. Kwanini uhusiano wa mapenzi unaendelea kudorora - na je itakuwa na athari ya muda mrefu?.
Kabla ya janga wanandoa walikuwa wanaishi kama "meli mbili zinazopishana usiku", amesema, mtaalamu mmoja mwenye makao yake huko Texas, Emily Jamea. Baadhi ya wanandoa walibaini kwamba awali wakati wa kutekelezwa kwa amri ya kutotoka nje, walikuwa na muda mwingi ndani ya nyumba ya kufanya tendo la ndoa ikilinganishwa na awali.
"Awali, janga hilo lilitoa fursa kwa watu ya kuungana tena ambayo pengine awali, waliweza tu kuwa pamoja wakati wa likizo," amesema Jamea. Lakini kadiri janga hilo lilivyokuwa linaendelea, hali hiyo ikaanza "kubadilika", amesema. "Kwa wanandoa wengi, hamu ya kufanya tendo la ndoa ikaanza kupungua."
Utafiti kutoka kila pembe ya dunia unaonesha hilo hilo. Uturuki, Italia, India na Marekani mwaka 2020 kote huko kumeonesha kupungua kufanywa kwa tendo la ndoa kwasababu ya kufungiwa.
"Nafkiri kikubwa kilichochangia hilo watu wengi walikuwa na msongo na mawazo," amesema Justin Lehmiller, mwanasaikolojia wa jamii na mtafiti wa Taasisi ya Kinsey, kulingana na utafiti uliofanywa Marekani.
Kwa wengi, janga hilo ambalo lilisababisha kufungiwa ndani lilitengeneza mazingira ya sintofahamu na hofu. Wengi waliingia hofu ya kiafya, ukosefu wa usalama katika suala la kifedha na mabadiliko mengine ya msingi. Msongo wa mawazo ulitokana na sababu hizo - bila kusahau matatizo yaliyotokana na matumizi kupita kiasi na hatimaye kukasababisha kupungua kwa tendo la ndoa.
Kwa namna mbalimbali, ugonjwa wa virusi vya corona umejidhihirisha kuwa sumu kwa tendo la ndoa na wengine wanachojiuliza ni je, hali ya kawaida katika mahusiano itaweza kurejea kuwa ya kawaida janga litakapotokomea, au hii ni athari itakayokuwepo kwa kipindi kirefu?
Kupungua kwa hamu ya tendo la ndoa
Jamea anasema kuwa wanandoa wengi walifurahia kipindi kile kifupi cha maisha ya ndoa mwanzoni wakati wa kufungiwa. Rhonda Balzarini, mwanasaikolojia wa kijamii na Profesa msaidizi katika chuo kikuu cha Texas, Marekani, alielezea kuogezeka kwa hamu ya kufanya tendo la ndoa kama wakati waliooana wameenda fungate wakati wote wanakabiliana na msongo wa mawazo.
"Wakati wa kipindi hicho walionekana kushirikiana," amesema Balzarini. "Lakini kadiri muda ulivyokwenda, raslimali zilionekana kupungua, watu waliendelea kuwa na msongo na mawazo zaidi na nguvu ikawa inaendelea kupungua, kukata tamaa na msongo mawazo vikaanza kukithiri. Na hilo lilipoanza kutokea huenda hapo ndio wapenzi walianza kuingia katika matatizo."
Balzarini alianza kuona hilo kwa washiriki wenye umri wa miaka 18 na wengine wakubwa zaidi, kutoka mataifa 57 katika utafiti uliofanywa na yeye pamoja na wafanyakazi wenzake wakati wa janga. Na kadiri muda ulivyoendelea kusonga, visa vingi vya msongo wa mawazo vikaanza kuripotiwa ikiwemo upweke, matatizo mengine ndani ya nyumba na wasiwasi mwingine ulitokana na janga la Covid-19, kulikochangia kupungua kwa hamu ya kufanya tendo la ndoa.
Cha msingi zaidi katika utafiti huu, kulingana na Balzarini, ni uhusiano uliopo kati ya msongo wa mawazo na hamu ya kufanya mapenzi. Mwanzoni mwa janga huenda msongo wa mawazo haukusababishwa wapenzi "kutatizika kiakili", anasema. Lakini zilipoendelea kwa muda, watu wakaanza kuchoka kiakili. Na "msongo wa mawazo ukaanza kuathiri hamu ya kufanya tendo la ndoa", anasema.
Mbali na matatizo ya kila siku yaliyotokana na janga la corona, tishio kubwa likaanza kujitokeza wakati idadi ya vifo na waliolazwa hospitali ilipoanza kuongezeka kote duniani.
Kuwa pamoja kipindi kirefu
Wakati Balzarini aliposikia kuhusu wanandoa kuanza kuoga mchana au kuogelea pamoja mwanzoni mwa janga, ile tajriba ya kuoneshana mapenzi zaidi kuliko kawaida hatimaye "ilipoteza dira," alisema.
Na hilo likafanya mahitaji ya kila siku kuongezeka na ikafika wakati wanandoa wakaanza kukosoana.
Lehmiller anaelezea hilo kama "athari ya kuwa na kitu kwa muda mrefu," na hilo likafanya "vijitabia vya kila mmoja vinavyochukiza mwenza wake kuanza kujitokeza." (Balzarini anakumbuka mmoja akimwambia hakuwahi kujua mwenza wake alivyokuwa na tabia ya kutafuna kwa sauti wakati wa mlo hadi wakati ule wamefungiwa.)
Na bila shaka kuwa na muda mwingi pamoja kunapunguza hamu ya kufanya tendo la ndoa. "Moja ya vya msingi kuendeleza uhusiano wa muda mrefu ni kuwa na kitu fulani cha upekee kwa mpenzi wako na pia kuwa mbalimbali kidogo," amesema Lehmiller. "Munapoonana kila wakati… ile hisia ya kuwa na kitu cha kipekee unachomfanyia mwenza wako kunogesha mapenzi inapotea."
Walipokuwa kando kando kabla ya janga kwa sababu ya shughuli za kijamii na kitaaluma, pia watu wanaweza kuanza kujiona hawana thamani na hilo litaathiri kujiamini katika ndoa. Hasa wanawake walilazimika kuweka taaluma zao kando wakati wa janga kwasababu ya kazi za nyumbani na kusomesha watoto wao nyumbani na kuchukua majukumu mengine kulikowafanya kuhisi kuwa na mzigo mkubwa.
Je hali inaweza kurejea kuwa ya kawaida?
Sio kwamba tendo la ndoa ndio limefika mwisho, hata hivyo, watafiti wa Taasisi ya Kinsey wameangazia tabia moja kuimarisha maisha ya ndoa. Mmoja kati ya washiriki watano kwenye utafiti walijaribu kitu kipya wakati wa ndoa, na ikasaidia kufufua tena hamu ya kufanya mapenzi.
"Watu waliojaribu mambo mapya walikuwa na uwezo wa kuimarisha ndoa zao," amesema Lehmiller.
Baadhi ya mambo mapya yaliyosaidia kuimarisha ndoa ni pamoja na "kujaribu mkao mpya wakati wa tendo la ndoa, kutumiana ujumbe wa mapenzi na kadhalika," kulingana na utafiti uliofanywa.
Lakini kwa walio kwenye mahusiano na tayari hamu yao ilikuwa imepungua zaidi ya mwaka mmoja uliopita na bado wanapitia changamoto hiyo, je ugonjwa wa corona utachangia athari hasi ya muda mrefu? Hilo inategemea, wataalamu wamesema.
Wakati umekuwa mgumu lakini kuna matumaini. Huku wengi wakiwa wanaendelea kupata chanjo, mabiashara yameanza kufunguliwa na baadhi ya wafanyakazi wameanza kurejea kazini. "Watu wameanza kurejea katika ratiba zao za kawaida," amesema Jamea.
Kurejea kwa hali ya "kawaida" ni kiashiria kizuri kwa wanandoa ambao wamekuwa na wakati mgumu wakati wa janga. "Kuna uwezekano mkubwa janga likianza kudhibitwa… mambo yakarejea na kuwa kama awali, amesema Lehmiller.