Aliyekuwa mchezaji soka Ujerumani Christoph Metzelder akiri kuonesha picha za unyanyasaji wa watoto

Iliyochapishwa

Aliyekuwa mchezaji soka Ujerumani Christoph Metzelder amehukumiwa kifungo cha nje kwa kipindi cha miezi 10 kwa kosa la kuonesha wengine picha za unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto.

Alikiri mbele ya mahakama moja huko Düsseldorf kwamba alikuwa ametuma picha hizo kwa wanawake watatu ambao pia wanachunguzwa.

"Naacha jeraha ambalo halitawahi kupona," mchezaji huyo aliyekuwa mlinzi, 40, amesema.

Pia aliomba msamaha kwa waathiriwa na kusema atarejesha tuzo zote alizopata kwa kuanzisha kituo cha kusaidia watoto kukabiliana na umaskini.

"Nilituma picha hizo licha ya kwamba nilijua wamepitia mateso yasiyoelezeka ambayo watoto hao wameyapitia," Metzelder amesema mahakamani Alhamisi. "Nakubali hukumu niliyopewa."

Alisema hajawahi kushiriki katika "unyanyasaji dhidi ya watoto na vijana" na kwamba alipata picha hizo kutoka mtandaoni.

Metzelder alishindia Ujerumani makombe 47 na alikuwa miongoni mwa kikosi cha wachezaji wa mwaka 2002 na 2006 kilichoshiriki mashindani ya Kombe la Dunia wakati timu ya taifa ilipoibuka mshindi wa pili na kuchukua nafasi ya tatu mtawalia.

Beki huyo wa kati aliisaidia Borussia Dortmund kushinda kombe la Bundesliga mwaka 2001-2002 akiwa na klabu hiyo kwa miaka saba kabla ya kushinda kombe la La Liga Uhispania akiwa na Real Madrid msimu wa mwaka 2007-08.

Metzelder alistaafu soka ya kulipwa mwaka 2014.