Mwanasesere wa ngono mwenye umbo la guruneti azua taharuki Ujerumani

Chanzo cha picha, POLIZEI HAUZENBERG
Wataalamu wa vilipuzi wameitwa kuchunguza kifaa kilichokuwa kinashukiwa kuwa kilipuzi katika jimbo la Bavaria nchini Ujerumani lakini baada ya uchunguzi kufanywa kikagundulika kuwa mwanasesere wa ngono.
Maafisa wamesema kifaa hicho chenye umbo la guruneti kilionekana kwenye karatasi angavu ya plastiki katika msitu ulio karibu na mji wa Passau.
Mwanamke mmoja aliyekuwa anafanya mazoezi, aliarifu polisi baada ya kukiona na kikosi maalum cha kubaini vilipuzi kikawasili mara moja.
Lakini polisi wa eneo wametoa taarifa kwa umma kwamba wataalam hao walibaini kwamba hakukuwa na haja ya kuwa hofu.
"Baada ya kufanya uchunguzi wa kina juu ya kile kilichokuwa kwenye mfuko, maafisa hao kwa haraka wakabaini kuwa ni mwanasesere wa mpira," Polisi ya Hauzenberg imesema katika taarifa iliyotoa.
"Kifaa hicho kilichukuliwa na kufanyiwa uchunguzi. Ikabainika kuwa ni mwanasesere wa ngono wa mpira, ndani yake kukiwa na kondomu ambazo hazijatumiwa na waya aina ya USB."
Maafisa hao wameongeza kuwa utafiti uliofanywa kwenye mtandao wa kijamii "umethibitisha walichokuwa wanashuku kwamba "kuna wanasesere wa ngono waliotengenezwa mfano wa umbo la guruneti".
Maafisa wa polisi wamesema kuwa wametupa vifaa hivyo vilivyoonekana katika eneo ambalo si la kawaida.
"Vilifikaje eneo hilo na kwanini bado vilikuwa hapo ni jambo ambalo litaendelea kuwa fumbo," taarifa ya polisi imesema.
Vilipuzi vilivyotumika katika vita vya pili vya dunia ambavyo havikuwahi kulipuka huwa vinapatikana mara kwa mara nchini Ujerumani na kusababisha wengi kulazimika kuhama makazi yao.












