Mkataba wa nyuklia wa Iran: Suala la hujuma lagubika mazungumzo muhimu

Iliyochapishwa

Vita vya chini kwa chini kati ya Israel na Iran vinaingiza giza katika kurejelewa kwa mazungumzo muhimu huko Vienna siku ya jumatano kuirejesha Iran na Marekani kwa mkataba wa 2015 kuhusu mpango wake wa nyuklia.

Mazungumzo hayo yalikuja siku tatu baada ya shambulio la kihujuma dhidi ya maeneo muhimu yaliyo na vinu vya nyuklia vya Iran karibu na mji wa Natanz, ambako mlipuko ulikatiza umeme katika eneo lote. Shambulio hilo liliharibu mitambo ya kutengeza uranium kwa ajili ya matumizi ya nyuklia - na kusimamisha kazi katika kituo hicho.

Siku moja kabla, Rais Hassan Rouhani alikuwa amefungua rasmi kituo hicho, kilicho na mitambo inayofanya kazi kwa haraka. Kituo cha awali kililipuliwa katika mazingira ya kutatanisha na "maadui" ambao hawakutajwa mwezi Julai mwaka jana.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kurejelewa kwa mkataba wa nyukilia wa mwaka 2015 ni hatari kwa nchi yake, ambayo Iran inachukulia kuwa hasimu wake. Akizungumza wiki iliyopita mkesha wa ukumbusho wa siku ya mauaji ya halaiki dhidi ya Wayahudi wakati wa vita vya pili vya dunia, alisema Israel italinda raslimali zake.

Hatua ya Iran kuangazia shambulio la hivi punde katika mazungumzo ya Vienna, kuielezea kuwa "ugaidi wa nyuklia" na kuilaumu Israel, ni dhihirisho kwamba pande zote zinahitaji kutafuta ufumbuzi wa haraka, na matokeo yoyote katika mazungumzo hayo hayataridhisha Iran pekee, Marekani na mataifa mengine yaliyo na uwezo duniani, bali pia Israel na majirani wa Iran.

Shambulio hilo pia limetoa nafasi kwa Iran katika mkakati wa mazungumzo ya kupanua haraka mpango wake wa nyuklia na kuwa uwezo wa kujadili masuala kwa maslahi yake.

Mzozo wa nyuklia wa Iran: Ya msingi

  • Mataifa yenye nguvu duniani hayaamini Iran: Baadhi ya nchi zinaamini Iran inataka kuwa na nguvu za nyuklia kwasababu inataka kuunda bomu la nyuklia - imepinga hili.
  • Kwa hivyo mkataba ulifikiwa: Mwaka 2015, Iran na nchi zingine sita zilifikia makubaliano makubwa. Iran ilikuwa iachane na shughuli zake za nyuklia ili iondolewe vikwazo ambavyo vimeathiri uchumi wake.
  • Sasa tatizo ni nini? Iran ilirejelea tena shughuli za nyuklia zilizopigwa marufuku baada ya rais wa zamani wa Marekani Donald Trump kuiondoa nchi hiyo katika mkataba wa nyuklia na kuiwekea tena vikwazo Iran. Ijapokuwa kiongozi mpya wa nchi hiyo Joe Biden anataka kujiunga tena na mkataba huo, pande zote zinataka mmoja wao achukue hatua ya kwanza.

Ikijibu, Iran ilitangaza kwamba kufikia Jumatano itaongeza uhuishaji wa madini ya uranium kwa hadi asilimia 60% - hatua ambayo inakaribia asilimia 90 inayohitajika kuunda bomu la nyuklia, kitu ambacho Iran inasema sio lengo lake. Tangazo hilo linatishia kurudisha nyuma mazungumzo: hatua kama hiyo ni hatari na haitakubaliwa na washirika wa Iran kama vile China na Urusi.

Mazungumzo hayo yanalenga kuleta Iran na Marekani pamoja ili kutekeleza mkataba, kumaanisha kuwa Iran itakomeshwa katika juhudi zake za kuwa na uwezo wa nyuklia na kuondolewa vikwazo vya Marekani ambavyo vimelemaza uchumi wa Iran na kuwaathiri vibaya raia wa nchi hiyo wapatao milioni 85.

Mkakati wa Kidiplomasia

Mazungumzo yanaendelea kati ya Marekani na Iran japo sio moja kwa moja, lakini yanaendeshwa kupitia usaidizi wa Uingereza,Ufaransa Ujerumani, Urusi, na China zikiwa kama mpatanishi chini ya uwenyekiti wa Muungano wa Ulaya, EU.

Ujumbe wa Iran umeelekezwa na Kiongozi Mkuu wa nchi hiyo Ayatollah Ali Khamenei isizungumze moja kwa moja na Marekani.

Wajumbe wa Iran na Marekani wako katika hoteli tofauti zilizo umbali wa mita 100. Naibu Mkuu wa sera za kigeni wa EU anaendesha mkakati huo wa kidiplomasia. Muda wa maana unapotezwa, wanasema maafisa wa Marekani ambao wako tayari kwa mazungumzo ya moja kwa moja.

Wiki iliyopita pande zote zilikubaliana kuunda makundi ya wataalamu kubuni ni mambo gani hasa Iran na Marekani zinahitaji kuzingatia ili kutekeleza mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015. Rais wa zamani wa Marekani Donald Trumpa aliiondoa nchi hiyo katika makataba huo mwaka 2018 na Iran imeendelea kuukiuka tangu wakati huo.

Utawala wa Rais Joe Biden, umesema uko tayari kurejea katika mkataba huo na kuondoa vikwazo ikiwa Iran utakomesha shughuli zake za nuklia kama ilivyofikiwa katika mkataba h wa kimataifa.

Taarifa zaidi kuhusu mzozo wa nyuklia wa Iran

Iran kwa upande wake, kwa mujibu wa Kiongozi Mkuu wake, itazingatia makubaliano hayo pale Marekani itakapowaondolea vikwazo vyote.

Zaidi ya vikwazo 1,500 ziliwekewa Iran baada ya Rais Trump kujiondoa katika mkataba huo, baadhi zikiwa zile zinazohusiana na shughuli za nyuklia. Lakini zinggine zinahusiana na masuala mengine - ikiwa ni pamoja na madai ya kujihusisha na shughuli za ugaidi, ukiukwaji wa haki za binadamu, Hatua ya Iran kuunga mkono makundi ya wanamgambo katika nchi jirani, na hatua ya Iran kuunda na kufanyia majaribio makombora ya masafa ya mbali.

Iran inasisitiza baadhi ya vikwazo vya Marekani ambavyo havihusiani na shughuli za kinyuklia zinafaa kuondolewa.

Kuhusi suala la ikiwa Iran itatekeleza mkataba wa nyuklia, Rais Rouhani amesema hiyo haitachukua muda hata kidogo, na kuongeza kwamba itachukua juhudiza hapa na pale za kuimarisha na kulegeza masharti machache. Lakini kuna ishara huenda mambo yakawa magumu zaidi vile alivyosema. Mkuu wa Shirika la Kawi ya Atomiki la Iran, Ali Akbar Salehi, amesema mchakato huo utachukua muda wakati ya miezi miwili hadi mitatau.

'Muda' unayoyoma

Halafu kuna suala la ikiwa mkataba wa mwaka 2015 bado unafikia malengo ya sasa hasa ikizingatiwa kwamba ulisainiwa miaka sita iliyopita. Mambo mengi yameibuka kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kawi ya atomiki la.

"Sidhani watasema moja kwa moja, 'Tunarejea katika mpango wa kwanza', kwasababu mpango wa kwanza haupo tena ," Mkurugenzi wa Mkuu wa IAEA Rafael Grossi alisema.

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Iran imeunda, kufanyia majaribio na kuweka mitambo ya kuhisha madini ambayo imesambaratisha hesabu ya viwango vilivyokubaliwa katika mkataba wa mwaka 2015.

Kabla ya mazungumzo hayo, Rais Rouhani aliweka bayana kwamba vikwazo vya Marekani dhidi ya nchi yake ni itapewa kipaumbele katika miezi minne ya mwisho iliyosalia kwa serikali yake.

Uchaguzi wa urais unatarajiwa kufanyika tarehe 18 mwezi Juni mwaka huu na Rais Rouhani atapokeza madaraka kwa serikali mpya kufikia tarehe 5 mwezi Agosti.