Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hasssan apokea ujumbe maalum wa Rais Kenyatta wa Kenya
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amepokea ujumbe maalum kutoka kwa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta uliowasilishwa kwake na Waziri wa Michezo, Utamaduni na Urithi wa nchi hiyo, Balozi Amina Mohamed.
Taarifa iliyotolewa leo Aprili 10, 2021 na mkurugenzi wa mawasiliano ya rais Ikulu nchini Tanzania , Gerson Msigwa inasema pia kwamba Rais Samia amefanya mazungumzo na Balozi Amina kuhusu dhamira ya
Tanzania na Kenya kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano katika nyanja mbalimbali hususani kiuchumi na kijamii.
Rais Samia aliupokea ujumbe huo katika Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais Samia amemhakikishia mwenzake wa Kenya kwamba Serikali yake ipo tayari kuendeleza mambo mazuri yaliyokuwa yakifanywa na mtangulizi wake Hayati John Magufuli na kutatua changamoto kati ya nchi hizo mbili.
Taarifa hiyo imesema Rais Samia amewataka mawaziri na wataalamu wa Tanzania na Kenya wanaounda kamati ya ushirikiano wa pamoja ambao hawajakutana tangu mwaka 2016 kukutana mara moja ili kufanyia kazi masuala mbalimbali ya kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili .
Amesema Kenyatta amemwalika Samia kufanya ziara nchini Kenya ili kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano.
Amemhakikishia kuwa Kenya ipo tayari wakati wote kushirikiana na Tanzania kwa kuendeleza, kukuza zaidi ushirikiano kati ya nchi hizo.
Katika kinachoonekana kama kuboresha uhusiano na ushirikiano wa mataifa ya Afrika mashariki Tanzania itaendelea na mpango wake wa kusaini makubaliano ya ujenzi wa bomba la mafuta na nchi jirani ya Uganda na kampuni ya Total hapo kesho jumapili .
Ujumbe wa Tanzania tayari umewasili Uganda kwa hafla hiyo na rais Suluhu anatarajiwa kukutana na mwenzake wa Uganda kesho katika ikulu ya Entebbe kwa hafla ya kutiwa saini kwa makubaliano hayo .