Kutana na akina mama wanaowalinda mabinti zao dhidi ya ukeketaji

    • Author, Saroj Pathirana
    • Nafasi, BBC World Service
  • Iliyochapishwa

Walinilaza chini na kunikata sehemu hii ya mwili - sikujua kwanini. Ilikuwa mara yangu ya kwanza kupitia mfadhaiko wa aina hiyo maishani: Sikujua nilichowakosea watu hawa wazima - ambao niliwapenda - wao kuwa juu ya yangu na kufungua miguu yangu nia yao ikiwa kuniumiza."

Layla (ambaye sio jina lake halisi) alikuwa na miaka 11 au 12 tu alipokeketwa.

Miongoni mwa jamii za Kiislamu wenye msimamo mkali, hasa katika maeneo ya vijijini, wanawake wanachukuliwa kuwa "wachafu" na pia "hawako tayari kuolewa" ikiwa hawajakeketwa.

Utamaduni huo ulipigwa marafuku nchini Misri tangu mwaka 2008 - na madaktari wanaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka 7 gerezani ikiwa watapatikana na hatia ya kutekeleza utamaduni huo. Pia yeyote atakayetafuta huduma hiyo anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka mitatu gerezani.

Lakini licha ya hatua hizo zote kupigwa, bado ni moja ya nchi ambazo utamaduni huo unafanywa kwa kiwango cha juu duniani. Na mara nyingi huwa unafanyika kwa kisingizio cha "upasuaji wa kimaumbile", kulingana na Reda Eldanbouki, wakili wa haki za binadamu anayeongoza kituo kinachosimamia kesi zinazokabili wanawake bila malipo.

Kituo hicho kinachohamisha wanawake masuala ya sheria mjini Cairo na hadi kufikia sasa kimewasilisha kesi 3,000 kwa niaba ya wanawake na kushinda kesi 1800 kati ya hizo, ikiwemo kesi sita zenye kuhusishwa na ukeketaji.

Huenda ikaonekana kana kwamba sheria inawependelea lakini kupata haki ni kitu kingine kabisa. Hata wakosaji wanapopatikana na hatia, mahakama na polisi wanakuwa na huruma sana dhidi ya waliotenda makosa, Eldanbouki amesema.

Ameelezea BBC kampeni zinazoendeshwa na kituo hicho dhidi ya utamaduni huo na kutambulisha wanawake watatu waliozungumzia tajriba yao na kwanini wanataka kulinda kizazi kijacho.

Simulizi ya Layla: 'Walinishika na kunikeketa… sikujua nilichokuwa nimeakosea'

Karibu miongo mitatu sasa, siku ile bado Layla anaikumbuka vyema kwenye fikra zake. Alikuwa tu ndio amepita mtihani wake.

"Badala ya kunituza kwa alama nzuri nilizopata, familia yangu ikanitafutia mkunga aliyekuwa amevaa nguo za rangi nyeusi, wakanifungia chumbani na kunizunguka," Layla anakumbuka.

Ni mwiko kuzunguzia ukeketaji kiasi kwamba Layla, 44, mwenye watoto wanne, hataki hata kusema anaishi wapi hasa huko Misri.

Bibi yake na majirani zao wawili wanawake ni miongoni mwa waliokusanyika siku ile.

"Kuishi kijijini, kama wengine tunafuga kuku nyumbani. Baada ya mwanamke kukeketa sehemu yangu hii ya mwili, alitupa kipande hicho kwa kuku waliokusanyika kukila," Layla anakumbuka.

Na tangu wakati huo, Layla hajawahi kula kuku au hata kuwafuga.

"Kwa wanakijiji, mwanamke ambaye hajakeketwa ni mwenye dhambi. Lakini dhana hii inaleta maana kweli? Hilo lina uhusiano gani na tabia za mtu? Wanafuata utamaduni ambao hata hao wenyewe hawauwelewi," amesema.

Alipojifungua mtoto wake wa kike, Layla hakutaka mwanae apitie alichopitia lakini hakuweza kumkataza mume wake kutekeleza utamaduni huo kwasababu alitaka kufurahisha familia yake.

Layla akaanza kuhudhuria warsha zilizoandaliwa na Eldanbouki, ambao walimpa hamasa ya kumlinda binti yake wa pili.

Simulizi ya Sharifa: 'Nilivuja damu sana nikakimbizwa hospitali baada ya kukeketwa'

Sharifa sio jina lake halisi alikuwa na umri wa takriban miaka 10 baba yake alipoamua kumkeketa.

"Mama yangu alikuwa anapinga mimi kufanyiwa utamaduni huu lakini baba yangu alitaka kufurahisha wazazi wake na dada zake na pia kuthibitisha kwamba yeye ndio mwenye sauti nyumbani, alinichukua na kunipeleka kwa daktari bila kumuarifu mama."

"Nilikuwa ninalia na sikuelewa kwanini baba yangu alitaka nikeketwe. Sikuelewa kilichokuwa kinaendelea lakini nilikuwa na wasiwasi baada ya kuona nimefunguliwa sehemu hiyo mbele yangu kuna daktari - Nilijua kuna kitu ambacho hakiko sawa.

"Alitumia kitu kama pini akanidunga kidogo. Nikaanza kuvuja damu hasa hadi ikabidi nipelekwe hospitali," Sharifa anakumbuka. "Baba yangu akaogopa na kulazimika kumwambia mama yangu - alikuwa anafikiria kuna kitu kibaya kinaweza kunitokea."

"Mama yangu - ambaye alikuwa na matatizo na moyo na shinikizo la juu la damu - alipoteza fahamu papo hapo baada ya kupashwa taarifa hizo," Anakumbuka. "Akaletwa hospitali niliyokuwa na kufariki dunia hapo. Na sasa hivi ninaishi na bibi yangu mzaa mama."

Akiwa pamoja na rafiki zake, Sharifa pia naye alihudhuria warsha ya ufahamu kuhusu suala la ukeketaji iliyoandaliwa na Eldanbouki na timu yake.

Mwaka 2013, daktari mmoja aligungwa jela miezi mitatu kwa kutekeleza ukeketaji dhidi ya msichana wa miaka 13.

Smulizi ya Jamila: 'Baada ya kukeketwa nilikuwa naogopa sana wakunga- Nikifikiria watanitendea tena kitendo kile'

Jamila, sio jina lake halisi, 39, alikeketwa alipokuwa na miaka 9.

"Ulikuwa wakati wa mapumziko na mama yangu akamleta mkunga mzee na majirani zetu wawili nyumbani. Alitayarisha kila kitu na akaniacha nao kwenye chumba," Jamila anasema.

"Nilipoingia ndani walinivua nguo na kila mmoja wao akanishika miguu. Mkunga yule alikuwa na kijembe kidogo alichokitumia kinikata nacho," anasema. "Mama yangu hakuwepo kwasababu

Mbali na machungu na kovu la kisaikolojia alilopata kwasababu ya kukeketwa, Jamila anasema alichopitia kilimbadilisha kabisa.

Awali alikuwa msichana mzungumzaji, jasiri na mwerevu darasani lakini baada ya hapo, yote yalibadilika, anasema. Alikwepa sana wanawake wazee.

Jamila anasema bado anahisi uchungu anapofanya mapenzi na mume wake.

"Maisha yenyewe yana panda shuka zake na tendo la ndoa linakuwa kama mzigo. Pengine kama ningekuwa nafurahia tendo la ndoa, hiyo ingenisaidia kusahau nilichopitia. Lakini kwa sasa ni matatizo tu."

Jamila alidhamiria kuwa binti yake hatapitia alichopitia na baada ya kuhudhuria warsha za Eldanbouki, akiwa pamoja na mume wake na familia yao, pia nao waliacha utamaduni wa kukeketa wanawake.

Kulingana na Shirika la Watoto Duniani la Umoja wa Mataifa (Unicef), asilimia 87 ya wasichana na wanawake wenye umri kati ya 15 hadi 49 nchini Misri wamekeketwa, huku asilimia 50 ya raia wa Misri wakiamini kwamba kukeketwa "ni hitaji la kidini".

Makala hii imeandikwa kwa msaada wa Reem Fatthelbab kutoks idhaa ya BBC ya Kiarabu. Michoro na Jilla Dastmalchi.