Trump awauliza waalikwa kwa sherehe ya harusi 'mnanikosa bado?'

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 2

Aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump alitokea katika harusi moja iliyokuwa ikifanyika katika eneo lake la mapumziko la Mar-a-Lago mjini Florida mwishoni mwa juma na kulalamika dhidi ya Joe Biden, China na Iran.

Rais huyo wa zamani alichukua kipaza sauti cha mshereheshaji na hakupoteza muda kuingia katika mazungumzo ya kisiasa.

Aliielezea hali katika mpaka wa Mexico na kuibua maswali mengine zaidi kuhusu uchaguzi wa urais wa mwezi Novemba, ambao alishindwa.

"Bado mnanikosa ?" aliwauliza waliohudhuria sherehe, ambao walimshangilia.

"Ninapata taariha hizo zote, na wananiambia kuhusu mpaka, wananiambia kuhusu Uchina, wananiambia kuhusu Iran ," Bw Trump alianza, katika video iliyotolewa na wavuti wa burudani wa TMZ.

" Tulikuwa tayari kufanya mpango, walikuwa tayari kufanya kila kitu, wangefanya chochote. na huyu mtu [Biden] anaenda anaondoa vikwazo na halafu anasema tungependa kufanya mazungumzo sasa ," alisema.

Rais Biden hajaondoa vikwazo dhidi ya Iran.

Mwezi February, Ikulu ya White House chini ya Biden iliondoa dai kutoka kwa utawala w Trump kamba Baraza la Uslama la Umoja wa Matiafa litekeleze vikwazo vya kimataifa dhidi ya Iran kwa kukiuka mpango wa nyuklia.

Bw Trump aliugeukia utawala wa Biden kuhusiana na hali katika mpaka wa Mexico. Idadi ya watu wanaowasili imeongezeka tangu Bw Biden aingie mamlakani, wakiwemo mamia ya watoto ambao hawajasindikizwa ambao wanashikiliwa katika mahabusu za wahamiaji.

"Mpaka sio mzuri sana. Umekua mbaya kuliko wakati wowote ule, alisema Bw Trump. "Kile kinachotokea kwa watoto, wanaishi katika hali duni . Wanaishi katika hali ambayo haijawahi kushuhudiwa na mtu yeyote. Hakujawahi kuwa na kitu kama hiki ."

Chini ya utawala wa Bw Trump, maelfu ya familia za wahamiaji walitenganishwa na watoto wao kutoka mwaka 2017 hadi 2018.

Rais huyo wa zamani aliamua kugeuza mazungumzo yake na kuzungumzia kushindwa kwake na Biden katika uchaguzi wa hivi karibuni, jambo ambalo Bw Trump alilipinga.

"Walisema pata kura milioni 66, sir, na uchaguzi umeisha. Nilipata kura milioni 75, na mliona kile kilichotokea ," alisema.

Bw Biden alipata zaidi ya kura milioni 80.

"Saa 10.30 usiku , ghafla, walisema hilo ni jambo la ajabu, kwanini wanafunga baadhi ya sehemu. Kuna mambo mengi yanaendelea sasa hivi ."

Bw Trump alimalizia tuhuma zake kwa "kuwatakia mema wanandoa wazuri ", John na Megan Arrigo.

Hii si mara ya kwanza kwa Bw Trump kujitokeza katika harusi za wafuasi wake.

Mnamo mwaka 2019, akiwa rais alionekana katika hafla ya harusi iliyofanyika katika klabu yake ya gofu iliyopo New Jersey, na kuwafanya bibi harusi, Bwana harusi na wageni waalikwa kushangilia, ''USA!, USA!''