Watu kadhaa wauawa katika shambulio la wanamgambo wa Kiislamu Msumbiji

Iliyochapishwa

Watu kadhaa wameuawa kufuatia shambulio lililotokea mjini Palma, kaskazini mwa Msumbiji, kwa mujibu wa msemaji wa idara ya usalama.

Watu saba wameuawa wakati wakijaribu kutoroka mapigano hayo katika hoteli moja, amesema Omar Saranga.

Mamia ya wengine wageni na wenyeji waliripotiwa kuokolewa.

Eneo hilo limevamiwa na wapiganaji tangu Jumatano.

Watu walioshuhudia wameelezea jinsi walivyokuwa wakijificha ili waweze kuokolewe kwa njia ya boti, katika fukwe walikokutana na miili iliyotenganishwa na vichwa.

Katika tovuti ya askari wa majini inaonesha boti kubwa zikiwa maeneo ya Palma, na katika fukwe ya Pemba mpaka eneo la kusini ambapo watu walikuwa wanajaribu kutorokea huko kwa namna yeyote - boti za mizigo, meli za abiria na aina nyingine za boti.

Tunafahamu nini kuhusu uokoaji huo?

Mkandarasi mmoja aliiambia BBC kuwa watu wengi walitoroka katika hoteli hiyo kwa makundi kwa kujificha pembezoni mwa ufukwe majira ya usiku waliweza kufanikiwa kutoroka na boti siku ya Jumamosi asubuhi.

Alisema watu wengi waliweza kufika salama na boti zilirudi Jumapili kuokoa wengine.

Alisema raia ambao walikuwa wanafanyakazi na kuishi katika eneo hilo walionekana kusaidia katika shughuli za uokoaji.

"Wauzaji wa bidhaa za ndani na makampuni, walikuwa mashujaa katika zoezi zima la uakoji.

Kwa muda mfupi walifanikiwa kuratibu namna ya kuwaokoa wahanga kwa kutumia boti na kufanikisha kuwaondoa wakiwa usalama."

"Sijui msaada kutoka makampuni makubwa ulikuwa wapi au hata kutoka nje ya nchi?" aliuliza.

Raia wa Afrika Kusini, Adrian Nel aliuliwa wakati akijaribu kutoroka wanamgambo hao, mama yake Bi. Meryl Knox aliiambia BBC.

Mume wake, Gregory, alifanikiwa kutoroka katika mji huo wa Palma - ingawa aliiambia AFP kuwa ilimbidi kubeba mwili wa marehemu mtoto wake mmoja wa kiume mpaka alipookolewa. Ingawa mtoto wake mwingine aliweza kutoroka.

Lakini walipoondoka, Bi Knox aliiambia BBC hakukuwa na jeshi linalowalinda, ilikuwa ni mtu tu kukimbia na kuokoa maisha yake.

"Hili suala lingeweza kuzuilika," aliongeza. "Mtoto wangu angekuwa hai mpaka sasa."

Pia unaweza kutazama:

Chanzo kimoja cha habari ambacho kilikuwa karibu na uokoaji kimeiambia AFP kuwa katika boti moja watu wapatao 1,400 waliwasili katika bandari ya mji wa Pemba, ambao ni karibu kilomita 250 (155 miles) kusini mwa Palma, Jumapili mchana.

Mashirika ya kutoa msaada yalisema boti ndogo kadhaa ambazo zilikuwa zimejaza watu zinategemewa kuwasili Jumatatu asubuhi.

Hali ikoje Palma?

Kampuni kubwa ya nishati ya Ufaransa Total ilisema ililazimika kusitisha shughuli katika mradi mkubwa wa gesi ulio karibu na eneo lenye mapigano.

Total iliongeza kuwa inaamini vikosi vya usalama vya Msumbiji, ambavyo vilikuwa vikifanya kazi ili kudhibiti eneo hilo.

Human Rights Watch ilisema kwamba mashuhuda walielezea kuwa waliona "miili barabarani na wakazi wakitoroka baada ya wapiganaji kufyatulia risasi kiholela watu na majengo".

Eneo la Kaskazini mwa Msumbiji limekumbwa na uasi tangu mwaka 2017.

Wapiganaji wanaohusishwa na kundi la Islamic State (IS) ndio wanaosababisha mzozo katika eneo lenye Waislamu wengi la Cabo Delgado.

Mapigano hayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 2,500 na watu 700,000 wamehama makazi yao.

Kuna taarifa ambazo hazijathibitishwa za raia wa Uingereza kunasa katika hoteli.

Msemaji wa ofisi ya mambo ya nje, Jumuia ya madola na Maendeleo ameiambia BBC: ''Ofisi yetu ya ubalozi mjini Maputo iko kwenye mawasiliano ya moja kwa moja na mamlaka za Cabo Delgado ili kupata taarifa zaidi kuhusu ripoti hizi.''

Waasi walianzisha shambulio la kushtukiza Palma mapema wiki hii wakishambulia maduka, benki na kambi za jeshi.

Mamia ya watu walitoroka mapigano, wakikimbilia misituni, mikoko au vijiji vya karibu. Karibu wafanyikazi wa kigeni 180 wa kampuni ya uzalishaji gesi na wazawa walitoroka katika hoteli ya Amarula Palma.

Wengine walijaribu kutoroka hoteli hiyo wakiwa na msafara wa magari Ijumaa, wakielekea pwani iliyo karibu, shirika la habari la Reuters lilimnukuu Lionel Dyck akisema. Bwana Dyck anaongoza kampuni ya usalama ya kibinafsi ya Afrika Kusini inayofanya kazi na serikali ya Msumbiji.

Lakini walivamiwa nje ya hoteli hiyo, Bw Dyck alisema, akiongeza kuwa watu wasiopungua 20 hapo awali walisafirishwa kwa usalama kwenye helikopta.

Mtu huyo wa Afrika Kusini aliyethibitishwa kuuawa alidhaniwa alikuwa akiendesha moja ya magari yaliyotumika kutorosha watu.

Chanzo kimoja kiliiambia BBC watu kadhaa walifanikiwa kuhamishwa na kufika mji wa Pemba, umbali wa kilometa 420 Kusini mwa Palma.

Pia unaweza kutazama: