Mpiga picha wa Somalia: 'Nataka iwe kawaida kwa wanawake kupiga picha'

Chanzo cha picha, Fardowsa Hussein
Mara nyingi nchi ya Somali inajulikana kwa picha za ghasia na uharibifu lakini maonesho ya upigaji picha katika mji wa Mogadishu, imekuwa changamoto siyo tu kukabiliana na dhana hiyo lakini pia kubadilisha mtazamo kwa wanaotazama picha hizo, Mwanahabari wa BBC Mary Harper ametuandalia taarifa ifuatayo.

Katika ukuta mkubwa wa rangi nyeupe katika eneo la hoteli, kuna picha zilizopigwa na rafiki wawili wa kike wa Somali.
"Ni muhimu kwa wanawake kuanza kutafuta tena nafasi za wanawake katika jamii," mmoja wa wasanii, Fardowsa Hussein, amesema.
Anasema kuwa wakati anapiga picha mitaani, mara nyingi wanaume huwa wanamkemea wakimwambia kwamba anastahili kuwa nyumbani badala ya kujiaibisha mbele ya umma.
"Nataka iwe kawaida kabisa kwa wanawake kama mimi kwenda nje na kupiga picha au kufanya filamu bila hofu ya kuabishwa au kunyanyaswa."

Chanzo cha picha, Fardowsa Hussein

Katika maonesho yaliyoandaliwa na Sagal Ali, mkurugenzi wa wakfu wa Sanaa Somali ambao aliuanzisha Septemba mwaka 2020.
Anasema kuwa upigaji picha nchini Somalia inachukuliwa kama kazi ya mwanamume "hasa inapokuja suala la wanaopiga picha mitaani. Wanawake hawatarajiwi kuwa nje kunakili maisha ya kila siku katika sehemu ambayo watu wanaendelea na shughuli zao za kila siku".
"Ubunifu na utamaduni umeharibiwa kwa zaidi ya miaka 30 ya vita nchini Somalia," anasema. "Lengo la wakfu wake ni kufufua utamaduni uliopotea na kutoa fursa kwa watu."
Pia anataka kubadili mtazamo wa watu, na katika maonesho haya ana imani ya kupinga mtazamo wa kuwa wanawake hawawezi kufanikiwa katika kazi za sanaa.
"Nilivutiwa na namna wanawake wanavyotazama wakati wanapigwa picha na hisia zinazojitokeza. Sidhani kama picha hizo zingeweza kupigwa na mmwanamume," Ali amesema.

Chanzo cha picha, Fardowsa Hussein

"Nilipiga picha hii karibu kusini mashariki mwa mji wa Hudur," Hussein amesema.
Ufugaji wa ngamia ni kitu kizuri zaidi ambacho unaweza kukiona. Vijana wadogo ndio wanaopeleka ngamia malishoni. Wavulana wawili wanaenda malishoni wakiwa na karibu ngamia 50 na wakati mwingine huwa wanaenda kwa siku sita hadi saba bila maji ya kunywa.
"Raia wa Somali wanasema hiyo ndio kazi ngumu zaidi kwa mtu kuwahi kufanya, lakini yenye faida zaidi kwasababu ngamia ndio wenye thamani kubwa sana katika utamaduni wetu."

Chanzo cha picha, Hana Mire

"Nilikuwa ndani ya tuktuk mjini Mogadishu nilipoona wasichana wawili," amesema mmoja wa wapiga picha, Hana Mire.
"Nilikuwa na furaha sana kipindi hicho. Nikaruka kutoka kwenye tuktuk niliyokuwa nimepanda na wao hawakujua kama mimi nilikuwa ninawapiga picha. Baada ya hapo nikawaonesha picha ile, na wakaipenda."

Chanzo cha picha, Fardowsa Hussein
Picha hii ya mwanamke akiwa baharini ndio anayoipenda sana Hussein.
"Alinyamaza kimya licha ya pilkapilka zilizokuwa zinaendelea," ameelezea.
Hussein anasema ukweli wa kwamba pia yeye naye alikuwa amevaa hijab hilo liliwafariji, na wakampa fursa ya kuwapiga picha na kunasa matukio yaliyokuwa yanayeendelea.

Chanzo cha picha, Fardowsa Hussein

Pia alifanikiwa kuchukua picha za wanawake wakiwa majini huku wakiwa wanapiga maji kwa miguu na mikono.

Chanzo cha picha, Hana Mire
"Awais alipenda picha hii," amesema Mire.
"Ana roho safi. Aliniambia kwamba mimi nilikuwa mpiga picha wa kwanza kumpiga yeye picha maishani mwake Anakabiliana na kila aina ya unyanyasaji."
Mire anahisi ni muhimu kuonesha vile Somalia inavyojumuisha kila mmoja.
"Mara nyingi watu hufikiria watu wa Somali ni kabila moja, kwamba wote wanazungumza lugha moja. Lakini huo sio ukweli."

Chanzo cha picha, Hana Mire

Picha hiyo ilipigwa ndani ya msikiti mmoja wa zamani eneo la Hamar Weyne, wakati wa sikukuu ya Eid al-Fitr.
"Mwanamke alikuwa amesimama huku wengine wakiwa wamepiga magoti na kuomba," Mire amesema.

Chanzo cha picha, Hana Mire

Mire pia alipiga picha ya Hamar Weyne, akiwa barabarani katika majengo yaliyojengwa mtindo wa Kiarabu.
"Hii ni moja ya sehemu ninayoipenda sana kupiga picha hapa Mogadishu," amesema.
"Nilimuona mwanamume huyu akitembea na nikapenda alichokuwa amevaa. Nikamuuliza kama naweza kumpiga picha na akakubali."

Chanzo cha picha, Hana Mire
Hii ni picha inayopendwa sana na Mire.
"Nilikuwa eneo la kale la Shangani. Hata kama nilikuwa Napata kumbukumbu za vita vilivyokuwa kupitia majengo, ilinikumbusha wazazi wangu na kumbukumbu za kufurahisha za uliokuwa wakati mmoja mji wa kifahari."
Anaelezea alivyokuwa amenyamaza, alitafakari tajriba ya wazazi wake alipomuona Alana akitazama bahari.
"Nilifikria ni mimi. Aliniwakilisha wakati nilipokuwa mtoto."

Chanzo cha picha, Hanna Mire
Wapiga picha wanahisi kwamba katika kipindi kirefu, nchi za Magharibi zimekuwa zikiendeleza dhana ya kwamba nchi hiyo ni eneo hatari zaidi duniani, iliyosambaratishwa na vita, magonjwa na janga la baa.
Wanasema wanataka kuchukua udhibiti wa historia ya nchi ya Somalia kuonesha vile maisha yanavyofurahiwa nchini humo.

















