Chanjo ya AstraZeneca : Wataalamu wachunguza usalama wake

Iliyochapishwa

Wataalam wa usalama wa chanjo kutoka shirika la afya duniani wanakutana siku ya Jumanne kutathmini upya chanjo ya Oxford -AtraZenica baada ya baadhi ya mataifa kusitisha usambazaji wake.

Mataifa ikiwemo Ufaransa na Ujerumani yamesema kwamba walikuwa wanachukua tahadhari huku kukiwa na ripoti kuhusu mgando wa damu miongoni mwa mataifa ya Ulaya.

WHO inasema kwamba hakuna ushahidi kuhusu mgando wa damu na chanjo hiyo na imeyataka mataifa kutositisha usambazaji wake.

Kitengo cha Matibabu cha bara Ulaya EMA - shirika linalodhibiti matibabu Ulaya pia linakutana Jumanne . limekuwa likisema awali kwamba chanjo hiyo inaweza kuendelea kutolewa.

AstraZeneca inasema kwamba utathmini wa watu milioni 17 waliopatiwa chanjo hiyo barani Ulaya ulibaini kwamba kulikuwa na matukio 37 ya watu waliopatikana na mgando wa damu .

Wataalam wanasema kwamba mgando wa damu ulioripotiwa sio wa kiwango cha juu katika umma.

Matukio yanayohusu mgando wa damu , mingine yakiwa na matukio ya platelets za kiwango cha chini yametokea katika idadi ndogo ya watu wanaopata chanjo hiyo.

''Maelfu ya watu wameripotiwa kuwa na mgando katika damu kila mwaka barani Ulaya kwasababu tofauti'', EMA ilisema.

Je mataifa ya Ulaya yanafanya nini?

Baadhi ya mataifa yamesitisha kwa muda utumizi wa chanjo hiyo , ikiwemo Ujerumani, Ufaransa, Italia na Uhispania.

Yanasema kwamba yalikuwa yanasitisha usambazaji wake kutokana na ripoti za mgando wa damu katika baadhi ya watumiaji wake.

Mgando wa damu hutokea ndani ya damu suala ambalo linaweza kuhatarisha Maisha ya muhusika iwapo hatopata matibabu ya haraka.

Mataifa hayo yalisisitiza kwamba ni hatua ya tahadhari. '

''Huu ni uamuzi wa kitaalam , waziri wa Afya wa Ujerumani Jens Spahn alisema akiongezea kwamba alikuwa anafuata mapendekezo ya taasisi ya chanjo.

Lakini watalaamu kadhaa wa tiba na wanasiasa Ujerumani , ambapo maambukizi yanaongezeka wamehoji kwamba chanjo hiyo inapaswa kutumika hadi kuthibitishwa kwamba sio salama.

''Astrazeneca ndio chanjo ya pili muhimu kwetu'', alisema Christopher Spinner, daktari mwandamizi kutoka chuo cha kiufundi cha mjini Munich . ''Matukio hayo sio ya kawaida''.

Mataifa mengine ikiwemo Austria , yamesitisha matumizi ya baadhi ya chanjo hiyo huku Ubelgiji , Poland, Czech na Ukraine zikisema kwamba zitaendelea kutoa chanjo ya AstraZeneca.

Ongezeko la visa zimefanya mataifa mengine kuimarisha masharti na kuna wasiwasi kuhusu kasi ya utoaji wa chanjo barani Ulaya ambayo tayari imeathiriwa na uhaba wake.

Nchini Itali , mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya tiba aliutaja uamuzi wa kusitisha matumizi ya chanjo hiyo kuwa ya kisiasa.

Kwanini uamuzi huo untokana na hatari?

Kutokana na kile kilichochapishwa kufikia sasa kiwango cha kutokea kwa mgando wa damu baada ya kupatiwa chanjo ni kidogo mno katika awamu hii.

Ukilinganisha, hatari ya Covid kwa wale wanaopatiwa ni muhimu.

Mataifa mengi ya barani Ulaya yanaendelea kukabiliana na maradhi hayo miongoni mwa watu walio katika umri wa miaka 70 na Zaidi.

Iwapo wataambukizwa na kuwa na dalili, wana fursa moja kati ya nne kuwa wagonjwa kupitia kiasi na kuhitaji uangalizi wa hospitalini.

Je WHO inasemaje?

Shirika hilo la Afya linasema kwamba linachunguza ripoti za kutokea kwa mgando wa damu .

Siku ya Jumatatu , msemaji alisema kwamba hakuna Ushahidi kwamba matukio hayo yanahusishwa na chanjo hiyo.

"Mara tu WHO inapoelewa kuhusu tukio hili , matokeo yake na mabadiliko yoyote yatawasilishwa kwa umma'', alisema msemaji wa WHO Christian Lindmeier .

Shirika la EMA ambalo kwa sasa linachunguza ripoti hiyo limesema kwamba chanjo hiyo itaendelea kutolewa.

Shirika hilo limesema kwamba faida za kupata chanjo zinashinda hatari ya madhara yoyote.

Mamlaka inayodhibiti tiba barani Ulaya imesema kwamba Ushahidi haumaanishi kwamba chanjo hiyo inasababisha mgando wa damu na kutoa wito kwa raia nchini humo kupata chanjo watakapohitajika kufanya hivyo.

Je Astrazeneca inasemaje?

Kampuni hiyo inasema hakuna ushahidi kuhusu ongezeko la hatari ya mgando wa damu kutokana na chanjo hiyo.

Imesema kwamba kote barani Ulaya na Uingereza kumekuwa matukio 15 ya mgando wa damu katika mishipa ya damu na matukio mengine 22 ya mgando wa damu unaofanyika katika mapafu umeripotiwa miongoni mwa wale waliopatiwa dozi.

Profesa Andrew Pollard , mkurugenzi wa chanjo hiyo ya Oxford aliambia BBC siku ya jumatatu kwamba kulikuwa na ushahidi wa kweli kwamba hakuna ongezeko la matukio ya mgando wa damu nchini Uingereza, ambapo idadi kubwa ya chanjo hiyo imetolewa kufikia sasa.