Morgan Carey: Ndugu ya Maria Carey amshtaki mwanamuziki huyo kwa kumchafulia jina

Iliyochapishwa

Ndugu mkubwa wa mwanamuziki maarufu duniani Mariah Carey anamshtaki msanii huyo kwa kumkashifu na kumsababisha dhiki kutokana na kumbukumbu yake alioandika hivi karibuni.

Morgan Carey , ambaye anataka kulipwa kwa kuchafuliwa jina anasema kwamba kitabu hicho kinadai kwamba yeye anapenda vurugu.

''Kutokana na hilo amepata matatizo ya kiakili na kumuharibia sifa'', wamesema mawakili wake.

Kesi hiyo imewasilishwa mwezi mmoja baada ya dadake Mariah kumshtaki kwa gharama ya $1.25m kufuatia uchapishaji wa kumbukumbu hiyo.

Alison Carey anasema kwamba vifungu vinavyodai kwamba alijaribu kumpatia dawa ya kumtuliza mtoto wa miaka 12 Mariah , na baadaye kumrushia chai iliokuwa ikichemka yalikuwa ya uzushi na yaliolenga "kumdhalilisha na kumuaibisha".

Alikana, madai hayo akisema kwamba msanii huyo hakutoa ushahidi wowote ili kuthibitisha madai hayo.

Kumbukumbu hiyo ya Mariah iliochapishwa Septemba iliopita na mauzo yake kuongoza mwezi Oktoba. Inahusu ufichuzi mwingi kuhusu maisha yake ikiwemo matatizo aliyokumbana nayo, kulelewa vibaya, ubaguzi wa rangi aliopitia akiwa mtoto na madai kwamba ndoa yake ya kwanza kwa afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya kurekodi muziki Tommy Motolla ilikuwa ya unyanyasaji.

Morgan Carey, aliezaliwa 1960, anasema kwamba nyota huyo alimuharibia sifa yake kwa kuandika kuhusu 'vita vikali' na babake ambavyo vilitokea wakati alipokuwa msichana mdogo.

Mariah aliandika kwamba ilichukua maafisa 12 wa polisi kuwatawanya ndugu yangu na baba yangu - lakini Morgan anasema kwamba tukio hilo halikuwa la kweli na kwamba katika hali ya kawaida ni maafisa wawili wa polisi ambao wangefika kukwamua mzozo wa kinyumbani.

Pia amemshtaki kwa vifungu vinavyosema kwamba alijaribu kumuibia fedha Mariah baada ya kufanikiwa; na kwamba rekodi zake zipo katika mfumo wa uhalifu wa taifa hilo.

''Morgan anaonyesha vitendo hivi kama usaliti mkubwa wa dadake na uongo mbaya kuliko hasira walizonazo'', mshtaka yaliowasilishwa katika mahakama ya Manhattan yalisema.