Mzozo wa Tigray Ethiopia: Blinken asema Marekani inasikitishwa na ukatili unaofanyika

Chanzo cha picha, AFP
Marekani imelaani vitendo vya kikatili katika jimbo la Kaskazini la Tigray nchini Ethiopia, na kuutaka Umoja wa Afrika kusaidia kutafuta ufumbuzi kwa kuwa ''hali inaendelea kuwa mbaya.''
''Tunasikitishwa na hali mbaya ya kibinadamu,'' alisema Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Anthony Blinken.
Ripoti ya shirika la Amnesty lilisema uhalifu dhidi ya binadamu unawezakana kuwa ulitekelezwa.
Mamia wameuawa na maelfu wamekimbia makazi yao katika kipindi cha miezi minne.
Mgogoro uliibuka tarehe 4 mwezi Novemba 2020 wakati serikali ya Ethiopia ilipoanzisha mashambulizi ya kukiondoa chama cha Tigray People's Liberation Front (TPLF) baada ya wapiganaji wake kuvamia makambi ya jeshi la serikali huko Tigray.
Katika ripoti iliyotolewa juma lililopita, Amnesty International imeshutumu vikosi vya nchi jirani ya Eritrea kwa kuua mamia ya watu mjini Aksum tarehe 28 na 29 mwezi Novemba, likisema kuwa mauaji ya watu wengi yanaweza kuwa uhalifu dhidi ya binadamu.
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, aliliambia bunge tarehe 30 mwezi Novemba mwaka jana kuwa ''hakuna raia hata mmoja aliyeuawa'' wakati wa operesheni.
Lakini mashuhuda wameeleza jinsi walivyoanza kuzika baadhi ya miili ya raia ambao hawakuwa na silaha waliouawa na wanajeshi wa Eritrea-wengi wao wavulana na wanaume waliopigwa risasi mitaani au wakati wa uvamizi wa nyumba kwa nyumba.
Shuhuda mmoja ameiambia BBC jinsi miili ilivyobaki mitaani kwa siku kadhaa bila kuzikwa, miili mingi ikiliwa na fisi.

Chanzo cha picha, Google © 2021 Maxar Technologies
Kukatwa kwa mawasiliano na kuzuiwa kuingia Tigray kumefanya yale yanayoendelea kutokana na mgogoro kushindwa kuripotiwa.
Hatahivyo, Waziri wa habari wa Eritrea Yemane G Meskel ametupilia shutuma kutoka kwa Amnesty, akiziita za ''kijinga'' na ''uzushi''.
Lakini Tume ya Haki za Binadamu ya Ethiopia imesema ripoti ya Amnesty international yapaswa ''kuzingatiwa'' na kuwa inafanyia uchunguzi shutuma hizo.

Chanzo cha picha, AFP
Pamoja na kutangaza ushindi baada ya vikosi vitiifu kwa serikali kudhibiti mji wa Mekelle mwishoni mwa mwezi Novemba, mapigano yameendelea eneo hilo.
Usalama na hali ya kibinadamu imezorota, huku kukiwa na ripoti za kuongezeka kwa unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanawake.
Juma lililopita Shirika la mpango wa chakula duniani (WFP) liliomba kiasi cha pauni milioni 72 ili kupambana na changamoto ya ukosefu wa chakula jimboni Tigray.
Shirika hilo limesema watu milioni tatu -karibu nusu ya watu wa Tigray- wanahitaji msaada wa chakula.












