Vita vya Syria: Ndege za Urusi zashambulia maeneo ya IS katika eneo la jangwa

Wanajeshi wa Urusi wamepelekwa Syria kuunga mkono serikali tangu 2015

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Urusi wamepelekwa Syria kuunga mkono serikali tangu 2015
Iliyochapishwa

Ndege za kivita za Urusi zimefanya mashambulizi kadhaa ya anga katika maeno ya wanamgambo wa IS kwenye jangwa la Syria, wanaharakati wamesema.

Jeti hizo zinaunga mkono operesheni za vikosi vinavyounga mkono serikali ya Syria ili kudhibiti barabara kati ya Homs na Deir al-Zour, kwa mujibu ya waangalizi.

Wanaamgambo wa IS wamefanya uvamizi na mashambulizi hivi karibuni , tukio la karibuni, siku ya Jumatani, wanajeshi tisa na wanamgambo waliuawa.

Waangalizi wa haki za binadamu nchini Syria wenye makazi yao nchini Uingereza, ambao wanafuatilia vita nchini Syria kwa kutumia vyanzo vya kimtandao , wamesema watu wengine watatu waliuawa siku ya Jumanne baada ya bomu lililotegwa ardhini na wanamgambo wa IS kulipuka katika jangwa Kusini mashariki mwa jimbo la Deir al-Zour

Mashambulizi ya anga ya Urusi siku ya Jumanne yaliua wanamgambo takribani 10 mjini Deir al-Zour na katika jimbo la Hama, wakati kukiwa hakuna taarifa za madhara kutokana na mashambulizi ya Jumatano katika eneo la al-Shawla.

Ramani ya Syria

Televisheni ya Syria, Televisheni ya upinzani, pia imesema kuwa ndege za Urusi zilikuwa zikishambulia maeneo ya wanamgambo wa IS kwenye jangwa mkoa wa Badiya.

Hatahivyo, vyombo vya habari vya serikali havisema chochote kuhusu operesheni iliyoripotiwa.

IS ilidhibiti eneo la kilomita za mraba 88,000 za mamlaka ya Syria umbali wa kutoka Magharibi mwa Syria kwenda Mashariki mwa Iraq na kuweka utawala wake wa kikatili kwa watu karibu milioni nane.

Licha ya kushindwa kwa kundi hilo huko Iraq mnamo 2017 na Syria mnamo 2019, wataalam wa UN wanakadiria kuwa zaidi ya wanamgambo 10,000 wanaendelea kufanya kazi katika eneo hilo, wakifanya uasi wa muda mrefu.

Wamejiunga makundi madogo madogo wakiwa wamejificha jangwani na vijijini, na yana uwezo wa kuvuka mipaka isiyo na ulinzi.

Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kupambana na ugaidi, Vladimir Voronkov, alionya wiki iliyopita "kuwa mabaki haya makundi ni kubwa ulimwenguni''.

Katika tukio tofauti siku ya Jumatano, polisi wa Uturuki walisema wamewakamata wanachama wawili waandamizi wa IS huko Ankara na kumwachilia msichana wa miaka saba kutoka jamii ya wachache ya Yazidi ya Iraq ambaye alikuwa anashikiliwa mateka. Mmoja wa washukiwa alitambuliwa kama afisa wa zamani wa jeshi la Iraq