Benjamin Acheampong: 'Hawawezi kutuchukulia kama wanyama,' asema mchezaji aiyelaghaiwa dola milioni 1

Iliyochapishwa

Benjamin Acheampong anasema alilaghaiwa akatoa dola milioni 1 na klabu moja ya mpira wa soka na amedhamiria kwamba hili halitawahi kutokea tena - hasa na klabu ile ile.

Mchezaji huyo raia wa Ghana alidhulumiwa zaidi ya dola milioni moja kufuatana na timu kubwa ya Misri, Zamaleck kuanzia mwaka 2018 na licha ya mahakama ya Usuluhishi wa mizozo katika michezo (CAS) kuagiza timu hiyo ambayo imekuwa mabingwa wa Afrika mara tano kumlipa mchezaji huyo kiasi sawa na hicho miezi miwili iliyopita, anasema bado hajapokea kima hicho.

"Hii si sahihi kabisa- hii ndio kazi yangu inayoniwezesha kukimu mahitaji ya familia yangu," kijana huyo, 30, amezungumza na BBC Spoti. "Haiwezekani waanze kuchukulia watu kama wanyama. Pia sisi ni binadamu na tulikuja hapa kufanyakazi."

Kama moja ya vilabu vikubwa Afrika kinadaiwa kwamba kilitumia vibaya mkataba wa mchezaji huyo ambaye hawakuwa na haja naye tena, kimeshutumiwa na mahakama ya CAS yenyewe kwa ukosefu wa maadili, kutumia njia za kutishia mchezaji bila huruma.

Acheampong, mshambuliaji huyo alijiunga na klabu hiyo ya Cairo kwa mkataba wa miaka minne mwaka 2017 lakini mkataba wake ukafutwa miezi 11 baadaye, na akasema kuwa kwamba Zamalek haikuwahi kumlipa vizuri.

Anasema kwamba alipojiunga na klabu nyingine ya Misri ya Petrojet kwa makubaliano ya mkopo kwa miezi mitano mwaka 2018, alilaghaiwa na kusaini nyaraka ambayo ilisema kwamba sio tu ataachana na mshahara wake na klabu ya Zamalek wakati atakuwa anachezea timu ya Petrojet - lakini pia mkataba wake wote.

Na hivyo ndivyo anavyosema alivyoporwa pesa zake zaidi ya dola milioni 1 bila kujua.

"Hakuna anayeweza kufanya hivyo," amesema Acheampong. "Kile ambacho ninajua nilitia saini, ilikuwa ni kwamba klabu ya Petrojet itanilipa kwa kipindi cha nusu msimu ambacho nitacheza nayo."

Desemba, Cas ilisema kwamba Acheampong alilazimika kwasababu kadhaa, kukatisha mkataba wake na Zamalek, ambayo sasa hivi inahitajika kumlipa dola milioni 1.1.

Na ilipofika wakati inaonekana ni kana kwamba atapokea pesa zake, kukatokea jingine jipya.

Zamalek ni moja ya vilabu vinavyoungwa mkono kikamilifu nchini Misri na kote Mashariki ya Kati.

Katika barua iliyotumiwa Fifa, Zamalek - ilitangaza kwamba imefikia makubaliano na ajenti wa mchezaji huyo ambapo raia huyo wa Ghana alikubali kupokea kima cha dola 250,000.

Na ilhali ajenti anayetajwa- ambaye alikuwa nahodha wa klabu hiyo ya Misri Nader El Sayed - hamuwakilishi tena mchezaji Acheampong, mchezaji huyo amesema. Anadai kwamba mchezaji huyo wa Misri ilitafuta makaratasi bandia akijifanya kwamba anaweza kuwasiliana na iliyokuwa klabu yake kwa niaba ya Acheampong.

El Sayed, ambaye nyaraka zake zinaonesha kwamba atapokea asilimia 20, ameliambia shirika la BBC kwamba nyaraka hizo "zimeidhinishwa" na ni "rasmi".

"Hoja ya kwamba Acheampong - wiki mbili tu baada ya uamuzi uliotolewa na Cas - ghafla angemuidhinisha mtu wa kando kufikia makubaliano ya chini ya asilimia 25 ya kiasi cha pesa ambacho alihitajika kupewa hilo ni kinaya," amesema Roy Vermeer, mshauri wa kisheria katika shirika la Umoja wa Wachezaji Duniani Fifpro.

Acheampong bado hajapokea pesa zozote kutoka kwa Zamalek klabu iliyoagizwa kumlipa hata hiyo hundi ya dola 250,000 - ambayo haitaki - iliyotolewa kwa jina lake kima ambacho anadai kilipewa El Sayed.

Alhamisi, Fifa,ambayo imefungua kesi ya utovu wa nidhamu dhidi ya Zamalek, huenda ikatoa uamuzi wa kupiga klabu hiyo marufuku ya kusajili wachezaji na pengine hata huenda ikapunguziwa pointi na kushushwa daraja.

"Ni lazima waadhibiwe," amesema Acheampong

'Zamalek ilikosa maadili'

Zamalek ilishinda kombe la Super Cup 2020 lakini ikapoteza katika fainali ya kumtafuta bingwa dhidi ya mahasimu wao Al Ahly.

Timu hiyo iliyoundwa mwaka 1911, Zamalek ni moja ya vilabu maarufu sana Afrika - ambapo Misri ni taifa ambalo limefanikiwa sana barani Afrika kwa kuzingatia klabu na hata wachezaji wa kimataifa na Mashariki ya Kati.

Nyumbani na nje ya nchi, mahasimu wa timu hiyo Al Ahly ndio pekee wameweza kuichabanga Zamalek katika rekodi ya taji la Afrika ambalo imelichukua kwa mara tano na mataji 12 ya Misri.

"Nilikuwa na furaha sana wakati ninajiunga na timu hiyo," amesema Acheampong, aliyekuwa katika timu ya vijana kimataifa nchini Ghana, wakati anakumbuka uhamisho huo Septemba mwaka 2017. "Ikiwa umepata fursa ya kuchezea Zamalek, wewe ni mchezaji mzuri."

Alijitokeza mara ya kwanza mnamo mwezi Desemba baada ya kufunga mara mbili kabla ya kuanza kushikilia nafasi za mshambuliaji mkuu. Lakini mwezi mmoja baadaye, kocha wa Zamalek alibadilishwa na mwingine ambaye mipangilio yake haikwendana na mchezaji huyo raia wa Ghana akachukua usukani.

Mwishoni Januari, Acheampong alitolewa kwa mkopo katika klabu ya Petrojet, na kutia saini mkataba - unaosemekana haukutimiza maadili kulingana na Cas - ambapo inadaiwa alitupilia mbali zaidi ya dola milioni.

"Kwasababu mkataba wote ulikuwa na thamani ya dola 1,225,804, hii ina maanisha kwamba alikubali dola 1,110,719 zikapotea, kwasababu klabu hiyo ilimlipa mchezaji huyo dola 115,085 pekee," Cas ilisema hivyo mnamo mwezi Desemba.

Wakati anajiunga na timu ya Petrojet kwa mkopo, Acheampong alistahili kuwa amelipwa dola 210,000 na Zamalek - lakini kima alichokuwa amepokea kilikuwa kimezidi nusu tu ya kiasi hicho - na baada ya mkataba wake wa mkopo kuisha, malipo mengine yaliyokuwa yamefikiwa ya dola 72,500, hayakuwahi kutimia.

"Kitaluma, huwezi kukosa kulipwa kwa miezi mitatu kulingana na sheria za Fifa utakuwa huru kuondoka. Kwa hiyo nikawa nasubiri hilo."

Baada ya kurejea kutoka kwa makubaliano ya mkopo, Acheampong alifungiwa kuingia katika timu ya kwanza na kufanya mazoezi pia na badala yake akawa anafanya mazoezi na timu ya vijana - dai ambalo Zamalek inakanusha lakini raia huyo wa Ghana ana ushahidi unaothibitishwa hilo.