Milio ya risasi yasikika Mogadishu wakati wa maandamano

milio
Iliyochapishwa

Milio ya risasi imeripotiwa kusikika katika mji mkuu wa Somali, Mogadishu, wakati kundi la viongozi wa upinzani likiwa limekaidi wito wa serikali wa kutaka watu kuepuka mikusanyiko na kuwa na maandamano.

Safari za kimataifa pia zimesitishwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Aden Adde uliopo mjini Mogadishu.

Maandamano ya amani yameanza yanayoongozwa na mgombea Urais kutoka upinzani Abdirahman Abdishaku wa chama cha Wadajir yameanza mjini Mogadishu.

Maandamano hayo yameanza licha ya serikali kufunga barabara na kupiga marufuku mikusanyiko ya watu.

Usalama umeimarishwa katika mji wa Mogadishu kabla hata ya kuanza kwa maandamano hayo yanayopinga serikali na pia milio ya risasi ilikuwa ikisikika.

.

Chanzo cha picha, SM

Maelezo ya picha, Viongozi wa upinzani ni miongoni mwa watakaoshiriki maandamano

Vurugu zilizotokea jana usiku

Wanajeshi wa serikali na vikosi waaminifu kwa wagombea wa upinzani, walianza kufyatuliana risasi Alhamisi saa saba usiku katika hoteli ya Maida karibu na makazi ya rais ambapo waliokuwa marais wa Somali walikuwa wanaishi.

Serikali na viongozi wa upinzani walikuwa wameshutumiana kwa kushambuliana ambapo katika mkutano wa wanahabari, waliokuwa marais wawili na viongozi wengine wa upinzani walishutumu serikali kwa kuvamia hoteli ya Maida waliokokuwa wanaishi.

Aliyekuwa rais wa Somalia Hassan Sheikh alisema "Inasikitisha kuona kwamba rais anayeondoka anamwaga damu ya raia ambao wanajitayarisha kufanya maandamano ya mania kuelezea maoni yao."

Xasan Xundubey Jumcaale

Chanzo cha picha, SNTV

Maelezo ya picha, Hassan Xundubey Jum'ale waziri wa mambo ya ndani nchini Somali

Akijibu madai hayo, waziri wa mambo ya ndani, Hassan Xundubey Jum'ale alitoa taarifa inayosema shambulizi hilo lilitekelezwa na vikosi wanaounga mkono wagombea wa urais na kuongeza kuwa serikali ilijibu tu shambulio hilo.

Barabara zote mjini Mogadishu zimefungwa na serikali imepeleka wanajeshi wa kitengo maalum kuimarisha usalama.

Pia imefunga njia zote za kuingia eneo la Daljirka ambako waandamanaji wa upinzani walikuwa wanapanga kufanya maandamano na kukutana huko.

Hadi kufikia sasa hakuna anayejua idadi ya waliojeruhiwa katika shambulio lililotokea jana usiku na kuna hofu kwamba hali huenda ikaendelea kuwa mbaya.

Madhumuni ya maandamano hayo ni nini?

Katika barua iliyoandikiwa wizara ya mambo ya ndani, baraza la wagombea wa upinzani lilisema kuwa katiba ya nchi hiyo inawaruhusu kufanya maandamano.

"Kifungu cha 20 cha katiba kinatoa uhuru wa kukusanyika na kufanya maandamano kinachoelezea kuwa kila mmoja ana haki ya kupanga na kushiriki maandamano ya amani bila kuomba ruhusa.

Madhumuni ya maandamano hayo ni upinzani kuonesha kwamba inapinga serikali wanayoielezea kama "wasioitambua na iliyopitwa na wakati".

.

Chanzo cha picha, SOCIAL MEDIA

Ingawa hali katika mji wa Mogadishu ni kama imerejea kuwa tulivu, bado kuna hofu ya kutokea kwa ghasia zaidi.

Serikali ya Somali imeonya dhidi ya kushiriki maandamano kwasababu nchi hiyo sasa hivi inapitia wakati mgumu kukabiliana na ugonjwa wa corona uliojitekeza tena nchini humo.

Wakati huo huo, Wizara ya Usalama imesema kuwa maandamano hayo huenda yakahatarisha zaidi hali ya sasa hivi.

Ubalozi wa Marekani nchini Somali pia umeonya raia wake juu ya hatari iliyopo katika maandamano na kupendekeza:

  • Wasikaribie maeneo ya maandamano
  • Wafuatilia kwa karibu vyombo vya habari vya eneo
  • Kuepuka mahali penye watu wengi
  • Wasijitambulishe wao ni kina nani
  • Na kuhakikisha wako mahali salama

Muhula wa Rais Mohamed Abdullahi Farmajo wa miaka minne ulikamilika Februari 8.

Makundi ya upinzani yamekuwa yakitoa wito ajiuzulu ingawa serikali imesema kuwa rais atasalia madarakani hadi utawala mpya utakapochaguliwa.

Hata hivyo hakuna tarehe iliyowekwa ya kufanya kwa uchaguzi.