Jean-Michel Sama Lukonde kuimarisha usalama Mashariki mwa DRC

Iliyochapishwa

Kufuatia uteuzi wake Jean-Michel Sama Lukonde Kyenge, amesema usalama utakuwa ni moja ya maeneo atakayoyapa kipaumbele, hususan katika eneo la mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo pamoja na katika jimbo la Katanga.

Waziri Lukonde ambaye ni Waziri wa zamani wa michezo ameteuliwa na Rais Felix Tshisekedi Jumatatu kuchukua nafasi ya Sylvestre Ilunga Ilunkamba, mshirika wa Joseph Kabila ambaye alijiuzuru mwezi uliopita baada ya kupigiwa kura na wabunge ya kutokuwa na imani nae.

Kuondoka wa Sylvestre Ilunga Ilunkamba ilikuwa ni ishara ya mwisho ya muungano wa serikali ya muungano baina ya chama cha Rais Tshisekedi na chama cha Kabila.

Waziri Mkuu mpya pia amesema kuwa serikali atakayoiongoza itawajumuisha wanawake na vijana zaidi.

Sama Lukonde amechukua wadhifa huo mpya baada ya kuongoza kampuni ya madini na aliwahi pia kuwa kiongozi wa waziri wa vijana na michezo nchini humo.

Lukonde mwenye umri wa miaka 43-ana mwezi mmoja tu wa kuunda serikali utakaoongoza kile kinachoitwa ''muungano mtakatifu'', wa walio wengi bungeni, baada ya kuvunjika kwa muungano baina ya Rais Tshisekedi na matangulizi wake Joseph Kabila.

Uteuzi wa Bw Sama Lukonde kama Waziri Mkuu ni hatua ya hivi karibuni ya Rais Tshisekedi ya kuwachagua viongozi wake binafsi kuchukua uongozi wa ngazi ya uwaziri katika serikali, ambayo imepitia historia ya misukosuko ya kisiasa, kabla ya kipindi cha makabidhiano ya madaraka kwa njia ya amani mwaka 2019.

Uteuzi wa Bw Lukonde umekuja kama wa kushangaza kwa baadhi ya wanasiasa wa DRC kwani wengi walidhani Rais Tshisekedi angemteua Waziri Mkuu kutoka katika majina mashuhuri kama vile Moise Katumbi , Bahati Lukwebo na Jean Pierre Bemba.

Jean-Michel Sama Lukonde ni nani?

Lukonde si maarufu sana katika siasa za DRC.

Aliingia katika Nyanja za siasa mwaka 2003 kwa mara ya kwanza.

Ni mzaliwa wa jimbo lenye utajiri wa madini nchini Congo la Katanga na aliteuliwa mwaka 2008 na Rais Tchisekedi kuongoza kampuni ya serikali ya madini -GECAMINES baada ya kujiunga na chama Rais Tshikedi.

Aliwahi kuchaguliwa kama mbunge katika uchaguzi wa mwaka 2006, akiwa na umri wa miaka 26.

Baadaye alikuwa waziri wa michezo ,lakini baadae alijiuzulu na kujiondoa kwenye muungano uliokuwa ukimuunga mkono Moise katumbi na kumuunga mkono Rais Tshisekedi.