Virusi vya corona: Jinsi corona inavyoathiri maisha na utamaduni wa kiswahili

Dunia nzima sasa inasumbuliwa na ugonjwa wa Corona. Mamilioni ya watu wameshaugua huku maelfu wakiwa wamepoteza dunia. Ugonjwa huu hauchagui tajiri wala masikini na unaambukiza watu wa dunia.
Hata hivyo, kuondoa sababu nyingine za kisayansi kuhusu kuambukiza au kutoambukizwa, ugonjwa huu umeleta changamoto nyingi kwa watu ambao kwa asili, wana utamaduni wa kuchangamana.
Wakati Corona ilipoanza kusikika kwa mara ya kwanza mwaka jana, kuliibuka mjadala mkubwa kuhusu ni kwa vipi China ilipata ugonjwa huo na ikaathirika sana lakini jirani zake - Japan, hawakupata tatizo kama hilo.
Dunia ikaja kufahamu baadaye kwamba kilichoikoa Japan; pamoja na mambo mengine ya kisayansi, ni utamaduni wake. Wajapani hawana utamaduni wa kusalimiana kwa kushikana mikono wala kukumbatiana. Wenyewe husalimiana kwa kuinamisha vichwa tu.
Utamaduni wao huo ukawaokoa na Japana haikuumizwa sana na ugonjwa huo kama ilivyokuwa kwa jirani zao hao.
Ni kwa vipi ugonjwa huu unaleta maswali mapya kwa jamii za Afrika? Kwa sababu makala haya yatasomwa zaidi na jamii zinazozungumza lugha ya Kiswahili; ni muhimu kuangalia ni kwa vipi ugonjwa huu umeathiri watu.
Shughuli ni watu ati
Miongoni mwa misemo maarufu ya lugha ya Kiswahili ni ule usemao kwamba shughuli ni watu. Msemo huu humaanisha kwamba kufanikiwa au kutofanikiwa kwa tukio lolote muhimu la kijamii - hutokana na idadi ya watu.

Chanzo cha picha, Getty Images
Harusi itakuwa kubwa endapo tu itahudhuriwa na watu wengi. Mtu mashuhuri akifariki, kupendwa kwake kutaonekana kwa kuzikwa na umati wa watu.
Ugonjwa wa Corona umeleta mtihani mkubwa kwenye jamii ya Waswahili kwa sababu kisayansi, ugonjwa huu husambazwa kwa njia ya hewa na palipo na mkusanyiko mkubwa, ndiyo hasa uwezekano wa kusambaa kwa kasi zaidi hujitokeza.

Katika zama hizi za Corona, zipo familia katika majiji ya Dar es Salaam (Tanzania) na Mombasa (Kenya) ambako utamaduni wa Kiswahili umetamalaki, ambazo ziliamua kuwa wasiende kwenye msiba wa mpendwa wao kwa sababu ya kuepuka msongamano.
" Marehemu baba alikuwa mtu wa watu hasa na watu wengi wangetamani kupata fursa ya kumzika alipofariki. Lakini, kuita watu nyumbani kwetu ambako tuna bibi mtu mzima mwenye magonjwa hatarishi kwa Corona lingekuwa jambo la hatari.
" Bibi mwenyewe alikuwa Analia tu kwamba watoto tumezuia watu wasimzike mpendwa wao kwa hadhi yake lakini ndiyo watoto tukashikilia msimamo wetu. Msiba ukawa wa kifamilia na sote tuko salama," anasema Ahmed M, mkazi wa Mbweni jijini Dar es Salaam.
Mahudhuria katika sherehe au misiba ni mojawapo ya misingi mikuu ya utamaduni si wa Waswahili pekee bali Waafrika kwa ujumla na bila ugonjwa huu mpya wa Covid umeleta changamoto kubwa katika mila na utamaduni huu.
Wanaopendana hula pamoja
Kwa muda mrefu, kwa sababu ya mazoea na utamaduni, ni kawaida kwa Waswahili kula kwa pamoja nyakati za mlo. Kimsingi, katika maeneo kama Dar es Salaam kulikuwa kumeanza kujengeka utamaduni wa watu kukutana na kula pamoja siku za Ijumaa.

Katika mgahawa mashuhuri wa Chef Pride uliopo katikati ya jiji, ni kawaida kwa watu mbalimbali kukutana na kula pilau au biryani kwa pamoja. Kuna utamaduni ulianza kujengwa kwamba mara watu watokapo katika ibada ya Ijumaa, njia huwa moja tu; kwenda kula.
Utamaduni huu umepata changamoto katika nyakati hizi. Ili watu wengi kujihisi wamekula pamoja, huwa wanaagiza sinia moja lililojaa biryani na nyama. Ili kula vizuri, ni lazima watu hawa wakae jirani jirani.
Huu huwa ni muda si wa kula pekee bali wa kupeana taarifa, utani na vicheko. Tabia zote hizo ni hatari katika wakati wa Corona. Kwa hiyo sasa, kabla mtu hajaita wenzake anaowapenda kwenda kula nao, huwa anajiuliza swali moja - kuna umuhimu wa kuhatarisha maisha yangu kwa ajili ya pilau au biryani?
Kusitiri marehemu
Huwezi kuzungumza kuhusu utamaduni wa Waswahili bila ya kuzungumzia dini yao. Wengi wa Waswahili ni Waislamu na katika dini yao kuna taratibu zimewekwa kwa ajili ya kusitiri marehemu kabla hawajazikwa.
Kama marehemu alifariki kwa ugonjwa wa Corona au wowote ule unaoweza kuambukiza, ni jukumu la wale wanaotakiwa kumsitiri kuhakikisha hawahatarishi maisha yao wakati wa kusitiri marehemu.
Kama ikionekana kwamba kuna hatari kwa wanaofanya kazi hiyo endapo marehemu alikufa kwa ugonjwa huo, kuna uwezekano mkubwa kwamba taratibu hizo zisifuatwe.
Kwa Mswahili na Muislamu, ni jambo la kuumiza roho kuona mpendwa akienda kuzikwa pasipo kufanyiwa taratibu zote za maiti kwa mujibu wa maelekezo ya vitabu vya dini. Lakini ugonjwa wa Corona umeleta hali hii na kwa bahati nzuri vitabu vya dini vina maelekezo mahususi kabisa kuhusu nini kinatakiwa kufanywa wakati wa magonjwa ya kuambukiza kama hili.
Unaweza pia kusoma:
Utani wa kipimo cha Covid 19 kutoka China
Si watu wengi walikuwa watu wazima wakati wa ugonjwa wa mafua makali (Spanish Flu) wa mwaka 1920 ulipopiga eneo la Afrika Mashariki. Mamilioni ya watu waliugua wakati huo lakini Waswahili bado wapo na wanadunda.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ni matarajio ya wengi kwamba wimbi hili la Corona litapita na mwishowe watu wataendelea na maisha yao kama kawaida. Kama ilivyo kawaida yao - pamoja na machungu yote wanayopitia, Waswahili wanaendelea kupashana taarifa na kutaniana kuhusu ugonjwa huu.
Kwa mfano, sasa wanataniana kuhusu kipimo cha Covid 19 kutoka China. Inaonekana, wako Waswahili walio tayari kwenda kaburini kuliko kukubali kupimwa Corona kwa njia ya Kichina.
Lakini usifikiri huo ndiyo ukweli. Wanataniana tu. Ikifika wakati wa kuokoa maisha yao kwa kuchanja, utawaona Waswahili wakiibuka na utani mwingine kujitetea kwanini wamekubali kipimo cha Mchina.












