Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mapinduzi ya Misri: 'Siku iliyokuwa imejaa hisia mbalimbali, waliokusanyika kila mmoja akipaza sauti kivyake'
Miaka kumi iliyopita, uwanja wa Tahrir katikati mwa Cairo ndio uliokuwa chanzo cha maandamano dhidi ya Rais Hosni Mubarak na serikali.
Mpiga picha Laura El-Tantawy alikuwa mmoja wa walioangazia maandamano hayo ambayo yalikuwa yanazidi kuongezeka na yaliobadilika na kuwa mapigano kati ya wanaopendelea na wasiopendelea serikali ya Mubarak na kutaka kumuondoa madarakani.
El-Tantawy alikuwa Italia maandamano yalipoanza katika mji mkuu wa Misri lakini alikuwa amedhamiria kufika eneo hilo licha ya kufahamu hatari zilizopo.
"Niliogopa sana kuwa hapo hasa kutokana na taarifa nilizokuwa ninazisikiliza - kukatwa kwa umeme, kukatwa kwa intaneti kote nchini humo, wavamizi waliokuwa juu ya paa wakiwafyatulia risasi waandamanaji na kulenga wapiga picha - na hasa wawakilishi wa vyombo vya habari."
Hata hivyo, mwishoni, El-Tantawy alihisi kwamba ni tukio la kihistoria na kutaka kulishuhudia.
"Nilipokuwa ninatazama taarifa za habari, nilihisi kuna kitu ambacho ninakikosa.
"Tayari nilikuwa nimeanza kuangazia Misri tangu mwaka 2005. Hakukuwa na shaka yoyote kwamba nilihitajika kuwa katika uwanja wa Tahrir kaangazia tukio hili la kihistoria kama sehemu ya maisha yangu."
Akiwa katika uwanja huo, El-Tantawy aliamini kwenda na vile hisia zake zingemwelekeza ili kuwa salama ingawa kwenda na kutoka katika uwanja huo ndio kulikuwa hatari zaidi kwasababu kulikuwa na makundi ambayo yangeiba kamera na kuvamia wanahabari.
"Picha hii niliipiga Februari 2, 2011," amesema El-Tantawy.
"Hii haikuwa siku nzuri sana katika uwanja wa Tahrir. Ilifahamika kama vita vya Farasi na Ngamia, pale wafuasi wanaompendelea Mubarak waliokuwa wamebeba mapanga na mijeledi ya farasi wakiwa na ngamia walipowasili katika uwanja huo na kuvamia waandamanaji.
"Ilikuwa siku yenye machungu na kushutusha. Nilikuwa kwenye vinjia vya nyuma ya uwanja huo nikipiga picha za waliojeruhiwa."
Likawa ndio moja ya matukio mabaya zaidi ya kumpinga Mubarak yaliyosababisha karibu watu zaidi ya kumi kupoteza maisha.
"Kila wakati nilikuwa naficha kamera zangu nikiwa naondoka kwenye uwanja wa Tahrir," amesema El-Tantawy.
"Mazingira yalibadilika kila siku.
"Ilikuwa eneo ambalo ubaguzi wa rangi, kidini, matabaka ya kijamii halikuwa tatizo. Kila mmoja alikuwa eneo hilo kwa sababu ya kutimiza lengo moja tu. Umoja uliokuwepo katika eneo hilo ulizidi tofauti zozote ambazo zingeibuka."
El-Tantawy alipiga picha Februari 11, 2011, siku ambayo Rais Mubarak alijiuzulu.
"Ilikuwa ni siku ambayo mimi kama mpiga picha nilihisi nimezidiwa na iliyojaa hisia chungu nzima.
"Nilikuwa najitahidi kunasa hisia za watu waliokuwa wamekusanyika, uzito wa siku hii ya kihistoria wakati tunajitahidi kuisherehekea kama raia wa Misri. Nakumbuka sauti, rangi zilizokuwa zimeshamiri na harufu ya wakati huo.
Anga lilikuwa limetanda fataki huku waliokusanyika kila mmoja akipaza sauti kivyake.
"Kilichosalia katika fikra zangu kwenye uwanja huu wa Tahrir ni thamani ya muda ule wa kihistoria.
"Hii ilikuwa ni hisia ya kipekee na mpya kwangu mimi kuhusu Misri - na kuwa na matarajio makubwa siku za usoni kuliko yaliyopita."
Kwa wengi, bila shaka, uwanja huu unatoa kumbukumbu mbaya za waliyopitia. Februari 22, 2012, El-Tantawy alikuwa miongoni mwa wanahabari waliokusanyika nje ya kituo cha polisi katika mji mpya wa Cairo wakisubiri tangazo la ikiwa aliyekuwa Rais Mubarak na waziri wake wa mambo ya ndano wakati huo, Habib al-Adly watashtakiwa kwa makosa ya kutoa maagizo ya kupiga risasi na kuua waandamanaji.
"Siku hii nilikutana na Safeya Abdelaziz Mohamed," amesema El-Tantawy.
"Kijana wake alikuwa miongoni mwa wengi waliofariki dunia wakati wa mapinduzi. Kulikuwa na hisia za kukubali hali na huzuni kwenye uso wake.
"Alitiririkwa na machozi wakati mahakama inatangaza uamuzi wake wa kuwaondolea lawama Mubarak na Adly."
Mwaka mmoja baadaye, El-Tantawy aliangazia hili tena Juni 2013, katika maandamano yaliyotokea uwanja wa Tahrir.
"Wakati huo kulikuwa na taarifa zinazosambaa katika vyombo vya habari kuwa wanawake hawaruhusiwi kushiriki maandamano katika uwanja wa Tahrir kwasababu ya ushawishi wa kundi la Muslim Brotherhood," alisema vuguvugu la kundi la Kiislamu ambako kiongozi wake alikuwa ameshinda urais katika uchaguzi wa kwanza wa urais baada ya kuondoka kwa Mubarak mwaka mmoja kabla.