Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Nourin Mohamed Siddig: Msoma Kurani aliyeupa mtindo wa kiafrika umaarufu
Nourin Mohamed Siddig aliposoma Kurani, watu duniani kote walielezea sauti yake kama yenye kujitokeza ya aina yake, mfano huzuni.
Sauti na mbinu yake ya kipekee ya kughani Kurani kulimfanya awe mmoja wa wasomaji maarufu wa Kurani duniani.
Athari zake, kifo chake akiwa na umri wa miaka 38 kupitia ajali ya gari nchini Sudan mnamo mwezi Novemba aliombolezwa kutoka nchini Pakistan hadi Marekani.
"Dunia imepoteza moja ya sauti ya kipekee kipindi hiki," aliandika ujumbe kwenye mtandao wa Twitter, Imamu Omar Suleiman kutoka Texas.
Hind Makki, msomi, raia wa Marekani mwenye asili ya Sudan alisema ni vigumu kuelezea sifa za usomaji huo.
"Kuna uhalisia wa Afrika ambao huzungumziwa hata kama hawawezi kuelewa moja kwa moja ni nini, wanakifurahia," amesema.
Kwa mujibu wa mwana historia Sylviane Diouf, sala, kukariri na kughani Kurani kwa watumwa Waislamu wa Afrika Magharibi, ambako kunaweza kusikika sawa na vile wanavyosoma Waislamu wengine wa eneo la Sahel hadi nchini Sudan na Somalia, huenda kumechangia "mtindo wa kipekee wa usomaji kwa Wamarekani wenye asili ya Afrika".
Kulingana na utamaduni, Kurani, kitabu kitakatifu kwa Waislamu, huwa kinasomwa kwa mtindo wa kama mawimbi fulani hivi, yaani kupaza na kushukisha sauti kama wimbo, jinsi ilivyokuwa ikihamasishwa Mtume Muhammad (S.A.W), aliyesema kuwa watu wanastahili "kuipendezesha Koran kwa sauti zao".
Mbinu tofauti tofauti za usomaji katika maeneo mbalimbali
Hupendeza zaidi usomaji wa Kurani wakati idadi kubwa ya watu wanajumuika pamoja kwa ajili ya matukio ya kidini kama vile ibada wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani katika sala ya tarawehe.
Pia kuna mashindamo mbalimbali ya kusoma na kukariri Koran kimataifa.
Hatahivyo, kumekuwa na aina mbalimbali za usomaji wa Kurani.
Huenda kukawa na utofauti wa toni na matamshi kulingana na jiografia, utamaduni na kulingana na historia katika dunia ya Kiislamu zaidi ya Mashariki ya Kati.
Usomaji wa Kurani wa Siddiq na pia kifo chake kulileta angalizo kubwa katika mtindo wa kiafrika wa kughani Kurani.
Mtindo wake aliotumia, chanzo chake ni shule ya kitamaduni ya kujifunza kusoma Kurani kijijini mwake, al-Farajab, magharibi mwa mji mkuu wa Khartoum, katikati ya miaka ya 1990.
Na hatimaye alipohamia mji wa Khartoum, aliongoza sala katika misikiti kadhaa mjini na watu wakaanza kupenda jinsi anavyoghani Kurani.
Umaarufu wake ulisambaa pale video zake alipokuwa akisoma Kurani zilipoanza kusambazwa kwenye mtandao wa YouTube.
Wakati sauti zinaelezewa kuwa na kiwango cha noti saba ambacho ni maarufu sana Mashariki ya Kati, usomaji wa Kurani wa Siddig ulikuwa kwa mtindo wa kiwango cha noti tano ambacho ni maarufu katika maeneo ambayo idadi kubwa ya watu ni Waislamu, eneo la Sahel na pembe ya Afrika.
"Hii ndiyo toni ambayo nimekuwa nikiifahamu nilipokuwa ninakua eneo la jangwani; ni kama [muziki wa kitamaduni wa Sudan]", amesema Al-Zain Muhammad Ahmad, msomaji mwingine maarufu wa Kurani nchini Sudan.
"Wanaosoma Kurani eneo la Mashariki huzingatia mfuatano wa sauti, kama ilivyo Misri, eneo la Hijaz, Afrika Kaskazini na kwingineko."
Katika miongo ya hivi karibuni, mitindo ya kughani Kurani Mashariki ya kati imekuwa maarufu kwenye maeneo mengi ya Afrika na kote duniani hasa maeneo ya mijini.
Wasikilizaji wa Koran wamekuwa wakifikia rekodi zilizopo, matangazo ya redio kupitia masafu mafupi, kaseti, CD zilizorekodiwa na kusambazwa au kuuzwa na mashirika kutoka Misri na Saudi Arabia.
Wanafunzi wanaorejea kutoka chuo kikuu cha Al-Azhar cha Misri na chuo kikuu cha Kiislamu cha Medina, pamoja na michango kutoka kwa mashirika ya maeneo ya ghuba, kumesaidia kusambaa kwa umaarufu wa mtindo wa kughani Kurani wa Mashariki ya Kati ikiwemo eneo la Afrika huku wengine hata wakifanya vizuri zaidi katika usomaji wa Kurani.
Lakini intaneti na mitandao ya kijamii kumebadilisha mambo hasa kutoka kizazi kichanga hadi sauti zilizozoeleka.
Kukubalika duniani
Ahmad Abdelgader, mpiga picha za video amekuwa akimrekodi Imam Jabbi wakati anasoma Kurani katika mtandao wa Youtube tangu mwaka 2017.
"Video maarufu iliyorekodiwa ni ile ya dua zilizosomwa kwa mtindo wa Kiafrika [du'a] iliyotazamwa na watu zaidi ya milioni mbili," alisema. "Watu wengi waliokuwa wanatazama walikuwa kutoka Ufaransa ambako kuna idadi kubwa ya Waislamu kutoka Afrika Magharibi ikifuatia na Marekani."
Rekodi hizo pia zimekuwa zikifuatiliwa katika shule mbalimbali za kujifunza kusoma Kurani.
Katika maeneo yenye idadi kubwa ya Waislamu, hasa ya vijijini barani Afrika, baadhi ya shule zinazofunza kughani Koran, hutumia mtindo wa Sudan ambao mara nyingi Siddig aliutumia katika usomaji wake wa Kurani.
Mtindo wake wa kusoma Kurani, ulikuwa unakumbusha mitindo ya kitamaduni ya watu mbalimbali miongoni mwa Waislamu na wafuasi wengi pamoja na waliokuwa waangalizi, bila shaka kuna funzo kubwa hapo.
Wakati maudhui ya Kurani yanakubalika, mitindo mbalimbali ya usomaji wa Kurani inatoa ujumbe kote ulimwenguni kupitia "muunganisho wa sauti nzuri za eneo na wenye kuleta maana kote duniani," ameelezea Profesa Frishkoph.
"Hiki ndio cha msingi."