Lil Uzi Vert: Mwanamuziki wa Marekani ajipandikiza almasi yenye thamani ya '$24m' kwenye paji la uso

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 2

Mwanamuziki wa Marekani ambaye pia ni mtunzi wa muziki Lil Uzi Vert amezua hisia kali mtandaoni baada ya kutumia takribani $24m , kununua almasi yenye karati 11 na kuipandikiza katika paji lake la uso , hatua iliowashangaza wengi.

Kulingana na BBC Pidgin, anasema kwamba alinunua almasi hiyo kutoka kwenye duka la Elliot Eliante kwa $24 millioni.

Lil Uzi Vert alisababisha hisia kali miongoni mwa mashabiki wake kote duniani alipochapisha video inayoonesha muonekano wake mpya na kuandika katika mtandao wa instagram ''Urembo ni Uchungu''{ Beauty is Pain}.

Je Lil Uzi Vert ni nani?

Jina rasmi la Lil Uzi Vert ni Symere Bysil Woods, mwanamuziki wa Marekani wa muziki aina ya Rap , na mtunzi.

Alizaliwa tarehe 31 mwezi Julai 1994 katika makazi ya Kaskazini mwa Philadelphia huko Francisville, nchini Marekani.

Kitu kinachomfanya mwanamuziki huyo kuwa tofauti na wengine ni idadi ya tatoo alizonazo mwilini na jinsi alivyojidunga vipuri usoni , mtindo tofauti wa nywele na mavazi ya zamani.

Lil Uzi alijipatia umaarufu baada ya kutoa wimbo wake wa Luv is Rage mwaka 2015.

Nyimbo nyingine zilizomfanya kuwa maarufu ni pamoja na wimbo wake wa kwanza Money Longer ambao aliutoa mwaka 2016., You was Right, Gucci Mane, Bad na Bouje iliokuwa katika nafasi 100 katika chati za Billboard nchini Marekani mbali na Tour Life iliyomshindia tuzo ya MTV kwa kuwa wimbo bora katika majira ya joto.

Mwanamuziki huyo anadaiwa kuwa na thamani ya dola milioni 16 lakini kati ya mwaka 2017 na 2018 alijipatia zaidi ya dola milioni 20 kutoka katika muziki unaopigwa mtandaoni na maonesho yake mubashara.