Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mzozo wa Tigray: Jinsi wakimbizi wanavyofariki dunia kwa njaa
Vyama vya upinzani nchini nchini Ethiopia katika ukanda wa Tigray vimetaka mapigano yanayoendelea katika taifa hilo yasitishwe mara moja.
Watu tayari wanafariki dunia kwa utapiamlo, ndio maana vyama vya siasa nchini humo vinaomba msaada wa Jumuiya ya kimataifa ili kusaidia taifa hilo.
Serikali ya Ethiopia inasema tayari wanapata msaada ambao umewafikia watu milioni 1.5.
Vyama hivyo vimetangaza kuwa watu 52,000 wameuawa tangu mwezi Novemba.
Ingawa hakuna maelezo yaliyofafanua kuhusu ongezo hilo la vifo, lakini taarifa hiyo inasema miongoni mwa watu waliouawa ni wanawake, watoto na viongozi wa kidini.
Serikali haijasema chochote kuhusu matukio hayo lakini ilisema hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya kiongozi wa zamani wa chama cha Tigray.
Wakimbizi wapatao 100,000 wa Eritrea wanaishi katika kambi ya Umoja wa mataifa Tigray na wameathirika na janga hilo.
Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia wakimbizi (UNHCR) alisema wakimbizi wanakula majani, na wanakabiliana na uhaba wa maji.
Mgogoro wa Tigray umefanya watu wapatao milioni mbili kukimbia makazi yao kwasababu ya ghasia zinazoendelea.
Jumatatu, Mkuu wa kambi ya wakimbizi ya Norway, Jan Egeland, alitangaza kuwa katika miaka 40 aliyofanya kazi ya kutoa huduma za kibinadamu hajawahi kukutana na janga la namna hii.
Katika taarifa ya pamoja, vyama vitatu vya upinzani kikiwemo chama cha Tigray Independence Party (TIP), Salsay Weyane Tigray na National Congress of Great Tigray, vilitangaza kuwa misaada ya chakula na dawa itachelewa, jambo ambalo litafanya hali kuwa mbaya zaidi katika eneo hilo.
Maeneo ua mijini na vijijini yameharibika sana kwasababu ya mabomu yaliyorushwa.
Uharibifu huo umeathiri huduma za afya, elimu na hata sehemu za ibada.
Picha inayoonesha watu 60,000 kutoka ukanda wa Tigray wakiishi katika kambi ya wakimbizi nchini Sudan.
Jumuiya za kimataifa pia nayo imeikosoa serikali ya Ethiopia.
Wiki iliyopita Marekani iliyataka majeshi ya Eritrea kuondoa haraka kikosi chake, taarifa zisizokuwa zimethibitishwa ziliripoti kuwa haki za binadamu zimekandamizwa.
Hata hivyo, serikali ya Ethiopia na Eritrea zimekanusha kupeleka majeshi yao eneo la Tigray.
Chama cha TPLF kiliongoza Tigray katika vita vilivyosababisha mauaji ya watu takriban 250,000 chini ya utawala wake wa miaka 30.
Chama hicho kiliondoka madarakani baada ya serikali ya Ethiopia kuudhibiti mji wa Mekelle, Novemba 28.
Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amekishutumu chama cha TPLF kwa kutishia kuingilia uhuru wa Ethiopia na kujaribu kupindua serikali baada ya chama hicho kudhibiti kambi ya jeshi mwezi uliopita.
Serikali ya Abiy ilitangaza kuwa uchaguzi uliofanyika eneo la Tigray uliendeshwa kinyume na sheria huku TPLF ikisema serikali ya Ethiopia ilikuwa imedhibiti mji wa Tigray kinyume na sheria.