Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Katibu mkuu wa UN aitaka dunia kuhakikisha mapinduzi ya Myanmar yanashindwa
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa wito dunia kuhakikisha kuwa mapinduzi ya Myanmar yaliyotokea Jumatatu yanashindwa.
Kubadilishwa kwa matokeo ya uchaguzi "hakukubaliki", alisema, na viongozi waliotekeleza mapinduzi wanastahili kueleweshwa kuwa hii sio njia ya kutawala serikali.
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linajadiliana taarifa ya pamoja lakini China inatarajiwa kuzuia maneno ya aina yoyote ile yanayoshutumu mapinduzi hayo.
Kiongozi aliyechaguliwa Aung San Suu Kyi alikamatwa na jeshi lilipofanya mapinduzi.
Polisi huko Myanmar - ambako pia kunafahamika kama Burma - baadaye ikawasilisha mashitaka kadhaa dhidi ya Bi. Suu Kyi, ambaye amezuiliwa hadi Februari 15.
Sio Bi. Suu Kyi wala rais aliyeondolewa madarakani Win Myint hakuna kati yao aliyezungumza chochote tangu kutokea kwa mapinduzi hayo.
Mapinduzi hayo yalioongozwa na mkuu wa jeshi Min Aung Hlaing, yamepelekea kutajwa kwa wanajeshi 11 kushikilia nyadhifa mbalimbali za uwaziri.
Jeshi ambalo lilitangaza mwaka mmoja wa hali ya dharura linatafuta namna ya kuhalalisha hatua iliyochukua kwa kudai kwamba uchaguzi uliofanyika Novemba mwaka jana ulikumbwa na udanganyifu, ambapo Bi. Suu Kyi aliyegombea tena urais kwa tiketi ya chama cha National League for Democracy (NLD) aliibuka na ushindi mkubwa.
Kuna taarifa kuwa jeshi limeagiza mtandao wa Facebook ufungwe nchini humo, kwa madai kuwa mitandao ya kijamii inafanya iwe "vigumu kurejesha uthabiti".
Alhamisi, watumiaji walisema kwamba hawakuweza kufikia mtandoa huo. Ukurusa wa Facebook uliundwa kuratibu upinzani katika mapinduzi hayo umependwa na makumi ya maelfu ya watu.
'Haikubaliki kabisa'
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kutekelezwa kwa katiba nchini Myanmar.
Amesema ana matumaini kwamba kutakuwa na umoja katika Baraza la Usalama wakati wa kujadili suala hilo.
"Tutafanya kila tunaloweza kuleta pamoja washikadau muhimu katika jumuiya ya kimataifa kutoa shinikizo zaidi kwa Myanmar kuhakikisha kuwa mapinduzi hayo yanashindwa," alisema.
"Haikubaliki kabisa kubadilisha matokeo ya uchaguzi na matakwa ya wananchi.
Ni matumaini yangu kwamba itawezekana kuelewesha Myanmar kuwa hii sio njia moja ya kutawala nchi na pia sio njia ya kusonga mbale."
Nchi za magharibi zimelaani mapinduzi hayo lakini juhudi za Baraza la Usalama za kufikia uamuzi mmoja zimegonga mwamba kwasababu China inaunga mkono Myanmar.
China ni miongoni mwa wanachama watano wa kudumu wa baraza hilo wenye haki ya kupiga kura ya turufu.
Kwa kipindi kirefu, Beijing imekuwa ikitetea nchini hiyo kwa kuingiliwa kimataifa na imeonya tangu kutokea kwa mapinduzi kuwa vikwazo au shinikizo la kimataifa litafanya mambo kuwa mabaya zaidi.
Pamoja na Urusi, zimekuwa zikilinda Myanmar dhidi ya ukosoaji wa Umoja wa Mataifa juu ya hatua ya jeshi ya kukandamiza kabila la Waislamu walio wachache la Rohingya.
Suu Kyi yuko wapi?
Imeripotiwa kuwa kiongozi aliyechaguliwa na raia nchini Myanmar Aung San Suu Kyi anazuiliwa katika makazi yake mji wa Nay Pyi Taw.
Anakabiliwa na mashitaka kadhaa ikiwemo kukiuka sheria za uingizaji na uuzaji bidhaa nchini humo na umilikiwa vifaa vya mawasiliano ambavyo ni knyume na sheria.
Mashitaka hayo yamewasilishwa mahakamani.
Alirudishwa rumande "kuhoji mashahidi, kuomba ushahidi na kutafuta wakili wa kisheria baada ya kumhoji mshtakiwa," hati hiyo inasema.
Bw.Win Myint anashtakiwa, chini ya sheria ya udhibiti wa majanga ya kitaifa, kwa kukutana na wafuasi katika msafara wa magari 220 wakati wa kampeni na kukiuka masharti ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona.
Mizizi yake ya kisiasa
Bi Suu Kyi ni mtoto wa kike wa shujaa wa uhuru wa taifa hilo Jenerali Aung Sun. Aliuawa alipokuwa na miaka miwili pekee , kabla Myanmar kujipatia uhuru wake kutoka kwa Uingereza mwaka 1948.
Mwaka 1960 alielekea India na mamake Daw Khin Kyi , ambaye alikuwa ameteuliwa kuwa balozi wa Myanmar mjini Delhi.
Miaka minne baadaye alielekea katika chuo kikuu cha Oxford nchini Uingereza ambapo alisomea filosofia , siasa na uchumi. Alipokuwa huko alikutana na mumewe , msomi Michael Aris.
Baada ya kuishi na kufanya kazi nchini Japan na Bhutan , aliishi nchini Uingereza ambapo alikuwa akiwalea wanawe wawili, Alexander na Kim, lakini Maynmar haikuwa mbali na fikra zake.
Wakati alipowasili katika eneo la Yangon mwaka 1988 - ili kumwangalia mamake aliyekuwa akiugua - Myanmar ilikuwa katikati ya machafuko ya kisiasa.
Maelfu ya wanafunzi , wafanyakazi wa ofisini na watawa walifanya maandamano wakitaka mabadiliko ya kidemokrasia.
''Sikuweza kupuuza kile kilochokuwa kikiendelea'' , alisema katika hotuba aliyoitoa katika eneo la Yangon tarehe 26 Agosti 1988.
Aliendelea na kuongoza upinzani dhidi ya dikteta wakati huo jenerali Ne Win.
Kifungo cha nyumbani
Akipatiwa msukumo na kampeni ya amani ya mwanaharakati wa haki za kibinadamu nchini Marekani Martin Luther King na Mahatma Gandhi wa India, alipanga mikutano na kusafiri nchi nzima akipigania mabadiliko ya amani ya kidemokrasia na uchaguzi huru.
Lakini maandamano hayo yalinyamazishwa na jeshi , ambalo lilichukua utawala kupitia mapinduzi ya tarehe 18 Septemba 1988.
Bi Suu Kyi aliwekwa chini ya kifungo cha nyumbani mwaka uliofuatia.
Serikali ya kijeshi iliitisha uchaguzi mwezi Mei 1990, ambapo chama cha Suu Kyi kilishinda kwa wingi wa kura lakini Junta ikakataa kukabidhi madaraka. Bi Suu Kyi aliwekwa chini ya kifungo cha nyumbani katika eneo la Yangon kwa miaka sita , hadi alipoachiliwa Julai 1995.
Aliwekwa tena chini ya kifungo cha nyumbani mwezi Septemba 2000 alipojaribu kusafiri kuelekea katika mji wa Mandalay akikiuka masharti ya kutosafiri.
Aliachiliwa huru bila kufunguliwa mashtaka mwezi Mei 2002, lakini baada ya mwaka mmoja alifungwa baada ya mzozo kati ya wafuasi wakena kundi lililokuwa likiungwa mkono na serikali.
Baadaye aliruhusiwa kurudi nyumbani - lakini chini ya masharti ya kifungo cha nyumbani.
Wakati mwingine alifanikiwa kukutana na maafisa wa chama chake cha NLD na baadhi ya wajumbe , lakini katika miaka ya awali hakuruhusiwa kukutana na watoto wake wawili au mume wake ambaye alifariki kutokana na saratani Machi 1999.
Mamlaka ya jeshi ilijitolea kumruhusu kwenda Uingereza kumuona wakati alipokuwa mgonjwa kupitia kiasi, lakini alikataa akihofia kwamba hatoruhusiwa kurudi katika taifa hilo.