Alison Carey: Mariah Carey ashitakiwa na dada yake kwa kuandika kitabu 'kinachomdhalilisha'

Chanzo cha picha, Getty Images
Dadake Mariah Carey anamshtaki gwiji huyo wa muziki nchini Marekani kumlipa $1.2m (£875,000) kwa kumsababishia 'dhiki ya kihisia' anayodai kutokana na matamshi aliotoa ndani ya kumbukizi yake .
Katika kitabu hicho , msanii huyo alitoa madai kuhusu tabia ya dadake mkubwa Alison , ikiwemo kwamba alimuweka Mariah katika hatari ya kutumiwa vibaya. Wakati alipokuwa na umri wa miaka 12.
Alison anakana madai hayo akisema kwamba Mariah hakutoa ushahidi wowote kuthibitisha madai hayo makali.
Anasema kwamba madai hayo yalilenga kumdhalilisha na kumuaibisha yeye.
Kwasasa anawasilisha kesi mahakamani ili kulipwa fidia kwa kuharibiwa sifa kama mtu asiye na moyo mzuri, kumuonesha unyonge, kumlipiza kisasi na kumdharau hadharani.
Kumbukizi hiyo kwa jina Maana ya Mariah Carey{ Meaning of Mariah Carey ilichapishwa mwezi Septemba.
Malalamishi ya Alison yaliopo katika kurasa mbili yaliwasilishwa katika mahakama ya juu ya New York siku ya Jumatatu.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ndani yake Alison alimtuhumu Mariah Carey kwa kutumia haiba yake kama mtu maarufu kumshambulia dada yake anayedai kuwa masikini, kwa lengo la kuvutia vichwa vikuu vya habari ili kuweza kukuza kitabu chake.
Pia anasema kwamba anakabiliwa na msongo wa mawazo kutokana na kiwewe alichopitia utotoni ambapo watoto wake walimtelekeza.
Katika kitabu hicho , Mariah anamuelezea dada yake kama mtu aliyeathiriwa sana.












