Biden asaini agizo kubadili sera ya familia za wahamiaji kutenganishwa na watoto wao

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Marekani Joe Biden amesaini maagizo matatu ya rais ya kuunganisha familia za wahamiaji zilizotenganishwa kutokana na sera ya utawala wa Trump na pia anataka kupitia tena ajenda yote ya uhamiaji kwa ukubwa zaidi.
Katika jaribio lake la kuzuia uhamiaji haramu, utawala wa Rais Donald Trump ulitenganisha watu wazima ambao hawakuwa na stakabadhi sahihi za uhamisho halali na watoto wao wakati wanavuka mpaka wa Marekani na Mexico.
Maagizo ya Bwana Biden yataanza kwa kuanzisha jopo kujaribu kuunganisha watoto wanaokadiriwa kuwa kati ya 600 na 700 ambao bado wametengana na familia zao.
Utawala wa Trump ulitenganisha watoto karibu 5,500 na wazazi wao ama waangalizi wao katika mpaka huo mwaka 2017-2018.
Utawala wa Rais Barack Obama - ambao Bwana Biden alikuwa makamu rais - pia ulitenganisha watoto na wazazi wao ambao hawakuwa na stakabadhi halali za kuishi Marekani, ingawa hilo lilikuwa nadra sana kutokea, kulingana na wanaharakati.
Moja ya maagizo ya Biden ni kuunda jopo litakaloongozwa na waziri mpya wa mambo ya ndani aliyeidhinishwa Alejandro Mayorkas - kufuatilia shughuli nzima ya watoto kuunganishwa tena na familia zao.
Maagizo ya pili na tatu ya Bwana Biden ambayo yaliwekwa saini Jumanne, yanaagiza kupitiwa tena kwa sera ya uhamiaji ya Bwana Trump ambayo ilikatisha utoaji wa hifadhi, ikapunguza shughuli za wahamiaji halali kuingia Marekani na kufuta ufadhili wa nchi za kigeni.
Akizungumza akiwa Ikuli, Bwana Biden amesema: "Tutafanyia kazi kufuta yaliyotekelezwa na utawala uliotangulia ambayo yanaenda kinyume na maadili na aibu kwa taifa, yaani kutenganisha watoto wakiwa mikononi mwa familia zao, mama na baba zao, mpakani bila mpangilio wowote wa kuunganisha watoto ambao bado wapo kizuizini na wazazi wao."
Bwana Biden pia amependekeza sheria ya kutoa hadhi ya makazi halali itakayotoa mwelekeo wa kupata makazi ya kudumu kwa raia wote takriban milioni 11 ambao hawana vyeti halali vya makazi.
Lakini wachanganuzi wanasema kuwa hadi kufikia sasa rais mpya amekwepa kubadilisha sera zenye msimamo mkali zilizotekelezwa na Trump ili kuzuia kuongezeka kwa uhamiaji haramu katika mpaka wa eneo la kusini.

Msichana mhamiaji aliyekamatwa na Marekani kwa siku zaidi ya 531
Na Patricia Sulbarán Lovera, wa BBC Mundo
Luisa, 9, kutoka El Salvador, sasa hivi ni mtoto mhamiaji ambaye amekuwa akizuiliwa kwa muda mrefu zaidi, kwa mujibu wa mashirika yanayotoa msaada wa kisheria.
Luisa wakati mwingine anasikika kuwa mwenye busara zaidi hata kuliko umri wake. Amekuwa akiandika barua kwa wanasheria, na kuomba mamlaka kumuachilia huru yeye na Ariana, mama yake kutoka kituo cha kuzuia wahamiaji cha Marekani huko Dilley, Texas.
Luisa amechoka na hali yake ya sasa. "Nimekuwa hapa kwa sikukuu mbili za krismasi," anasema. "Natamani sana kupika. Natamani sana kujipikia chakula changu. Nimejifunza Kiingereza kidogo. Lakini nataka kujifunza mengi nikiwa shuleni wala sio hapa."
Mama yake, Ariana, anasema msichana huyo hapendi chakula anachopewa katika kituo walichozuiliwa na kwamba kadiri muda unavyozidi kusonga, tabia yake pia imebadilika. "Anakula matunda pekee na wakati mwingine hali kabisa," anasema.
Ariana, 31, yeye mwenyewe amepata matatizo kwa sababu ya wasiwasi mwingi.
"Natumia dawa na kuna wakati ambao nilipatwa na mshutuko wa moyo. Sikujua ni nini. Madaktari waliniambia kwamba chanzo chake ni kuwa na wasiwasi kupita kiasi.
"Kuna wakati huwa nahisi kama sio mimi niliye humu ndani."

Wanaharakati wataka Biden kuchukua hatua madhubuti zaidi
Na Angélica M Casas, wa BBC News
Wakati Rais Biden anaanza kufuta sera za utawala wa Trump juu ya uhamiaji kupitia maagizo kadhaa ya rais, bado baadhi ya wanaharakati wa kutetea wahamiaji wanaona wakati wa kusherehekea haujafika.
"Matarajio ni kwamba utawala huu utachukua hatua madhubuti zaidi, maamuzi thabiti na ya kijasiri kwa kubadilisha sera za mtangulizi wake haraka iwezekanavyo,"amesema Alejandra Gomez, mkurugenzi mwenza mtendaji wa shirika moja ililopo Arizona amesema:
"Ni hatua muhimu ya kwanza. Lakini wakati kuna umuhimu wa kupitia tena sera ya uhamiaji ya Trump, pia kuna ulazima wa kuchukuliwa kwa hatua madhubuti. Hiyo ndio sababu baadhi yetu ambao tunaruhusiwa kupiga kura tulimchagua."
Hadi kufikia sasa, hakuna agizo la Biden ambalo limebadili moja kwa moja sera za uhamiaji za Trump.
"Jamii yetu ya wahamiaji, imepitia mateso mengi sana katika kipindi cha miaka minne," amesema Gomez.
Anasema, Bwana Biden anajua jamii ya wahamiaji inataka nini.


Hatua ya kutenganisha watoto na wazazi wao ilifikiwa vipi?
Chini ya sera ya uhamiaji ya "kutovumilia tena" ambayo ilipitishwa Aprili 2018, watu wazima ambao hawakuwa na vyeti halali vya uhamiaji waliokuwa wanavuka mpaka wa Marekani na Mexico walishtakiwa kwa kosa la uhalifu na kufungwa jela.
Makosa hayo awali yalikuwa yanachukuliwa kama ukiukaji wa sheria.
Kwasababu watoto wa wahamiaji walioshitakiwa haikuwezekana pia nao kushitakiwa kwa makosa ya uhalifu, hawakuruhisiwa kufungwa jela na wazazi wao na kusababisha watoto hao kuwekwa katika makazi ya muda au vituo vya kuwatunza watoto.
Picha na video za watoto wakiwa wamelala kwenye mikeka katika vituo walivyozuiliwa ambavyo vilikuwa na msongamano wa watoto zilisababisha hasira miongoni mwa wananchi na kufanya Bwana Trump kusitisha hatua hiyo mnamo mwezi Juni.
Wiki iliyopita, Wizara ya sheria chini ya Bwana Biden ilifuta sera hiyo.
Hata hivyo, katika baadhi ya vituo ambako baadhi ya watoto walikuwa wanazuiliwa wakati wa utawala wa Rais Obama, watoto takriban 60,000 ambao hawakuwa na wazazi wao walizuiliwa katika mpaka wa kusini na kufungwa kwenye magereza hayo mwaka 2014 pekee.
Maafisa wa enzi ya Obama wamesema kutenganishwa kwa familia za wahamiaji ilikuwa nadra sana kutokea kwa mfano, katika matukio ambayo kulikuwa na sababu ya kushukiwa kuwa kuna usafirishaji haramu wa watoto ingawa idadi kamili haijulikani.












