Virusi vya Corona: Uingereza yapiga marufuku abiria kutoka Tanzania, DRC

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 2

Serikali ya Uingereza imepiga marufuku abiria kutoka Tanzania na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuzuia maambukizi ya aina mpya ya virusi vya corona.

"Ili kusaidia kuzuia kuenea kwa aina ya COVID-19 iliyogundulika Afrika Kusini, tunapiga marufuku abiria wote wanaoingia kutoka Tanzania na DRC kuanzia saa 10 alfajiri kesho (Ijumaa)," ameandika Bw Grant Shapps, waziri wa uchukuzi nchini Uingereza kupitia mtandao wake wa Twitter Alhamisi usiku.

Zuio hilo linaanza kwa wasafiri wote waliotoka ama kupita nchini Tanzania na DRC ndani ya siku 10 zilizopita. Hata hivyo, raia wa Uingereza na Ireland na raia kutoka mataifa mengine ambao wenye vibali vya ukaazi wataruhusiwa kuingia ila watatakiwa kujitenga nyumbani pamoja na familia zao kwa siku 10 baada ya kuwasili.

Tanzana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zimeongezwa kwenye orodha ya Uingereza ya nchi zilizopigiwa marufuku ya wasafiri wake kuingia nchini humo kama hatua za kudhibiti maambukizo ya aina mpya ya virusi vya Corona vilivyogunduliwa nchini Afrika kusini.

Awali mwezi huu mataifa mengine 11 ya Afrika yalipigwa marufuku kama hiyo. Mataifa hayo ni; Namibia, Zimbabwe, Botswana, Eswatini, Zambia, Malawi, Lesotho, Msumbiji na Angola - visiwa vya Ushelisheli na Mauritius.

Uingereza ilipiga marufuku abiria kutoka Afrika Kusini Desemba 24.

Uingereza ni miongoni mwa mataifa ambayo yanakabiliana na janga la virusi vya corona kwa kiwango kikubwa na uchumi wake ukiwa umeyumba kutokana na wimbi la kwanza la virusi mambukizi ya corona.

Wakati mataifa mengine yakipambana na janga hili Rais wa Tanzania John Magufuli alisema mwezi Juni mwaka jana kuwa taifa lake 'lipo huru na maambukizi ya virusi vya corona' kutokana na maombi ya wananchi.

Hata hivyo Shirika la Afya duniani (WHO) lilieleza wasiwasi wake juu ya hatua zinazochukuliwa na taifa hilo dhidi ya kukabiliana na Covid-19.

Serikali ya Tanzania imeondoa sharti wageni wanaoingia nchini humo kukaa karantini kwa muda wa siku 14, hata hivyo wanaowasili wote wanapimwa joto na endapo wataonesha dalili za COVID-19 ndio watahitajika kujitenga kwa muda wa siku 14.

Serikali za Tanzania na DRC bado hazijazungumzia hatua hiyo ya Uingereza.