Msafara wa wahamiaji waliokuwa wakielekea Marekani wazuiwa na maafisa wa Guatemala

Iliyochapishwa

Msafara wa wahamiaji kutoka Amerika Kusini uliokuwa ukielekea nchini Marekani umekutana na marungu na gesi za kutoa machozi nchini Guatemala, ambapo vikosi vya usalma vilifunga njia yao ya kupita kuelekea Marekani.

Maelfu ya watu walizuiwa kwenye barabara karibu na mpaka wa Guatemala na Honduras. Serikali imesema haingekubali "matembezi ya umati wa watu kinyume cha sheria ".

Wahamiaji wanaokadiriwa kuwa 7,000 , wengi wao kutoka Honduras, wameingia katika siku za hivi karibuni, wakikimbia umasikini na ghasia.

Wanatumaini kusafiri hadi Mexico, na baadaye kuufikia mpaka wa Marekani.

Kila mwaka, maelfu ya wahamiaji wa Amerika ya kati hujaribu safari hii ili kujaribu kufika Marekani, mara nyingi hutemea kwa miguu.

Rais mteule wa Marekani Joe Biden, kutoka chama cha Democrat, ameapa kuondoa sera kali za uhamiaji zilizowekwa na mtangulizi wake, Donald Trump, kutoka Republican.

Lakini utawala wa Bw Biden ,ambao utachukua mamlaka Jumatano, umewaonya wahamiaji kutofanya safari , kwa sababu sera za uhamiaji hazitabadilishwa mara haraka.

Nini kilichotokea wakati msafara wa wahamiaji ulipoingia Guatemala?

Wakati wahamaiaji walipokuwa wakivuka mpaka wa Guatemala kuelekea kwenye mpaka wake na Mexico, waliozingirwa na vikosi vya usalama karibu na kijiji cha Vado Hondo kilichopo kusini -mashariki.

Kikundi cha wanajeshi na maafisa wa polisi walifunga barabara , na kuwazuia wengi wao kuendelea na safari. Baadhi ya wahamiaji hao bado walilazimisha kwa nguvu kupita, na kuwafanya maafisa wa usalama kuwasukuma nyuma.

Video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, inaonesha vikosi vya Guatemala vikitumia gesi za kutoa machozi, vifaa vya kujikinga na marungu kuwarudisha nyuma wahamiaji. Watu kadhaa walijeruhiwa katika tukio hilo.

Wahamiaji wengi walirudi nyuma na kuweka kambi, huku baadhi wakisubiri karibu na mpaka ili kujaribu tena bahati yao ya safari ya kuelekea nchini Marekani baadaye . Wengine walitorokea kwenye milima iliyopo karibu na kujificha huko.

"Kwa bahati nzuri, vikozi vyetu vya usalama viliweza kudhibiti vita hivi ," Guillermo Díaz, mkuu wa shirika la uhamiaji la Guatemala , aliliambia gazeti la New York Times "Tuliweza kutuliza kila kitu katika hali tatanishi."

Taarifa kutoka ofisi ya rais wa Guatemala zinasema kuwa : "ujumbe wa Guatemala ni wa wazi: Haina ya matembezi ya wahamiaji haramu wanaosafiri kwa makundi ya watu wengi hayatakubalika, hii ndio maana tunashirikiana kwa pamoja na mataifa jirani kutatua tatizo hili kama suala la kikanda ."

Ni kwanini kuna idadi kubwa ya watu wanaokuja sasa?

Wahamiaji wanasema mateso, ghasia na umasikini ndio hali halisi ya maisha wanayoishi kila siku katika mataifa yao. Hali imekuwa mbaya hata zaidi kutokana na vimbunga vikubwa ambavyo viliyapinga maeneo ya Amerika ya kati mwezi Novemba mwaka jana.

Kwahiyo, katika kutafuta maisha bora, wanataka kufika Marekani kwa matumaini ya kupata kazi na usalama.

Dania Hinestrosa, mwenye umri wa miaka 23 ambaye anasafiri na binti yake, aliliambia shirika la habari la AFP: "hatuna kazi, hakuna chakula, Kwahiyo niliamua kwenda Marekani ."

Ahadi ya sera mpya za uhamiaji chini ya utawala wa Biden pia inadhaniwa kuwachochea baadhi ya wahamiaji kufanya jaribio la kuufikia mpaka wa Marekani.

Utawala wa Marekani unaoingia madarakani unasema nini?

Maafisa wa Bw Biden wamekwisha waonya wahamiaji wa America ya Kati wasifanye safari za hatari kuelekea kwenye mpaka wa Marekani.

Akizungumza na shirika la habari la NBC afisa wa Bw Biden ambaye jina lake halikutajwa alisema wahamiaji wanaojaribu kudai ukimbizi nchini Marekani "wanahitaji kuelewa kuwa hawataweza kuja Marekani mara moja ".

Utawala wa Biden utawapa kipaumbele wahamiaji wasio na vibali ambao tayari wanaishi nchini Marekani, sio wale wanaoelekea nchini humo kwa sasa, afisa huyo alisema.

"Uwezo wa mchakato kwenye mpaka sio kama mwangaza kiasi kwamba unaweza kuuwasha na kuuzima ," Susan Rice, mmoja wa washauri wa Bw Biden wa sera. Aliliambia shirika moja la habari za kihispania- Efe mwezi Disemba.

"Wanaomba uhamiaji na ukimbizi wanapaswa kutoamini kabisa wale wanaowaambia kuwa mipaka itafunguliwa ghafla kushugulikia kila mtu kuanzia siku ya kwanza. Haitakuwa hivyo ."

Mark Morgan, naibu kamishna wa forodha na ulinzi wa mpaka ,wiki iliyopita aliwaambia wale watakaokua wahamiaji kwenye mpaka wa kusini mwa Marekani "usipoteze muda na pesa zako ".

Wajibu wa Marekani wa "utawala wa sheria na afya ya umma" hautaathiriwa na mabadiliko ya utawala, alisema katika taarifa.

Misafara ya makumi kadhaa, baadhi ikiwa ya maelfu ya watu wameondoka kutoka Amerika ya kati katika miaka ya hivi karibuni. Kundi kubwa zaidi lilitoka Hondurus mwezi Oktoba mwaka 2018, na kumfanya rais Trump kusema "ani uvamizi".

Lakini wote wamempinga Bw Trump, ambaye aliziwekea shinikizo nchi za Mexico, Guatemala, Honduras na El Salvador kwa kuwakamata wa wahamiaji haramu kaskazini mwa nchi.