Jimbo la Magharibi la Darfur: Mapigano yasababisha vifo vya watu 48

Iliyochapishwa

Ghasia kati ya makundi ya kikabila katika jimbo la Magharibi mwa Darfur zimesababisha mauaji ya watu 48, kulingana na chombo cha habari cha Sudan kikinukuu muungano wa madaktari.

Mapigano katika mji mkuu wa jimbo hilo , Elgeneina , yalianza siku ya Jumamosi baada ya mzozo ambapo mtu mmoja alidungwa kisu hadi kufa.

Masharti ya kutotoka nje yamewekwa na waziri mkuu Abdalla Hamdok ametuma ujumbe kuchunguza.

Mzozo wa Darfur ulioanza mwaka 2003 ulipelekea mamlioni ya watu kutoroka eneo hilo na licha ya makubaliano ya amani kuna hali ya taharuki.

Ghasia za Jumamosi zinajiri chini ya wiki , baada ya walinda amani kutoka Umoja wa Mataifa na vikosi vya Umoja wa Afrika kutoa usalama kwa serikali ya Khartoum baada ya kuhudumu kwa takriban miaka 13, kulingana na mwandishi wa BBC Youssef Taha.

Ghasia kama hizo katika eneo la El Geneina mwaka uliopita , ambazo zilisababisha vita kati ya wafugaji wa Kiarabu na wale wasio Waarabu zilisababisha mauaji ya zaidi ya watu 100.

Mapigano ya hivi karibuni , ambayo yalisababisha watu 100 kujeruhiwa yalitokea katika kambi moja ya watu ambao walikuwa wamewachwa bila makao kufuatia mzozo huo wa Darfur.

Mgogoro mbaya zaidi kati ya wanaume wawili uligeuka na kuwa mapigano makali kati ya wapiganaji waliojihami, kilisema chombo cha habari AFP .

Makubaliano ya amani yaliohusisha makundi karibia yote katika eneo la Darfur yalitiwa saini mwaka uliopita.

Mzozo huo wa Darfur ulianza chini ya utawala wa rais Omar al- Bashir ambaye alipinduliwa 2019 na anasakwa na mahakama ya kimataifa ya ICC kwa madai ya kutekeleza uhalifu wa kivita katika eneo hilo.

Haki kwa watu wa Darfur ndio kilichokuwa kilio cha makundi ya kiraia yaliounga mkono kuondolewa madarakani kwa rais huyo baada ya kutawala kwa takriban miongoni mitatu.

Muungano wa wataalamu nchini Sudan ambao ulikuwa mbele katika vuguvu dhidi ya rais Bashir , ulitoa wito kwa serikali ya mpito iliopo kukabiliana na makundi hayo yaliojihami ambayo yamekuwa yakitembea na kuwatesa raia tangu kuanguka kwa utawala uliopita , kilisema chombo cha habari cha Sudan.