Tangazo la mtu anayekula Sandwichi ya popo lachunguzwa kufuatia hisia Australia

Iliyochapishwa

Tangazo moja linalomuonesha mtu mmoja akiwa anakula popo aliyewekwa ndani ya Sandwichi linachunguzwa na bodi ya matangazo nchini Australia.

Tangazo hilo kutoka kwa kampuni ya matangazo ya Boating Camping Fishing Store BCFS limetazamwa zaidi ya mara 250,000 katika mtandao wa Youtube.

Katika tangazo hilo mtu mmoja anafanya mzaha kwamba mlipuko wa virusi vya corona ulisababishwa na mtu aliyekuwa akila popo.

Huku maradhi ya kwanza yakidaiwa kutoka katika soko la wanyama mjini Wuhan, China hakujakuwa na thibitisho la moja kwa moja kwamba ndio chanzo cha virusi hivyo na kusambaa kwake.

Kampuni hiyo ya tangazo imepokea malalamishi kadhaa kuhusu tangazo hilo la majira ya joto na iko katika harakati ya kuangazia malalamishi hayo ili kuona iwapo tangazo hilo linakera , alisema msemaji wa kampuni hiyo ya matangazo akizungumza na BBC.

Msemaji wa BCF awali alikua ameaviambia vyombo vya habari vya Australia kwamba tangazo lake linatambua kwamba raia wengi wa Australia watasalia majumbani mwao msimu huu wa joto na akawataka kutembelea maeneo yao ya nyumbani.

''Ni kweli kwamba tunaelewa athari za mlipuko huu na kusambaa kwake , lakini ni wazi kwamba tangazo hili limeundwa kuwa na malengo kama hayo''.

BCF sio mgeni kwa bodi ya kudhibiti matangazo nchini Australia ikiwa miongoni mwa kampuni zenye matangazo yaliowakera wengi katika mwaka 2016 na 2018.

Katika kipindi cha miaka iliopita BCF imeanzisha utamaduni wa kampeni za kukera kwa lengo la kufurahisha , smemaji aliongezea. Tutakuwa na wakosoaji na tunaheshimu hilo.