Ajali ya Treni: Watu 66 wajeruhiwa katika ajali ya treni Tanzania

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 1

Shirika la Reli Tanzania (TRC) limethibitisha kutokea kwa ajali iliyohusisha treni ya abiria iliyokuwa safarini kutoka jijini Dar Es Salaam ikielekea maeneo ya Tabora, Katavi (Mpanda), Kigoma na Mwanza ikiwa na abiria 720 siku ya Jumamosi.

Kufikia sasa watu watatu wamethibitishwa kufariki dunia miongoni mwao mtoto mmoja na wengine 66 wakijeruhiwa.

''Treni hii iliwasili Dodoma majira ya saa 9:15 alasiri na Kuondoka Dodoma majira ya Saa 11:40 Jioni. Treni hii iliwasili katika kituo cha Kigwe majira ya saa 12:25 Jioni na Kuondoka saa 12:27 Jioni.'' Ilisema taarifa ya TRC iliyotolewa kwa umma.

Shirika la Reli Tanzania halikutoa maelezo yoyote kuhusu chanzo cha ajali hiyo lakini limesema: ''uchunguzi unaendelea kufanyika na shirika litaendelea kutoa taarifa''.

Abiria waliojeruhiwa wameondolewa katika eneo la tukio na wamekuwa wakipokea matibabu katika hospitali ya mkoa jijini Dodoma.

Makamu wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan,amefika katika hospitali hiyo kuwapa pole waliojeruhiwa.