Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
WHO yaonya hatari ya kuwa na kisonono sugu kwasababu ya corona
Wataalamu wa afya wa Shirika la Afya Duniani (WHO), wameonya kuwa huenda kukatokea ugonjwa sugu wa kisonono kwasababu ya utumiaji mbaya wa vijiuasumu au dawa za kuzuia na kuua bakteria kipindi hiki cha corona.
Kulingana na wataalamu, ugonjwa wa zinaa wa kisonono umepata mazingira yanayochangia uwe sugu kwasababu dunia nzima inaendelea kutumia nguvu nyingi kuhakikisha inakabiliana na virusi vya corona.
Kuna zaidi ya visa milioni 90 vya ugonjwa wa kisonono kila mwaka kote duniani na idadi hiyo inaongezeka kwa asilimia 17, kulingana na ripoti ya WHO.
Kisonono sugu kinaweza kusababisha maambukizi ya virusi vya ukimwi kuongezeka mara tano pamoja na maambukizi ya macho ambayo huenda yakasababisha upofu.
Ingawa WHO inasema visa vingi vya maambukizi ya ugonjwa wa zinaa wa kisonono ni Afrika, nchi za magharibi pia nazo zinashuhudia ongezeko la ugonjwa huo.
Idadi kubwa ya watu wenye ugonjwa huo wa zinaa imebainika hospitalini kote duniani kwasababu ya matumizi mabaya ya dawa za kukabiliana na bakteria zinazotumika kupambana na ugonjwa wa corona.
Msemaji wa WHO alizungumza na gazeti la Sun Online kuhusu vile hatua hiyo na ukosefu wa huduma kwa magonjwa ya zinaa wakati huu wa janga la corona huenda kukachochea kuongezeka kwa kisonono sugu.
Msemaji huyo wa WHO alisema: "Matumizi mabaya ya dawa za kuua bakteria kunaweza kufanya ugonjwa wa kisonono kuwa sugu kutibika. Mfano, Azithromycin - dawa ya kawaida ya kutibu maambukizi ya mfumo wa kupumua - ilitumika kama dawa ya kutibu corona mwanzoni wa janga hili''.
"Wakati wa janga la corona, kupata tiba kwa ajili ya magonjwa ya zinaa pia iimekuwa tatizo. Hii inamaanisha kuwa visa vingi vya magonjwa ya zinaa havipati matibabu inavyostahili na hivyo basi watu wengi wanajitibu wenyewe''.
Aidha, msaidizi wa WHO katika kitengo cha uchunguzi wa dawa za kuua viini, Dkt. Hanan Balkhy, ameonya dhidi ya utumiaji mbaya wa dawa za kuua bakteria kiholela, kwa lengo la kukabiliana na virusi vya corona.