Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je ni faili gani za Mohammed bin Salman zinazosubiriwa na Joe Biden na kwanini?
Ripoti ya Gazeti la ''Washington Post'' ambayo inaashiria kwamba utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump ulikuwa unatafakari uwezekano wa kutoa kinga ya kisheria kwa Mwanamfalme Muhammad Bin Salman asifunguliwe mashtaka, imezua mjadala kuhusu masuala tata yanayomzunguka mwanamfalme wa Saudia, na jinsi utawala mpya wa Joe Biden unaongia madarakani utakavyoshughulikia masuala hayo ikizingatiwa kwamba unatofautiana wa mtangulizi , Donald Trump.
Kulingana na BBCArabic, ombi la kinga ya kisheria, kwa mujibu wa Washington Post, ni la kesi dhidi ya Salman, iliowasilishwa mahakamani na afisa wa zamani wa intelijensia wa Saudia Saad al-Jabri, mtoro aliye uhamishoni nchini Canada.
Gazeti hilo limenukuu katika taarifa yake likisema vyanzo vya habari ambavyo vimeomba visitajwe , vinasema Idara ya mambo ya nje ya Marekani ilituma ombi kwa wakili wa Saad Al-Jabri, kutaka ufafanuzi wa kisheria ikiwa inaweza kuitikia ombi la Saudi Arabia la kumpatia msamaha Muhammad bin Salman, wakati mahakama ya Marekani inataka kuanzisha kesi ya Al-Jabri dhidi ya bin Salman.
Idara ya Haki katika wizara ya mambo ya nje ya Marekani inashauriana na pande husika, ili kufikia uamuzi wa pamoja na wizara ya haki mahakamani.
Endapo ombi la ulinzi wa kisheria litaidhinishwa huenda jina la Mohammed bin Salman likaondolewa katika orodha ya washtakiwa katika kesi nyingine yoyote itakayowasilishwa mahakamani dhidi yake nchini Marekani, kando na kesi ya mauaji ya mwandishi wa Saudi Arabia na mwanahabari Jamal Khashoggi.
Kwa mujibu wa wachambuzi, ombi la Saudi Arabia linaashiria hofu ya Bin Salman na utawala wake dhidi ya utawala mpya unaoingia madarakani nchini Marekani unaoongozwa na Joe Biden ikizingatiwa faili kadhaa ambazo hazijashughulikiwa kumhusu Mwanamfalme wa Saudi, ikiwa ni pamoja na vita vya Yemen na kesi ya mauaji ya Khashoggi.
Hali ya haki za binadamu nchini Saudi Arabia, zinaashiria kipindi kigumu kinaikodolea macho utawala wa Saudi Arabia, hususan ikizingatiwa kile kilichoandikwa katika "Washington Post"kwamba Biden aliwahi kusema anatafakari kutathmini upya uhusiano wa Washington na Riyadh.
Vita vya Yemen
Vita vya Yemen vimetajwa katika vituo kadhaa vya habari vya Magharibi na katika ripoti za mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu kama janga kubwa katika historia ya mwanadamu.
Rais Mteule wa Marekani Joe Biden, anaonekana kupinga sera za Bin Salman hasa kuhusiana na vita vya Yemen, na kampeni yake, wakati alipoteuliwa rasmi kuwa mgombea urais wa chama Democratic, alisema endapo atashinda uchaguzi, "tutatathmini upya uhusiano wetu na Saudi Arabia, na kukomesha msaada wa kuunga mkono harakati za nchi hiyo katika vita vya Yemen".
Ijapokuwa kesi ya mauaji ya mwandishi wa Saudia na mwanahabari Jamal Khashoggi katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia nchini Uturuki, mnamo Oktoba 2, 2018, ilitikisa mtazamo wa watu duniani kuhusu nchi hiyo ya Uarabuni, utawala wa Trump, kulingana na baadhi ya wachambuzi, haukuwa tayari kutoa taarifa iliyokuwa nayo kuhusu nchi ni nani aliyehusika na mauaji hayo licha ya tuhuma kwamba maafisa wa karibu wa bin Salman walidaiwa kumuua mwandishi wa Saudia ambaye alikuwa akiishi nchini Marekani.
Katika taarifa ya mwaka 2018, Trump alisema kwamba Mohammed bin Salman huenda alihusika moja kwa moja na mauaji hayo, lakini makundi ya kutetea haki za binadamu yalimkosoa kwa kutokuwa muwazi kuwataja waliomuua Khashoggi, ili kulinda mkataba wa silaha wa nchi hiyo na Saudi Arabia.
Mtazamo wa Biden unaonekana kutofautiana kabisa na ule wa Trump kuhusu kesi ya Khashoggi, na mara kadhaa ameelezea haja ya kuhakikisha haki inatekelezwa kuhusiana na kesi hiyo.
Mwezi Oktoba mwaka huu, Biden ambaye alikuwa mgombea urais wa Democratic, alisema katika taarifa iliyochapishwa katika tovuti yake rasmi kwamba:
"Miaka miwili iliyopita, maajenti wa Saudia, walitekeleza agizo la Mwanamfalme, Mohammed bin Salman, la kuuawa kwa mwanahabari wa Saudia aliyekuwa akiishi Marekani, Jamal Khashoggi.
Kuhusiana na Khashoggi, aliongeza kuwa, "Madai ambayo alilipia na maisha yake, ni kukosoa sera ya serikali katika nchi yake." Kuzingatia uhuru wa kujieleza haki ambayo ni ya kimataifa, "kama alivyokuwa akipenda kuelezea.
Kuwakamata wanaharakati
Katika ripoti yake iliyochapishwa hivi karibuni, mhariri wa BBC wa masuala ya usalama Frank Gardner, alisema kesi hiyo unaiweka uongozi wa Saudia katika hali ambayo inawalazimu kusafisha taswira ya nchi kimataifa.
Mamlaka ziliwakamata wanaharakati 13 waliokuwa wakiandamana kwa amani nchini Saudia, na baadhi yao kushambuliwa, kutokana na " kosa" la kutaka kupewa uhuru wa kuendesha magari na kukomesha mfumo wa wanaume kuwapa idhini wanawake ruhusa ya masuala muhimu kuwahusu - hali ambayo ilionekana kudhibiti uhuru wao.
Watu kadhaa walikamatwa mwaka 2018, miongoni mwao mfungwa maarufu Loujain Al-Hathloul, kabla ya marufuku ya wanawake kuendesha magari kuondolewa.
Maafisa wa Saudia walithibitisha kwamba Al-Hathloul alikuwa anatuhumiwa kwa kuchunguza masuala ya ndani na "kwa niaba ya nchi za kigeni," lakini hawakutoa ushahidi wa kuthibitisha madai hayo, huku marafiki zake wakisema, hakufanya kitu kingine isipokuwa kuhudhuria kongamano la kimataifa, kuhusu haki za binadamu na kutoa maombi ya kazi ya Umoja wa Mataifa.
Gardner pia aliongezea kusema, kutokana na kile kinachofanyika katika vita vya Yemen, uongozi wa Saudia umejiweka katika njia panda na sasa unatafuta njia ya kujiondoa kistaarabu katika mzozo huo.
Biden pia alikua amesema katika taarifa hiyo hiyo wakati alipokuwa mgombea wa urais kwamba ataunga mkono harakati zote za haki za kibinadamu na kuongezea kwamba Marekani itapatia kipaombele thamani ya demokrasia na haki za kibinadamu pamoja na washirika wake katika sekta ya usalama.
Na aliendelea kusema , ''nitatetehea haki za wanaharakati , na wapinzani wa kisiasa na waandishi kote duniani ili kusema wanachofikiria bila uwoga wa kushambuliwa na kuwajibishwa''.
Haya ndio baadhi ya masuala yanayomzunguka mwanamflame wa Saudia Mohammed bin Salman , ambayo anasubiri jinsi utawala mpya wa Marekani utakavyokabiliana nayo , na ijapokuwa wengi wanaamini kwamba utawala mpya wa Biden utachukua mwelekeo tofauti, Wengine wanaamini kwamba Biden hatahatarisha uhusiano wake na taifa hilo.
Badala ya kumpoteza mshirika mkuu wa kimkakati ambaye anaipatia pato kubwa Marekani , kupitia ununuzi wa Silaha na jinsi maafisa wa Saudia wanavyoelezea uhusiano kati ya Riyadh na Washington ni wa kimkakati ambao ni zaidi ya mtu binafsi anayeongoza mataifa hayo mawili.