Yemen: Mapacha waliozaliwa wakiwa wameunganika wako 'katika hali hatari'

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 1

Madaktari katika mji mkuu wa Yemen Sanaa, wametoa ombi la dharura la kuokoa maisha ya mapacha wawili waliozaliwa siku ya Jumatano wakiwa wameunganika.

Mkuu wa hospitali ya al-Sabeen ambako watoto hao wa kiume walizaliwa amesema wako katika "hali hatari" na wanahitaji upasuaji wa dharura ambao unaweza tu kufanyika nje ya nchi.

Uwanja wa ndege wa Sanaa ulifungwa kutokana na vita vya muda mrefu nchini Yemen, ambayo imeharibu kabisa miundo mfumo wa afya.

Kituo cha misaada cha Saudi Arabia kilicho na makao yake nchini humo kimesema kinatathmini ikiwa itaweza kusaidia

"Uchunguzi wa kimatibabu umeonesha kuwa mapacha hao wameunganika lakini kila mmoja ana moyo wake, lakini moyo wa mmoja wao uko katika hali ambayo sio hali ya kawaida," Mkurugenzi wa hospitali ya Al-Sabeen Majda al-Khatib aliambia shirika la habari la AFP.

Alisema hospitali hiyo haina vifaa muhimu vinavyohitajika kutoa taswira kamili ya hali yao "ni viungo gani vilivyounganika".

Ikijibu ombi hilo, Shirika la misaada la mfalme Salman liliandika katika Twitter yake: "#KSrelief inaelezea kujitolea kwake kusaidia hali ya watoto hao kuchunguzwa na wataalamu wa afua wa Saudi Arabia na kutathmini uwezekano wa kuwatenganisha [mapacha hao]."

Mji wa Sanaa kwa saa unashikiliwa na waasi wa Kihouthi, kwa miaka kadhaa wamekuwa wakipigana na wanajeshi wa muungano wanaoongozwa Saudi-Arabia.

Mwaka uliyopita, mapacha waliokuwa wameunganika walifariki nchini Yemen wiki mbili baada ya kuzaliwa .

Mapacha waliounganika

  • Huwa wanafanana kwasababu wameumbwa kutokana na yai moja
  • Ni nadra sana kupata mapacha walioungana, wanakadiriwa kuwa moja kati ya karibu mapacha 200,000 wanaozaliwa.
  • Mara nyingi huunganika sehemu ya kifua, tumbo au nyonga
  • Karibu asilimia 70% ya mapacha waliounganika ni wa kike
  • Kumekuwa na nadharia mbili kwanini wanaunganika:

Huenda mgawanyiko katika viinitete viwili hulifanyika baadaye kuliko kawaida, na mapacha wakagawanyika kidogo, au sehemu za viinitete vilivyobaji viliendelea kuwasiliana na sehemu hizo za mwili huungana kadri zinavyokua.