Matokeo ya uchaguzi Marekani 2020: Trump amebaki na mapingamizi gani kisheria?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Na Jake Horton
- Nafasi, BBC Reality Check
- Iliyochapishwa
Wajumbe kutoka kila jimbo walikutana tarehe 14 Desemba kumuidhinisha rasmi Joe Biden kama rais ajaye wa Marekani, lakini Rais Trump amesema mchakato wa kisheria "utaendelea kusonga mbele".
Hakuna chochote kinachozuia timu ya kisheria ya Bw Trump kufungua mashtaka zaidi, lakini wataalam wanasema nafasi ya kufanikiwa inazidi kuwa ndogo.
Kwa hivyo ni kesi gani za kisheria zinaweza kuathiri matokeo?

Mfululizo wa kushindwa hadi sasa huko Pennsylvania
Hapa ndipo Bwana Trump aliweka mapingamizi mengi, na ingawa Bwana Biden tayari amethibitishwa kuwa mshindi kwa zaidi ya kura 80,000, Rais hajaacha majaribio ya kubadili matokeo.
Timu ya wanasheria ya rais ilidai wapiga kura katika maeneo yanayotegemewa Democrats walipewa nafasi zaidi ya kurekebisha makosa kwenye kura zao za posta kuliko mahali pengine.
Wakati mwanzoni walipopoteza kesi hiyo, mawakili wake waliipeleka kwenye mahakama ya rufaa ya nchi hiyo. Ilikataliwa huko pia, huku jaji akisema: "Mashtaka ya ukiukaji haki ni makubwa. Lakini kuita uchaguzi kutokuwa na haki haufanyi hali kuwa hivyo. Mashtaka yanahitaji madai maalum na kisha uthibitisho. Hatuna hayo hapa."
Timu ya Bw Trump ilisema watapeleka kesi hiyo kwa Mahakama Kuu ya Marekani.
Inaonekana hakuna uwezekano kwamba mahakama itasikiliza rufaa yoyote kama hiyo, na wataalam wa sheria wanasema hata ikiwa ingefanya hivyo, kesi hiyo ingekuwa na nafasi ndogo ya kufanikiwa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika kesi hiyo hiyo, timu ya rais pia ilidai kwamba zaidi ya kura 680,000 za posta zilihesabiwa bila uangalizi mzuri kutoka kwa waangalizi wa kura.
Hii ilifuata mvutano wa kisheria juu ya wapi waangalizi hawa waliruhusiwa kuwepo wakati wa kuhesabu - timu ya Trump ikisema kwamba waangalizi wa kura walizuiliwa kuona kile kinachoendelea.
Mahakama Kuu ya Pennsylvania mwishowe iliamua kwamba maafisa wa uchaguzi hawakuvunja sheria.
Mahakama huko Pennsylvania pia zilikataa madai kadhaa ya kisheria yaliyotolewa na kampeni ya Trump kuhusu kura za posta karibu 9,000 walisema hazina maelezo, kama vile tarehe ya kupiga kura au anuani ya mpiga kura.

Madai mengi yalitupiliwa mbali au kutatuliwa katika majimbo mengine
Mfululizo wa mashtaka huko Michigan, Wisconsin, Nevada, Georgia na Arizona hadi sasa yameshindwa kuzaa matunda.
Haya yote ni majimbo ambayo Bwana Biden amethibitishwa kuwa mshindi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kura za Wisconsin zilihesabiwa tena katika kaunti za Dane na Milwaukee, na Georgia ilikuwa na hesabu ya nchi nzima - zote zilithibitisha Bw Biden kuwa mshindi.
Kulikuwa pia na kesi iliyowasilishwa na jimbo la Texas, likiungwa mkono na Rais Trump, ambayo ilidai matokeo huko Georgia, Michigan, Pennsylvania na Wisconsin hayakuwa halali kwa sababu ya mabadiliko ya taratibu za kupiga kura kwa sababu ya janga la virusi vya corona.
Mahakama kuu Marekani imekataa kusikiliza madai hayo, ikisema Texas haikuwa na msingi wa kisheria wa kuwasilisha kesi hiyo.

Mapingamizi mengine yaliyofikishwa Mahakama Kuu?
Rais Trump amerejea kusema kwamba mapingamizi ya kisheria yanapaswa kusikilizwa na Mahakama Kuu ya Marekani, lakini alikubali kuwa hii inaweza kuwa ngumu.
Pamoja na mafanikio kidogo katika Mahakama za mwanzo, haijulikani ikiwa Mahakama Kuu ya Marekani ingekuwa tayari kusikia mapingamizi ya kisheria ya rais.
"Hakuna mchakato wa kawaida wa kupeleka mizozo ya uchaguzi katika Mahakama Kuu" anasema Prof Richard Briffault wa Shule ya sheria ya Chuo Kikuu cha Columbia.
Hadi sasa, uchaguzi wa mwaka 2000 ndio pekee ulioamuliwa na Mahakama Kuu ya Marekani.
Katika mwaka huo, Democrat Al Gore alipoteza jimbo la Florida - na uchaguzi wa rais - kwa kura 537 kati ya jumla ya karibu milioni sita waliopiga kura katika jimbo hilo.
Hii ilifuatiwa na mchakato wa kuhesabiwa tena wenye utata ambao ulidumu kwa zaidi ya mwezi mmoja - hadi Mahakama Kuu ilipoamua kuacha kuhesabu tena na kumpa ushindi George W. Bush wa Republican.












