Kala Jeremiah: Mtu yeyote mwenye nafasi ya kusikilizwa na kusikika ana fursa ya kuleta mabadiliko katika jamii yake

kala

Chanzo cha picha, Kala Jeremiah

    • Author, Esther Namuhisa
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Iliyochapishwa

Ni nadra sana kukuta mwanamuziki wa kizazi kipya kuimba nyimbo za maudhui tofauti na mapenzi.

Yawezekana ndio sababu mwanamuziki huyu Kala Jeremaiah ameonekana kuwa wa tofauti na hata kuwa miongoni mwa watu 16 waliotunukiwa tuzo ya mabingwa wa mabadiliko nchini Tanzania.

Katika sehemu ya maadhimisho yanayoendelea ya Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia nchini Tanzania, Wanawake katika Sheria na Maendeleo barani Afrika (WiLDAF) na Umoja wa Kupambana na Ukatili wa Kijinsia (MKUKI), kwa Ufadhii wa Shirika la Umoja Wa Matafa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) na Ubalozi wa Denmark nchini Tanzania, waliandaa hafla ya kusherehekea Mabingwa 16 wa Mabadiliko na miongoni mwao ni watu binafsi ambao wanafanya kazi nchini humo kila siku kutetea na kulinda haki za wanawake na wasichana kuwawezesha kuishi maisha bila ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.

Uteuzi wa mabingwa 16 uliotokana na mamia ya majina ni njia ambayo inatoa motisha ya kuleta mabadiliko ili kuondoa ukatili na unyanyasaji wa kijinsia na mila kandamizi nchini Tanzania.

Kwa upande wake Kala Jeremiah anadhani mabadiliko yanaanza na yeye kwasababu;

"Mtu yeyote mwenye nafasi ya kusikilizwa na kusikika ana fursa kubwa ya kuleta mabadiliko katika jamii yake," hayo ni maneno ya Kala Jeremiah ambaye ni mwanamuziki nchini Tanzania.

Jeremiah anasema sanaa yake inaambatana na kusaidia watu wengine.

"Huwa sifikiriii kuimba wimbo kama wimbo bali huwa nafikiria kutoa mafunzo, kumuinua yule aliyekata tamaa na kumpa burudani.

Kiria

Chanzo cha picha, Joyce Kiria

Kwa karma yangu naamini nimegusa maisha ya watu wengi.

Wimbo wa 'wanandoto' ambao unayahusu maisha ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu unatoa nafasi ya kumkumbusha msikilizaji wa wimbo yangu kuwa yule mtoto aliyeko barabarani hakufika pale kwa kupenda bali naye ana ndoto ya kuishi maisha mazuri.

Wimbo mwingine ambao Kala Jeremiah anajivunia maudhui yake ni wimbo wa 'kijana' anasema ametumia nafasi yake kama kijana ili kumuonesha na kumuelimisha kijana mwingine juu ya maisha na uwajibikaji.

Kala Jeremiah anasema ameamua kutoa huduma kupitia muziki wake hivyo hafanyi biashara katika muziki huo ili kuwapa fursa watu waweze kuelimika na kuburudika kupitia muziki.

"Muziki wangu sio biashara bali ni jukwaa la elimu bure," anasema Kala Jeremiah."

Joyce Kiria maarufu kama dada wa 'Wanawake Live'

Kwa zaidi ya miaka 10, anasema amekuwa katika harakati binafsi za kujitoa kwa ajili ya jamii yake.

"Kama mwathirika wa unyanyasaji wa kijinsia niliamua kuanzisha wanawake live kupaza sauti za wanawake kupigania haki zao.

Naamini kuwa Mabadiliko yanaanza na mimi , hivyo niliamua kujitoa maisha yangu ili kuleta mabadiliko.…kazi hii inanifanya nitoe utu wangu na heshima katika jamii."

Joyce

Chanzo cha picha, Joyce Kirya

Kupitia kipindi chake cha Wanawake live anasema anakuwa anajaribu kuibua matukio ya kijamii.

"Kwa kuonesha matukio ya ukatili ambayo yanatokea katika jamii mfano kama mume amemchoma mkewe kisu…. na kuna kesi nyingi za kutisha na kustaajabisha katika jamii zinaweza kuleta mafunzo katika jamii kabla ya madhara kutokea kwa upande wao"

Aidha ameeleza kuwa haijawa kazi rahisi kwake kwa kuwa amekutana na upinzani mkubwa kutoka kwa wanawake wenzangu.

Joyce alikuwa anafanya kazi za ndani yaani 'housegirl' lakini sasa ameamua kuanzisha kituo maalum kwa ajili ya kuwatetea katika ajira.

Janeth Mawinza

Janeth Mawinza

Chanzo cha picha, Janeth Mawinza

Yeye anatembea nyumba kwa nyumba kuibua unyanyasaji katika jamii inayomzunguka.

Katika kampeni ya nyumba kwa nyumba tunakutana na kesi ya ubakaji, ulawiti na kupigwa.

Mfano kuna unyanyasaji wa msichana kung'atwa meno na mwajiri wake kwa zaidi ya miezi mitatu mfululizo na kisa kingine cha msichana mwingine kuwa anachomwa na pasi na mwajiri wake.

"Nyumba yangu huwa ni hifadhi wahanga wa unyanyasaji na jeshi la polisi huwa msaada wangu wa karibu pamoja na serikali za mtaa.

Hali ngumu ya wasichana wengi ilimpa hamasa kuweza kusaidia wasichana hao wanaonyanyaswa,"anasema Janeth.

Janeth Mawinza

Chanzo cha picha, Janeth Mawinza

Rhobi Samweli

Rhobi anatokea maeneo ya Serengeti ana taasisi yake inayoitwa 'Hope For girls' inayokabiliana na ukatili wa kijinsia kama vile ukeketaji, ndoa za utotoni, uonevu kwa wajane na nyinginezo.

Kikubwa anachofanya Serengeti mkoani Mara , ni kutoa elimu kwa jamii dhidi ya ukatili wa kijinsia.

jul

Chanzo cha picha, Julian MARCUS

"Mbinu tunazozitumia kufanya majadiliano katika jamii ni Kuwa na road shows, kuonesha filamu na kuwahifadhi wasichana katika 'safe house' yaani nyumba salama."

Nyumba hizo salama zina uwezo wa kuhifadhi watu 55 lakini wako watu 107 kwa sasa.

Huo ni mipango wa jinsi ya kumtetea mhanga wa ubakaji, ndoa za utotoni, Ukeketaji.

Njia nyingine inayowasaidia ni kutumia Ramani au 'Mapping' kutafuta wahanga wa ukatili.

Katika nyingine ya ulinzi wa mama na mtoto ,kuna wamama 87 ambao tunawaita digital champion.

Wamama hao 87 wanapewa Smart phone kuwapa motisha na kusaidia kurahisisha kazi yao ya kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia vijijini.

Mpaka sasa Rhobi anasema wameweza kuokoa maisha ya wasichana zaidi ya 1000 dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia.

Selemani Kipunguni

Selemani Kipunguni

Chanzo cha picha, Suleman

Katika mwaka unaogawanyika na mbili kama huu 2020, huwa ndio msimu maalum wa ukeketaji .

Na kama mtoto alieenda kukeketwa akikutwa ameanza kufanya ngono , basi mzazi anapewa faini kwa kushindwa kutoa malezi bora.

Faini huwa ni ng'ombe na fedha.

Sulemani anasema sababu kubwa ya kufanyika kwa ukeketaji ni kuonesha thamani katika jamiii kwa kutaka kuolewa.

"Kama mwanaume natambua nafasi ya mwanamke kwa kiasi kikubwa sana.

Nilipokuwa mdogo mtu wa kwanza niliyemuamini alikuwa mama.

Hivyo hata kama changamoto wanazozipitia licha ya kuwa hazinifikii moja kwa moja ila ninajua madhara na ubaya wa unyanyasaji wa jinsia.

Jambo la ukeketaji linalofanyika katika jamii ninayoishi huwa linaonekana kuwa jambo la kawaida yaani kama shughuli nyingine yeyote.

Tangu mwaka 2010 ninaona wasichana wakikeketwa na tunaalikwa; tunakula na kunywa kama shughuli nyingine, sawa kabisa na kwenda harusini.

Faraja ya wengi huwa ni ndoa.

Hivyo mimi huwa natumia mbinu ya kuamsha mjadala miongoni mwao kuhusu jambo hilo na mwisho wa siku wanapata jibu wenyewe kuwa thamani ya ndoa si ukeketaji.

Harakati shirikishi inanisaidia kutatua matatizo yao kiurahisi bila kuvutana.

Wakati naanza harakati za kupinga ukeketaji maeneo ya kipunguni na kitunda jijini Dar es Salaam nilifanya utafiti halisia kwa kushiriki kwenye sherehe za ukeketaji ambapo watoto wa kike waliokeketwa hupitishwa barabarani wakitokea kwa ngariba wakishangiliwa na ndugu huku wakiwa wamevalishwa mavazi ya kiume .

Mtu asiyefahamu hawezi kugundua kwamba hao ni watoto wa kiume au wa kike."