Mpishi akiri kutekeleza makosa ya wizi wa medali na picha katika makazi ya Malkia

Iliyochapishwa

Mpishi msaidizi katika makao ya kifalme ya Buckingham amekiri kuwa aliiba medali na picha ndani ya makazi ya Malkia.

Adamo Canto, 37, alifikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi wa Westminster na kukiri kutekeleza makosa matatu ya wizi kati ya Novemba 11, 2019 na Agosti 7, 2020.

Polisi walipata bidhaa za kutosha tu alizoiba katika makazi yake, ndani ya jengo la Royal Mews eneo la makazi ya kifalme la Buckingham.

Kipindi cha janga la virusi vya corona, jukumu la Canto lilibadilishwa ikiwa zaidi linaegemea kufanya usafi ambako kulimwezesha kuingia ofisi nyingi zaidi pamoja na maeneo mengine ambayo katika hali ya kawaida hakuruhusiwa kuingia, mahakama iliarifiwa hivyo.

Baadhi ya bidhaa alizoiba thamani yake ni kati ya pauni 10,000 na pauni 100,000 zilizokuwa zimeorodheshwa kuuzwa katika mtandao wa manunuzi wa eBay, mwendesha mashtaka Simon Maughan amesema.

Jumla ya bidhaa 37 zilikuwa zinauzwa kwa thamani yake katika mtandao wa uuzaji bidhaa wa eBay, Bwana Maughan alisema huku Canto akitengeneza pauni 7,741.

Moja ya bidhaa zilizokuwa zinauzwa ni picha ya rais wa Marekani Donald Trump alipokuwa anahudhuria hafla ya serikali alipotembelea Uingereza iliyouzwa kwa pauni 1,500.

Canto pia alichukua picha iliyokuwa na sahihi rasmi za Mwanamfalme Harry na Mwanamfalme William na mke wake Kate.

Bidhaa 77 zilichukuliwa kutoka eneo la makazi ya mfalme huku vingine vikiibwa kutoka maeneo mbalimbali kama kwenye makabati ya wafanyakazi, chumba cha picha za Sanaa za Malkia na ukumbi wa sanaa wa Duke of York.

Canto pia alikubali kuiba medali ya tuzo ya heshima ya Bath ya msimamizi ya masuala ya nyumbani ambayo iliuzwa kwa pauni 350 mtandaoni.

Canto pia alikubali kuiba tuzo ya heshima kutoka kwa kabati la aliyekuwa afisa wa jeshi la Uingereza Meja Jenerali Richard Sykes, ambayo alituzwa na Malkia mwaka 2010.

Jaji Alexander Jacobs alimwachilia huru Canto kwa dhamana na kumuarifu kuwa anakabiliwa na hukumu ya kifungo gerezani wakati anasubiri hukumu.