Uchaguzi wa Marekani 2020: Mshirika wa Trump amtaka rais akiri kushindwa

Chanzo cha picha, Getty Images/AFP
Mshirika wa karibu wa Donald Trump amemsihi kuachana na jitihada zake za kuendelea kupinga matokeo ya uchaguzi dhidi ya mpinzani wake Joe Biden.
Aliyekuwa gavana wa New Jersey Chris Christie alikitaja kikosi cha sheria cha rais kama "aibu kwa taifa".
Rais Trump amekataa kukubali kushindwa katika uchaguzi wa Novemba 3, akidai kulikuwa na wizi wa kura bila kutoa ushahidi wowote.
Wafuasi wengi wa Repubublican wameunga mkono juhudi za Trump za kupinga matokeo ya uchaguzi ingawa idadi hiyo imekuwa ikipungua kadiri siku zinavyosonga mbele.
Jumamosi, Bwana Trump alipata pigo jingine katika jimbo la Pennsylvania, baada ya jaji kutupilia mbali kesi yake ya kupinga matokeo alikokuwa anataka mamilioni ya kura zilizopigwa kwa njia ya posta kufutwa.
Jaji Matthew Brann alisema madai yake hayana msingi na amekosa ushahidi wa kutosha kuthibiti madai hayo.
Uamuzi wa jimbo la Pennsylvania unamuwezesha Biden kuidhinishwa kama mshindi wa jimbo hilo Jumatatu. Biden ndiye rais mteule kupitia chama cha Democratic ambaye anaongoza kwa kura 80,000.
Bwana Biden anakadiriwa kumshinda Rais Trump kwa kura 306 dhidi ya 232 katika kura za wajumbe ambazo ndiyo hutumika kumbaini mshindi wa urais Marekani.
Chris Christie alisema nini?
Bwana Christie amesema mara nyingi timu ya Trump imekuwa ikijadili wizi wa kura "ikiwa nje ya mahakama, lakini wakifika mahakamani hawazungumzi lolote kuhusiana na hoja hiyo".
"Nimekuwa mfuasi wa Trump. Nimempigia kura mara mbili. Lakini uchaguzi una matokeo yake na hatuwezi kuendelea kuonesha kwamba hakuna kilichotokea ilihali kinaonekana wazi."
Bwana Christie alikuwa gavana wa kwanza kumuidhinisha Trump kama mgombea wa urais mwaka 2016. Pia alimsaidia rais katika maandalizi yake ya kukabiliana na mpinzani wake Joe Biden kwenye mdahalo wa urais mapema mwaka huu.
Jumapili wabunge wengine wa Republican walimtaka rais Trump kukiri kuwa ameshindwa.
Gavana wa Maryland Larry Hogan ameiambia CNN Jumapili, hatua ya timu ya Trump kuendelea kupinga matokeo ya uchaguzi "imeanza kuonesha chama cha Republican kama kisichokuwa na maana".
Katika ujumbe wa Twitter, Gavana Hogan amesema Bwana Trump aache "kucheza gofu na kukubali kuwa ameshindwa".
Kipi kinachoendelea kwa Biden?
Hatua ya rais kukataa kushindwa imekanganya mchakato wa kawaida wa kupokezana madaraka unaofuata baada ya uchaguzi.
Joe Biden anatarajiwa kuchagua baraza lake la mawaziri kwa mara ya kwanza Jumanne, amesema Ron Klain, chaguo la rais mteule kama Mkuu wa wafanyakazi katika Ikulu.
Akizungumza na televisheni ya ABC Jumapili, Bwana Klain alitoa wito kwa utawala wa Trump kufanikisha mabadilishano na madaraka.

Chanzo cha picha, Reuters
Inasemekana kuwa timu ya kampeni ya Biden inajiandaa kwa sherehe ya kuapishwa kwa rais huyo mteule itakayofanyika Januari 20, lakini idadi ya watakao hudhuria sherehe hiyo itakuwa ndogo kwasababu ya mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya corona.












