Uchaguzi Marekani 2020: Biden apata ushindi katika jimbo la Georgia na kuimarisha ushindi

Iliyochapishwa

Rais mteule wa Marekani Joe Biden amepata ushindi katika jimbo la Georgia, kulingana na makadirio ya BBC, akiwa ni mgombea Mdemocratic wa kwanza kufanya hivyo tangu 1992.

Ushindi huo unaimarisha ushindi wa Bw Biden, na kumpa jumla ya kura 306 za wajumbe, ambazo mfumo wa Marekani unazitumia kumchagua rais wa nchi hiyo.

Rais Donald Trump anakadiriwa kupata ushindi katika jimbo la North Carolina, na kufikia kura 232 za wajumbe.

Bw Trump, ambaye bado hajakubali kushindwa, kwa mara ya kwanza ameashiria uwezekano kuwepo kwa utawala mpya mwezi Januari.

Akionekana mtaratibu na mnyonge, badaye aliashiria kushindwa kwake wakati alipokuwa akizungumza na kikosi kazi chake cha virusi vya corona katika White House, ambapo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa rais huyo kuonekana hadharani tangu taarifa za makadirio ya kushindwa kwake zilipoanza kutolewa na vyombo vya habari vya Marekani.

Wakati nchi ikikabiliwa na ongezeko la mlipuko wa Covid-19, Bw Trump amesema hawezi kutoa agizo la kukaa nyumbani kukabiliana na virusi, akiongeza kuwa : '' kwa lolote litakalotokea siku zijazo, hakuna anayejua utawala gani utakaokuwep: Ninadhani muda utaeleza ."

Rais Trump, ambaye hakumtaja kwa jina Bw Biden, hakukubali maswali kutoka kwa waandidhi wa habari. Shinikizo linaendelea kongezeka dhidi ya Bw Trump , Mrepublican, akibali ushindi wa Bw Biden na kusaidia kurahisisha kipindi cha mpito cha kupokezana utawala kutoka kwa rais mmoja kuelekea mwingine.

Matokeo katika jimbo la Georgia na North Carolina yalikuwa ni ya mwisho kukadiriwa katika mbio za kuelekea ikulu ya White House. Kura za wajumbe za Bw Biden zimekuwa sawa na hesabu ya Bw Trump aliyoipata katika ushindi dhidi ya Hillary Clinton mwaka 2016. Wakati huo Bw Trump aliuelezea ushindi huo kama "wa kishindo".

Rais Trump aliwasilisha madai ya kisheria katika majimbo muhimu na kutoa madai yasio na ushahidi ya wizi mkubwa katika uchaguzi . Lakini juhudi zake zilirudishwa nyuma mara tatu Ijumaa:

  • Katika jimbo la Arizona, timu yake ilifuta madai ya kisheria ya kutaka tathmini upya ya masanduku ya kura zilizopigwa katika siku ya uchaguzi baada ya kubainika wazi kuwa ushindi wa hasimu wake aulikuwa wa wazi. Madai hayo yalitolewa kwa misingi ya dai kuwa kura halali zilikataliwa.
  • Katika jimbo la Michigan, jaji alikataa ombi la waangalizi wawili wa kura Warepublican -ambao walidai kulikuwa na wizi katika kaunti ya Wayne County - kuzuwia uhalalishwaji wa matokeo ya uchaguzi katika eneo Detroit
  • Katika majimbo ya Philadelphia, Pennsylvania, maafisa wa kampeni ya Trump waliomba vifurushi kadhaa vya kura zilizopigwa kwa njia ya posta zisikubalike lakini ombi lao lilikataliwa.

Kuhesabiwa kwa mikono kwa kura kunatarajiwa kufanyika katika jimbo la Georgia kwasababu wagombea hao wamezidiana kiwango kidogo sana cha kura, lakini maafisa wa Biden wanasema kuwa hawatarajii kubadilika kwa matokeo katika jimbo hilo.

Unaweza pia kusoma:

Maafisa wa Biden wanataka apewe maelezo

Huduma za utawala nchini marekani (GSA), ambalo ni shirika la serikali lenye jukumu la kuanza mchakato wa kipindi cha mpito, bado halijamtambua Bw Biden na mgombea mwenza Kamala Harris kama washindi.

Wakati huo huo, maafisa wa Biden bado hawajapata uwezo wa kupata taarifa za siri za usalama, mashirika ya kitaifa na pesa zinazohitajika kuhakikisha kunakuwepo na urahisi wa kukabidhiana madaraka baina yake na Trump. Msemaji wa Biden Jen Psaki alisema kuwa ukosefu wa taarifa hizi unaweza kuathiri uwezo wa Bw Biden wa kuongoza.

"Unahitaji taarifa zilizofika kwa wakati halisi ili kukabiliana na mzozo wa muda huo ," alisema hayo akizungumzia athari za janga la virusi vya corona . "Ni muhimu kwamba timu yetu ya wataalamu wapatiwe uwezo huo ".

Akiongezea kauli yake kuhusu miito hiyo, mkuu wa zamani wa wafanyakazi wa Trump, John Kelly, alisema kuwa kuchelewa kuanza kwa kipindi cha mpito cha kupokezana madaraka kunaathiri usalama wa taifa. ''Sio mchakato ambao unaanzia kutoka sifuri hadi 1,000 kwa saa'', aliliambia gazeti la Politico.

Mapema , kikundi cha maafisa wa zamani wa usalama 150 kiliitaka GSA kumtambua rasimi Bw Biden ili waweze kupata taarifa kuhusu "masuala muhimu na ya haraka ya usalam wa taifa ". Idadi ndogo lakini inayoendelea kuongezeka ya Warepublican pia wanaunga mkono miito ya kupewa kwa taarifa za kiintelijensia kwa rais mteule.

Trump anaendelea kupinga matokeo ya uchaguzi

Bw Trump aliendelea kupinga matokeo ya uchaguzi kwa msururu wa tweet Ijumaa , bila kutoa ushahidi wa madai yake ya wizi. Pia alisema kuwa huenda akajiunga na wafuasi wake katika mkutano uliopangwa kufanyika siku ya Jumamosi mjini Washington

Ujumbe wake ulitolewa saa kadhaa baada ya maafisa wa uchaguzi kusema kuwa kura za urais '' zililindwa zaidi kuwahi kushuihudiwa z katika historia ya Marekani'', likiwa ni jipo la moja kwa moja zaidi kutoka kwa maafisa wa shirikisho na majimbo dhidi ya madai ya Trump.

Taarifa ya pamoja ya Alhamisi ilitolewa na baraza la uratibu wa miundombinu ya uchaguzi la serikali - ambalo linawajumuisha maafisa wa ngazi ya usalama wa ndani ya nchi na tume ya usaidizi ya uchaguzi ya Marekani pamoja na maafisa wa ngazi ya jimbo ambao husiamania uchaguzi na wawakilishi wa sekta ya mashine za kupigia kura.

" Uchaguzi wa Novemba 3 ulikuwa ni uchaguzi uliolindwa zaidi katika historia ya Marekani. Sasa hivi, kote nchini, maafisa wa uchaguzi wanatathmini na kuchunguza mara mbili mchakato wote wa uchaguzi kabla ya kukamilisha matokeo," kikundi hicho kilisema.