Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ethiopia yapuuzia wito wa kimataifa kusitisha shambulio la kijeshi
Waziri mkuu wa Ethiopia ameapa kuendelea na shambulio la kijeshi katika jimbo la Tigray - licha ya wito wa kimataifa kumtaka kusitisha zoezi hilo.
Utawala wa Abiy Ahmed unakishutumu chama tawala cha eneo la Tigray, Tigrayan People's Liberation Front (TPLF)- kufanya mashambulio kadhaa katika jeshi.
Na TPLF imejibu kuwa watazika vichwa vyao kwenye mchanga na kupuuzia hatari iliyotolewa.
Wito wa kimataifa wa kutaka Ethiopia kusitisha shambulio hilo umeonekana kupuuziwa.
Joto la mashambulizi likizidi kupamba moto huko Tigray.
Akihutubia kwa njia ya televisheni waziri mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed ametangaza kuwa operesheni ya kijeshi imefanikiwa. Na kuongeza kuwa operesheni hiyo itaendelea.
Serikali ya shirikisho tayari imetangaza hali ya hatari katika jimbo la Tigray kwa kipindi cha miezi sita.
Uwanja wa ndege umefungwa.
Huduma za simu, mtandao na huduma za kibenki zimefungwa kaskazini mwa Ethiopia' katika eneo la Tigray kufuatia ghasia zilizoibuka katika eneo hilo.
Raia walisikia milio ya risasi siku ya Jumatano kutoka maeneo ya pembezoni mwa mji wa Mekelle, eneo ambalo kamanda wa jeshi la taifa yupo.
Mamlaka jijini Addis Ababa zinasema mzozo huo na kundi dogo unaweza kusababisha kuvunja amani ya taifa.
"Hali hii imefikia kiwango ambacho haiwezi kuzuiwa na kudhibitiwa kupitia njia za kawaida za utekelezaji wa sheria," taarifa kutoka ofisi ya Waziri Mkuu ilisema.
Mamlaka za kitaifa pia zimekatiza huduma za umeme, simu na intaneti katika jimbo la Tigray.
Hali ya taharuki kati ya serikali na TPLF, ambayo ilikuwa sehemu ya muungano tawala kabla ya kukosana na Bw. Abiy, imeongozeka katka miezi ya hivi karibuni, huku pande zote mbili zikilaumianakwa kupanga njama ya kutumia nguvu ya kijeshi.
Siku ya Jumanne, bunge la kitaifa lilipendekeza TPLF kutambuliwa kama "shirika la kigaidi."
Bw. Abiy amesema nini?
Waziri Mkuu Abiy amesema washambuliaji "walijaribu kuiba" mali ya kijeshi katika shambulio hulo la siku ya Jumatano asubuhi, akiongeza kuwa "mpaka umevukwa" hatua iliyolazimisha serikali kuu kuchukua hatua ya kijeshi.
Nini kinafanyika Tigray?
Mwandishi wa BBC Tigrinya, Girmay Gebru ameripoti kuwa milio ya risasi ilisikika katika mji kuu wa jimbo la Tigray, Mekelle, mapema Jumatano lakini hali ya utulivu imejea.
Watu sasa wanaendelea na shughuli zao za kawaida lakini magari ya uchukuzi wa umma hayafanyi kazi kwa sababu ya mamlaka katika jimbo hilo na kudhibiti matembezi na pia kufunga anga za eneo hilo, ameongeza ripota wetu.
Benki na ofisi pekee ya ndani ya Ethio Telecom inayomilikiwa na serikali - kampuni pekee ya simu nchini - imefungwa. Shirika la ndege la Ethiopia limesimamisha safari za ndege kwenda eneo hilo.
Mamlaka za Tigray zimesema nini?
Afisa wa eneo hilo amedai kuwa vikosi vya ulinzi wa kitaifa vilivyopelekwa katika eneo hilo vimeungana nao lakini madai hayo hayajathibitishwa.
Wiki iliyopita viongozi wa Tigray walimzuia jenerali aliyetuliwa na Bw. Abiy kuchukua wadhifa mpya , wakisema hana tena mamlaka ya kuchukua hatua kama hiyo.
"Hatutakuwa wa kwanza kupiga risasi na hatutakuwa wa kwanza kufumba macho," Getachew Reda, afisa wa ngazi ya juu wa TPLF, aliambia shirika la habari la AFP wiki iliyopita.
Usiku wa Jumanne, saa kadhaa kabla ya tangazo la bwana Abiy, Wondimu Asamnew, amabaye nai kiongozi mwingine wa ngazi ya juu ya jimbo la Tigray, ameambia AFP kwamba serikali ya kitaifa imekuwa ikiwapeleka wanajeshi katika mpaka wa Tigray - madai ambayo hayajathibitishwa.
Mzozo huu umeytokana na nini?
Rais wa eneo la Tigray, Debrestion Gebremichael, aliwaambia wanahabari siku ya Jumatatu kwamba serikali inapanga kuwashambulia - akidai ilikuwa adhabu kwa kuandaa uchaguzi wake wa bunge la Tigray mnamo Septemba, kinyume na uamuzi wa serikali ya muungano na uamuzi wa bodi ya uchaguzi kuahirisha uchaguzi wote kufuatia kuzuka kwa janga la corona.
Serikali imetaja uchaguzi huo kuwa "haramu". Bodi ya kitaifa ya uchaguzi tangu wakati huo ilisema uchaguzi mkuu unapaswa kukufanyika mwezi Mei au Juni mwaka ujao.
TPLF imeshikilia uongozi wa kisiasa wa Ethiopia kutoka mwaka 1991 hadi 2018, wakati bwana Abiy alipoingia madarakani kufuatia maandamano ya nchi nzima yaliyofanywa na jamii ya Oromo. Tangu wakati huo nguvu ya chama hicho imefifia.
Bwana Abiy, ambaye alipewa tuzo ya Amani ya Nobel Peace mwaka 2019 kwa kumaliza uhasama kati ya Ethiopia na Eritrea, anakabiliwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa jamii yake, huku mapigano ya kikabila yakishuhudiwa katika maeneo kadhaa ya nchi na shutuma kwamba amebadilisha mageuzi ya kisiasa aliyoanzisha, na viongozi wa upinzani wamefungwa tena.