Virusi vya corona: Rais Uhuru Kenyatta apiga marufuku mikutano ya kisiasa kwa siku 60

Iliyochapishwa

Mikutano yote ya kisiasa nchini Kenya sasa imepigwa marufuku ili kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Akizungumza baada ya mkutano wa kuangazia hali ilivyo nchini , rais Kenyatta amesema kwamba kama viongozi ''tumeshindwa kuwaongoza raia kufuata na kuheshimu masharti ya kukabiliana na corona yaliowekwa''.

''Tumefeli kama viongozi kuhakikisha kuwa kuna kutokaribiana na kwamba watu wanavaa barakoa na kuosha mikono mara kwa mara''.

Uhuru Kenyatta hatahivyo amesema kwamba viongozi wa kisiasa wanaweza kuandaa mikutano yao katika kumbi mbali mbali kwa kuhakikisha kwamba wanafuata maagizo ya kukabiliana na ugonjwa huo.

''Ni janga kuona viongozi wakiruhusu hatari ya virusi hivi'' , alisema Uhuru Kenyatta.

''Umma umeacha kufuata masharti yaliowekwa kutokana na viongozi kushindwa kutoa uongozi'' , aliongezea.

''Sisi kama viongozi hatuna budi kujitolea , lazima tuwaonyeshe watu wetu mwelekeo. Kusimama na kusaidia kukabiliana na mlipuko huu''.

Uhuru amesema kwamba maambukizi ya ugonjwa huu yameongezeka kwa asilimia 16 mwezi Oktoba .

''Hii ni mara nne kile kilichokuwepo mwezi Septemba . Siku 38 baadaye ni bahati mbaya kwamba tunaona kwamba idadi ya maambukizi imeongezeka'' ,alisema.

Aidha amesema kwamba mikutano hiyo inapaswa kuwa na thuluthi moja ya idadi ya watu inayofaa kujaza kumbi hizo.

"Ni wapi tulikosea na ni kipi tungefanya tofauti? Masharti makali yalisaidia kushusha maambukizi'' .

''Tumerudisha nyuma yale yote tuliokuwa tumepiga hatua''.

Rais huyo alisema kwamba miezi minane imewafunza Wakenya kwamba lazima wachukue majukumu wao wenyewe kukabiliana na virusi hivyo.

''Nawakumbusha tena kwamba serikali haina uwezo kuangalia tabia ya raia'', alisema.

''Sio kupenda kwangu kufunga uchumi wa nchi, tunataka kuwa wazi . lakini hilo litategemea jinsi raia watakavyochukua hatua dhidi ya virusi hivyo.

Siku ya Jumanne , naibu wa rais William Ruto alitangaza kwamba ameahirisha ziara zake katika kaunti tatu za mashariki kufuatia wasiwasi wa maambukizi ya awamu ya pili .

''Kwasasbu hii , nimeamua kupunguza mikutano yang una umma hadi wakati mwengine'', Ruto alisema katika Twitter.

Alitarajiwa kuzuru Kitui, Machakos na makueni wikendi hii.

Amri ya kutotoka nje

Miongoni mwa mabadiliko hayo mapya ni kubadilisha muda wa masharti ya kutotoka nje kote nchini kutoka saa tano usiku hadi saa nne hadi saa kumi alfajiri.

Kiongozi huyo wa taifa , akichukua hatua hiyo pia alisema kwamba masharti hayo mapya yataanza kutekeleza mara moja kuanzia tarehe 4 Novemba hadi Januari 3 2020.

''Amri ya kutotoka nje inayoendelea kutekelezwa nchini imeongezwa hadi tarehe 3 Januari 2021 na kuanzia usiku wa leo Jumatano, amri hiyo itaanza kutekelezwa kati ya saa nne usiku hadi saa kumi alfajiri'', alisema rais Uhuru Kenyatta.