Waziri Mkuu wa Ethiopia aagiza 'shambulio' la kijeshi

Iliyochapishwa

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ameamuru majeshi kudhibiti hatua za mamlaka katika jimbo Tigray, kufuatia madai ya shambulio dhidi ya kambi ya kijeshi.

Bwana Abiy ameituhumu chama tawala katika eneo hilo,Tigray People Liberation Front (TPLF), kwa kufanya shambulio hilo.

Shambulio hilo limesababisha "mashuhuda wengi kujeruhiwa, na mali kuharibiwa", alisema katika hutuba kupitia televisheni.

Baraza la mawaziri liliweka hali ya hatari katika jimbo hilo kwa miezi sita.

"Hali hii imefikia kiwango ambacho haiwezi kuzuiwa na kudhibitiwa kupitia njia za kawaida za utekelezaji wa sheria," taarifa kutoka ofisi ya Waziri Mkuu ilisema.

Mamlaka za kitaifa pia zimekatiza huduma za umeme, simu na intaneti katika jimbo la Tigray.

Hali ya taharuki kati ya serikali na TPLF, ambayo ilikuwa sehemu ya muungano tawala kabla ya kukosana na Bw. Abiy, imeongozeka katka miezi ya hivi karibuni, huku pande zote mbili zikilaumianakwa kupanga njama ya kutumia nguvu ya kijeshi.

Siku ya Jumanne, bunge la kitaifa lilipendekeza TPLF kutambuliwa kama "shirika la kigaidi."

Bw. Abiy amesema nini?

Waziri Mkuu Abiy amesema washambuliaji "walijaribu kuiba" mali ya kijeshi katika shambulio hulo la siku ya Jumatano asubuhi, akiongeza kuwa "mpaka umevukwa" hatua iliyolazimisha serikali kuu kuchukua hatua ya kijeshi.

Nini kinafanyika Tigray?

Mwandishi wa BBC Tigrinya, Girmay Gebru ameripoti kuwa milio ya risasi ilisikika katika mji kuu wa jimbo la Tigray, Mekelle, mapema Jumatano lakini hali ya utulivu imejea.

Watu sasa wanaendelea na shughuli zao za kawaida lakini magari ya uchukuzi wa umma hayafanyi kazi kwa sababu ya mamlaka katika jimbo hilo na kudhibiti matembezi na pia kufunga anga za eneo hilo, ameongeza ripota wetu.

Benki na ofisi pekee ya ndani ya Ethio Telecom inayomilikiwa na serikali - kampuni pekee ya simu nchini - imefungwa. Shirika la ndege la Ethiopia limesimamisha safari za ndege kwenda eneo hilo.

Mamlaka za Tigray zimesema nini?

Afisa wa eneo hilo amedai kuwa vikosi vya ulinzi wa kitaifa vilivyopelekwa katika eneo hilo vimeungana nao lakini madai hayo hayajathibitishwa.

Wiki iliyopita viongozi wa Tigray walimzuia jenerali aliyetuliwa na Bw. Abiy kuchukua wadhifa mpya , wakisema hana tena mamlaka ya kuchukua hatua kama hiyo.

"Hatutakuwa wa kwanza kupiga risasi na hatutakuwa wa kwanza kufumba macho," Getachew Reda, afisa wa ngazi ya juu wa TPLF, aliambia shirika la habari la AFP wiki iliyopita.

Usiku wa Jumanne, saa kadhaa kabla ya tangazo la bwana Abiy, Wondimu Asamnew, amabaye nai kiongozi mwingine wa ngazi ya juu ya jimbo la Tigray, ameambia AFP kwamba serikali ya kitaifa imekuwa ikiwapeleka wanajeshi katika mpaka wa Tigray - madai ambayo hayajathibitishwa.

Mzozo huu umeytokana na nini?

Rais wa eneo la Tigray, Debrestion Gebremichael, aliwaambia wanahabari siku ya Jumatatu kwamba serikali inapanga kuwashambulia - akidai ilikuwa adhabu kwa kuandaa uchaguzi wake wa bunge la Tigray mnamo Septemba, kinyume na uamuzi wa serikali ya muungano na uamuzi wa bodi ya uchaguzi kuahirisha uchaguzi wote kufuatia kuzuka kwa janga la corona.

Serikali imetaja uchaguzi huo kuwa "haramu". Bodi ya kitaifa ya uchaguzi tangu wakati huo ilisema uchaguzi mkuu unapaswa kukufanyika mwezi Mei au Juni mwaka ujao.

TPLF imeshikilia uongozi wa kisiasa wa Ethiopia kutoka mwaka 1991 hadi 2018, wakati bwana Abiy alipoingia madarakani kufuatia maandamano ya nchi nzima yaliyofanywa na jamii ya Oromo. Tangu wakati huo nguvu ya chama hicho imefifia.

Bwana Abiy, ambaye alipewa tuzo ya Amani ya Nobel Peace mwaka 2019 kwa kumaliza uhasama kati ya Ethiopia na Eritrea, anakabiliwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa jamii yake, huku mapigano ya kikabila yakishuhudiwa katika maeneo kadhaa ya nchi na shutuma kwamba amebadilisha mageuzi ya kisiasa aliyoanzisha, na viongozi wa upinzani wamefungwa tena.